Tafuta

Sherehe ya Fumbo la Ekaristi Takatifu: Kiu ya uwepo endelevu wa Mungu na upendo wake wa daima. Sherehe ya Fumbo la Ekaristi Takatifu: Kiu ya uwepo endelevu wa Mungu na upendo wake wa daima. 

Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Kiu ya Uwepo na Upendo wa Mungu!

Baba Mtakatifu anasema, mkazo hapa ni mahali pa Karamu ya Mwisho! Mahali ambapo waamini wanaweza kumkaribisha Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Waamini kwanza kabisa lazima wawe na kiu ya uwepo wa Mungu katika nyoyo zao, tayari kumkaribisha Kristo Yesu anayekuja kuadhimisha Ekaristi Takatifu pamoja nao kama kielelezo cha upendo endelevu katika maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo. Sakramenti nyingine, kama zilivyo pia huduma zote za Kanisa na kazi za utume, zinaungana na Ekaristi Takatifu na zinaelekezwa kwake. Kwani katika Fumbo la Ekaristi Takatifu mna kila hazina ya maisha ya kiroho ya Kanisa, yaani Kristo Yesu mwenyewe, Mwanakondoo wa Pasaka. Ekaristi Takatifu ndio ishara thabiti na sababu ya hali ya juu kabisa ya ushirika katika uzima wa kimungu na umoja ule wa Taifa la Mungu ambalo unalifanya Kanisa liwepo. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kilele cha tendo la Mungu la kuutakatifuza ulimwengu katika Kristo Yesu na kilele cha tendo la kumwabudu Mwenyezi Mungu wampalo watu Kristo Yesu, na kwa njia yake wampalo Baba katika Roho Mtakatifu. Kwa njia ya adhimisho la Ekaristi Takatifu, waamini wanaungana tayari wao wenyewe na Liturujia ya mbinguni na wanaanza kutangulia kushiriki uzima wa milele Mungu atakapokuwa yote katika wote! Kwa ufupi kabisa, Fumbo la Ekaristi Takatifu ndio jumla na muhtasari wa imani ya Kanisa. Kumbe, namna ya waamini kufikiri hulingana na Fumbo la Ekaristi Takatifu na Ekaristi kwa zamu yake huimarisha namna yao ya kufikiri. Rej. KKK 1324 – 1327.

Baba Mtakatifu Francisko Jumapili tarehe 6 Juni 2021 ameadhimisha Sherehe ya Mwili na Damu Azizi ya Bwana Wetu Yesu Kristo, “Corpus Domini”. Hii ni Sherehe inayowarejesha tena waamini Siku ya Alhamisi Kuu, Mama Kanisa alipokuwa anakumbuka Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Kristo Yesu, alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, yaani Mwili na Damu yake Azizi, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni siku ambayo Sakramenti ya Daraja Takatifu iliwekwa na Kristo Yesu ili kuendeleza sadaka ya Msalaba na huduma ya upendo. Baba Mtakatifu anasema, ni Mitume waliomuuliza Kristo Yesu, wamwandalie wapi ili aweze kula Pasaka pamoja na wanafunzi wake. Baba Mtakatifu anasema, mkazo hapa ni mahali pa Karamu ya Mwisho! Mahali ambapo waamini wanaweza kumkaribisha Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Waamini kwanza kabisa lazima wawe na kiu ya uwepo wa Mungu katika nyoyo zao, tayari kumkaribisha Kristo Yesu anayekuja kuadhimisha Ekaristi Takatifu pamoja nao kama kielelezo cha upendo endelevu katika maisha yao! Baba Mtakatifu anasema yule mwanaume aliyekuwa amechukua mtungi wa maji akawa ni dira na mwongozo kwa Mitume wa Yesu waliokuwa wanatafuta kuzima kiu kwa maji ya uzima. Kila mtu anayo kiu ya: upendo, furaha na mafanikio katika maisha.

