Tafuta

Papa Francisko anaihamasisha familia ya Mungu Amerika ya Kusini kushikamana ili kukabiliana vyema na changamoto mbalimbali za maisha. Papa Francisko anaihamasisha familia ya Mungu Amerika ya Kusini kushikamana ili kukabiliana vyema na changamoto mbalimbali za maisha. 

Papa: Shikamaneni Kukabiliana na Changamoto za Maisha Kwa Imani

Kumbukizi la Miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Mfumo wa Mshikamano wa Kuwaingiza Wakimbizi na Wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi Amerika ya Kusini na Mexico. Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 umechangia kwa kiasi kikubwa kwa nchi mbalimbali Amerika ya Kusini kufunga mipaka yake na hivyo wakimbizi na wahamiaji wengi kuathirika vibaya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, Kuwalinda, Kuwaendeleza na Kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na hatimaye kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, sera na mikakati hii inamwilishwa pia kwenye Makanisa mahalia, ili kuwasaidia watu hawa ambao mara nyingi wanajikuta wakitumbukia katika biashara ya binadamu na viungo vyake; mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo na nyanyaso dhidi ya utu, heshima na haki zao msingi. Imegota miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Mfumo wa Mshikamano wa Kuwaingiza Wakimbizi na Wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi huko Amerika ya Kusini na Mexico ulipozinduliwa. Vatican kunako mwaka 2012 ikashiriki kama mtazamaji maalum. Mshikamano unaosimikwa katika kanuni auni ni muhimu sana katika ulimwengu mamboleo hasa baada ya maambukizi makubwa ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambalo limesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

UVIKO-19 umepelekea mtikisiko mkubwa katika huduma ya afya, ukuaji wa uchumi kitaifa na Kimataifa pamoja na kuharibu umoja na mafungamano ya kijamii. Binadamu akatambua kwamba kwa hakika ni mavumbi, lakini yenye thamani machoni pa Mungu. Wameumbwa kama familia moja ya binadamu inayopaswa kujikita katika: Elimu na malezi ya uaminifu, ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kushirikiana; kwa kulinda na kudumisha amani na maridhiano; kwa kusaidiana na kuondokana na mashindano yasiyokua na mvuto wala mashiko. Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita kutokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, watu wa familia ya Mungu Amerika ya Kusini wamejikuta wakiogelea katika hali mbaya ya maisha na ukata kutokana na sera pamoja na uchumi tenge, hali ambayo imetikisa pia msingi wa maisha na tunu za kifamilia. Watu wengi wamejikuta wakiwa mbali na familia zao pasi na makazi; wajane na yatima. Kumekuwepo na matukio makubwa ya unyanyasi na vipigo majumbani; mauaji ya wanawake; ongezeko la makundi ya kihalifu kitaifa na Kimataifa.

Biashara ya haramu ya silaha; biashara haramu ya dawa za kulevya, biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na kuendelea kushamiri kwa mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Hili ni eneo ambalo limekumbwa na athari kubwa za mabadiliko ya tabia nchi. Yote haya ni mambo ambayo yamechangia makundi makubwa ya watu kuzikimbia nchi na familia zao. Hii ni sehemu ya ujumbe uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya kumbukizi la Miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Mfumo wa Mshikamano wa Kuwaingiza Wakimbizi na Wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi huko Amerika ya Kusini na Mexico. Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 umechangia kwa kiasi kikubwa kwa nchi mbalimbali Amerika ya Kusini kufunga mipaka yake na hivyo wakimbizi na wahamiaji wengi kuathirika vibaya. Watu wasiokuwa na makazi maalum hata katika nchi zao wenyewe wameendelea kukabiliana na hali ngumu ya maisha, kwa kukosa ulinzi na usalama na hata kama hii ni haki yao Kimataifa. Katika matatizo na mateso yote haya, kuna binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu anaendelea kuteseka, haya ni mateso pia ya Kristo Yesu. Kuwanyima watu hawa hifadhi na mahitaji msingi ni kinyume cha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Kuwapokea maana yake ni kutoa fursa kwa wakimbizi na wahamiaji kuingia katika nchi husika kwa njia salama zinazozingatia sheria za nchi; kwa kutoa hati za kusafiria na kuwapatia wakimbizi na wahamiaji nafasi ya kuweza kukutana na kujiunga tena na familia zao. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jumuiya na Mashirika mbali mbali yatasaidia kutoa msaada wa kiutu kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji wanaokabiliwa na hali tete zaidi. Hawa ni watu wanaokimbia vita, nyanyaso na uvunjifu wa haki msingi, utu na heshima ya binadamu, waangaliwe kwa jicho la huruma kwa kupewa hati za muda na huduma makini kadiri ya utu na heshima yao kama binadamu, ili kutoa nafasi kwa watu hawa kukutana na wenyeji wao, ili hatimaye, kuboresha huduma, daima usalama na utu wa mtu, ukipewa kipaumbele cha kwanza kabla hata ya kuangalia usalama wa taifa, sanjari na kuvifunda vyema vikosi vya ulinzi na usalama kwenye mipaka ya nchi.

Baba Mtakatifu anawataka watu wa Mungu katika Ukanda wa Amerika ya Kusini kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Uchafuzi na uharibifu mkubwa wa mazingira umepelekea watu kukosa mahali pa kufanyia shughuli zao za uzalishaji na huduma, kukosa makazi na fursa za ajira. Ulinzi na huduma kwa familia; elimu makini; ulinzi na usalama ni mambo muhimu sana. Wanawake na wasichana wanapaswa kuangaliwa kwa jicho la pekee sana ili kulinda utu, heshima na haki zao msingi sanjari na kuondokana na mfumo dume unaowadhalilisha wanawake. Kuna haja ya kuendeleza mshikamano unaosimamiwa na kanuni auni kama sehemu ya maboresho katika sekta ya elimu ambayo kimsingi imeathirika sana kutokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete ili kupambana na biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo inayodhalilisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Watuhumiwa wafikishwe kwenye vyombo vya sheria na waathirika wahudumiwe kiroho na kimwili.

Changamoto zote hizi anasema Baba Mtakatifu Francisko zinahitaji kushughulikiwa kwa kujenga na kudumisha mshikamano, umoja na udugu wa kibinadamu, ili kuweza kujenga mwingiliano wa uchumi shirikishi, utamaduni na siasa inayozingatia upendo kwa Mungu na jirani; tayari kusimamia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni mwaliko wa kuondokana na vita, kinzani na mipasuko, tayari kuchuchumilia na kuambana misingi ya haki, amani na maridhiano. Utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko, ubinafsi na uchoyo sanjari na upweke ni mambo ambayo yanawatumbukiza watu wengi pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya jamii. Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa kusema kwamba, Mama Kanisa anaendelea kutembea bega kwa bega na watu wa Mungu Amerika ya Kusini, ambao wametambua umuhimu wa kuwa ni Jumuiya inayosimikwa kwenye ukarimu, tayari kusonga mbele katika mchakato wa mshikamano, imani na matumaini thabiti!

Mshikamano 30 yrs
12 June 2021, 15:45