Tafuta

Mwaka wa Kawaida wa Liturujia ya Kanisa unasimikwa katika Mafumbo ya Maisha ya Kristo Yesu anayetembea na waja wake akiwatakatifuza. Mwaka wa Kawaida wa Liturujia ya Kanisa unasimikwa katika Mafumbo ya Maisha ya Kristo Yesu anayetembea na waja wake akiwatakatifuza. 

Papa Francisko: Mwaka wa Kawaida wa Liturujia ya Kanisa!

Mifano iliyotolewa na Kristo Yesu ilikuwa inagusa undani wa maisha ya watu; alikuwa anakazia ukweli wa mambo uliofahamika kwa wasikilizaji wake. Haya ni mambo aliyokuwa anayaibua kutoka katika uhalisia wa maisha yak ila siku! Waamini wanaalikwa kusikiliza Neno la Mungu, kuangalia matukio kwa imani, matumaini na mapendo, ili kuendelea kulishangaa Fumbo la Maisha ya Mungu

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baada ya maadhimisho ya Kipindi cha Pasaka na Sherehe kuu ambazo ni kitovu, amana na chemchemi ya imani, matumaini na mapendo ya watu wa Mungu, Mama Kanisa anaendelea kuadhimisha Kipindi cha Mwaka wa Kanisa. Hiki ni kipindi ambacho Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu anatembea pamoja na kati ya waja wake, huku akiwatakatifuza, ili waweze kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani, unaosimikwa katika: ukweli, umoja, msamaha, uvumilivu, huduma, maadili na mshikamano. Rangi ya Kipindi cha Kawaida cha Mwaka wa Kanisa ni Kijani, alama ya matumaini. Hii ni sehemu ya mabadililo ya Liturujia ya Kanisa yaliyoletwa na Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Hiki ni kipindi ambacho waamini wanahamasishwa kurutubisha imani, matumaini na mapendo; kuboresha mahusiano na mafungamano yao na Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake kwa njia ya Neno la Mungu, Sala na Sakramenti za Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili ya Kumi na Moja ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, tarehe 13 Juni 2021 amesema, kwa njia ya mifano mbalimbali iliyotolewa na Kristo Yesu katika mahubiri yake, Jumapili hii, Kanisa linarejea tena katika Kipindi cha Mwaka wa Kanisa. Mifano iliyotolewa na Kristo Yesu ilikuwa inagusa undani wa maisha ya watu; alikuwa anakazia ukweli wa mambo uliofahamika kwa wasikilizaji wake. Haya ni mambo aliyokuwa anayaibua kutoka katika uhalisia wa maisha yak ila siku! Huu ni mwaliko kwa waamini kusikiliza kwa makini Neno la Mungu, kuangalia matukio mbalimbali kwa jicho la imani, matumaini na mapendo, ili kuona na kuendelea kulishangaa Fumbo la Maisha ya Mungu.

Haya ni matukio ambayo yanaambatana kuficha uwepo wa Fumbo la Mungu katika maisha ya waja wake. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufungua macho yao ya imani na kuanza kumtafuta Mungu katika kazi yake ya uumbaji kama ambavyo alipenda kusema Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Mama Kanisa takatifu huchukulia wajibu wake kuadhimisha kwa kumbukumbu takatifu kazi ya ukombozi ya Bwanarusi wake aliye Mungu katika siku zilizopangwa katika mwenendo wa mwaka mzima. Kanisa linaadhimisha Jumapili, “Dominika” yaani “Siku ya Bwana”. Hii ni Siku ya Mwenyezi Mungu alipokamilisha kazi ya uumbaji na kujipumzisha. Ni Siku ya Kristo Yesu kwa sababu Kanisa linakumbuka Ufufuko wale uletao uzima wa milele. Ni Siku ya Kanisa kwa sababu waamini wanakusanyika kuadhimisha Liturujia ya Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu, tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.

Jumapili ni siku ya Binadamu kwa sababu, hii inapaswa kuwa ni siku ya mapumziko kwa walio wengi. Ni siku ya kutafakari kuhusu mambo ya nyakati! Katika mzunguko wa mwaka mzima Mama Kanisa anakunjua Fumbo la Kristo Yesu: tangu Umwilisho na kuzaliwa; hadi kupaa mbinguni, mpaka siku ya Pentekoste na kungojea kwa tumaini lenye heri kurudi kwake, ili kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho.  Ni katika muktadha huu, Kanisa huwafungulia waamini wake utajiri na uweza wa mastahili ya Bwana wake. Kwa njia hii uwepo wa mafumbo haya unakuwapo kwa nyakati zote, ili kutoka humo waamini waweze kuchota na kujazwa neema ya wokovu. Kwa kuadhimisha katika mzunguko huo wa kila mwaka mafumbo ya Kristo Yesu, Kanisa humheshimu kwa upendo mkuu Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa; huwakumbuka watakatifu na mashahidi wa imani. Kumbe, Mama Kanisa katika vipindi mbalimbali vya Mwaka wa Kanisa na kadiri ya utaratibu wa Kimapokeo, linatimiza wajibu wake wa kuwakomaza waamini kwa njia ya matendo ya kiroho na kimwili; mafundisho, sala pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili; toba na wongofu wa ndani! Rej. SC 102 -105.

Mwaka wa Kanisa

 

13 June 2021, 14:45