Mambo ya dunia kamwe hayawezi kuzima kiu ya maisha ya ndani, bali ni Mwenyezi Mungu peke yake. Mwamini hana budi kutambua kiu ya Mungu katika maisha yake. Atambue kwamba, anamhitaji Mwenyezi Mungu, ili kuonja uwepo na upendo wake wa daima, ili kumsaidia kusonga mbele katika hija ya maisha. Lakini inasikitisha kuona kwamba, kiu ya kumtafuta Mungu inaonekana kuzimika kwa watu wengi. Mwanamke Msamaria awe ni kielelezo cha chemchemi ya matumaini, kwa watu wanaomtafuta Kristo Yesu ili aweze kuzima kiu ya maisha yao ya ndani. Kiu ya uwepo wa Mungu iwasukume waamini kwenda kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka. Bila kiu ya upendo na uwepo wa Mungu, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yanakosa mvuto na mashiko na hivyo kunyauka kama “kigae”. Huu ni mwaliko hata kwa Kanisa kutoridhika na kikundi kidogo cha waamini wanaohudhuria Ibada ya Misa Takatifu. Kanisa halina budi kutoka ili kukutana na watu na hatimaye kuamsha tena kiu ya waamini ya kutaka kujiunga tena na Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, ili waamini waweze kuadhimisha vyema Fumbo la Ekaristi Takatifu, hawana budi kuandaa nyoyo zao, kama ilivyokuwa kwa Mitume waliomwandalia Karamu ya Mwisho kwenye Chumba cha juu. Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu yanahitaji mahali na nyoyo za watu; maneno na vitendo. Kristo Yesu katika hali ya unyenyekevu akiwa amejificha chini ya maumbo ya Mkate na Divai anajitambulisha kwao. Uwepo wa Mungu wakati mwingine, si rahisi sana kuonekana. Ikiwa kama nyoyo za waamini zitaonekana kama ghala ya kutunzia mambo ya kale; nyoyo iliyogubikwa na: giza, uchoyo na ubinafsi, itakuwa ni vigumu sana kutambua uwepo mwanana wa Mungu katika maisha yao. Hii ni fursa ya kupanua wigo wa maisha, ili kumwabudu na kumtukuza Mwenyezi Mungu. Kimsingi hii ndiyo dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Lengo ni kupanga na kutekeleza kwa pamoja mikakati ya shughuli za kichungaji. Kanisa halina budi kuwa ni mahali pa pana zaidi pa kuwakutanisha waamini, huku wakiwa na mikono wazi ili kuonesha ukarimu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Ekaristi Takatifu ni chakula cha mahujaji, waliochoka katika safari ya maisha. Katika Kanisa la watakatifu na wenyeheri, hakuna nafasi hata kidogo kwa wadhambi na wanyonge. Kanisa halina budi kufungua malango yake, ili kusherehekea pamoja kwa kumzunguka Kristo Yesu. Liwe ni Kanisa ambapo watakatifu na wadhambi, wote kwa pamoja wanaweza kuingia na kumsherehekea Kristo Yesu anayemega Mkate wa uzima. Kielelezo cha Kristo Yesu anayemega Mkate ni alama ya Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha imani ya Kanisa. Kristo Yesu ni chakula kilichoshuka kutoka mbinguni, tayari kuwakirimia waja wake maisha mapya. Kristo Yesu anageuka kuwa ni Mwanakondoo wa Pasaka anayeyamimina maisha yake kwa ajili ya wokovu wa walimwengu. Katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, waamini wanamtafakari na kumwabudu Mwenyezi Mungu, chemchemi ya upendo. Kristo Yesu anajimega na kutoa sadaka kwa ajili ya walimwengu.

Ili kuadhimisha na kumwilisha Fumbo la Ekaristi Takatifu katika uhalisia wa maisha, waamini hawana budi kujikita katika upendo kwa Mungu na jirani. Huu ni upendo unaopaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Hii ni changamoto kwa kila mwamini kujimega na kujisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa jirani zao. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kutokana na hali tete ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO- 19, waamini mjini Vatican hawakuweza kufanya Maandamano Makubwa ya Ekaristi Takatifu, kielelezo cha imani yao kwa Kristo Yesu katika Maumbo ya Mkate na Divai. Maandamano makubwa ya Ekaristi ni sehemu ya maadhimisho ya Sherehe ya Mwili na Damu Azizi ya Bwana Wetu Yesu Kristo, “Corpus Domini”. Lengo ni kumshuhudia Kristo Yesu wanayekutana naye kila siku ya maisha, ili kuasha tena ile kiu ya kutaka kukutana na Mwenyezi Mungu katika maisha. Huu ni mwaliko wa kuwafungulia watu nyoyo, ili kuasha kiu na hatimaye kuwashirikisha wengine upendo wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa mahubiri yake, amewataka waamini kuwa na ari na mwamko mpya wa huruma na mapendo; umoja na mshikamano wa kidugu, ili walimwengu waweze kuona kwa njia ya ushuhuda wa waamini upendo wa Mungu usiokuwa na kifani!

Papa Corpus Christi

 

07 June 2021, 15:47