Tafuta

Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya aafya ya binadamu yanapaswapia kuzingnatia mahitaji ya mtu mzima: akili, mwili na roho. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya aafya ya binadamu yanapaswapia kuzingnatia mahitaji ya mtu mzima: akili, mwili na roho. 

Mchakato wa Maboresho ya Afya: Uzingatie: Akili, Mwili na Roho!

Baba Mtakatifu anasema, Nafsi, Mwili na Roho ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana katika uwepo wake. Milango ya fahamu inamwezesha mwanadamu kuguswa na mahangaiko ya jirani zake, kuwa na huruma, unyenyekevu na upole unaosimikwa katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kielelezo kwamba, mambo yote haya yanategemeana na kukamilishana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anapenda kuchukua fursa hii, kuwashukuru wale wote wanaofanya kazi zao usiku na mchana, ili kupambana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Ugonjwa huu ni changamoto kubwa katika mchakato wa kudumisha mshikamano na udugu wa kweli wa kibinadamu. Huu ni wito wa kuendelea kutafakari kuhusu miundombinu ya huduma ya afya, ili kuhakikisha kwamba, wagonjwa wote bila upendeleo wanapata huduma makini! Wote wakiwa wameungana pamoja, wanapania kujenga mkakati wa kulinda zawadi ya uhai! #UniteToPrevent. Mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni katika Kristo Yesu Mkombozi na Mwokozi ambamo sura ya kimungu iliyoharibiwa na mtu kwa dhambi imerudishiwa uzuri wake wa asili na kuongezewa utukufu kwa neema ya Mwenyezi Mungu. Sura ya kimungu iko ndani ya kila mwanadamu. Inang’ara katika muungano wa watu kwa mfano wa umoja wa Nafsi tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Mwanadamu kwa kujaliwa roho isiyokufa, ni kiumbe peke yake duniani ambacho Mwenyezi Mungu amekitaka kwa ajili yake mwenyewe. Tangu kutungwa mimba kimekusudiwa na heri ya milele.

Binadamu hushiriki nuru na nguvu ya Roho wa Mungu. Kwa akili yake anaweza kutambua mpango wa vitu vilivyoanzishwa na Muumba. Anaweza kwa uhuru wake kujiongoza kufikia jema lake la kweli. Anapata ukamilifu wake katika kutafuta na kupenda kile kilicho kweli na chema. Kwa sababu ya roho yake na nguvu zake za kiroho, za akili na utashi, binadamu amekirimiwa uhuru, ishara inayopendelewa ya sura ya kimungu! Rej. KKK 1703-1705. Ni katika muktadha huu, Baraza la Kipapa la Utamaduni kwa kushirikiana na Mfuko wa “Care Foundation”, Mfuko “Faith Foundation” pamoja na Mfuko wa “Stem Foundation” kuanzia tarehe 6 hadi 8 Mei 2021 limekuwa likifanya mkutano kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Mkutano huu umenogeshwa na kauli mbiu “Kuchunguza Akili, Mwili na Roho jinsi ubunifu wa mifumo mipya ya mawasiliano inavyo boresha afya ya binadamu”. Mkutano huu umejielekeza zaidi katika maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika tiba ya mwanadamu. Umezungumzia pia nafasi ya imani katika mchakato wa tiba kwa magonjwa yanayomsibu mwanadamu, bila kusahau tasaufi ya maisha yake ya kiroho.

Huu umekuwa ni mkutano wa tano, ambao umetoa fursa kwa washiriki wake kuchambua na kupembua kwa umakini mkubwa mada hizi, hususan katika kipindi hiki ambacho Jumuiya ya Kimataifa inakabiliana na janga kubwa la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Hapa wajumbe wamekazia umuhimu wa kuunganisha akili, mwili na roho katika tiba na kinga ya magonjwa yanayomwandama mwanadamu; utu, heshima na haki zake msingi zikipewa kipaumbele cha kwanza anasema Kardinali Gianfranco Ravasi, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Utamaduni. Kumbe, ni muhimu sana kwa wataalam na wafanyakazi katika sekta ya afya, pamoja na watafiti katika magonjwa ya binadamu kutambua na kuthamini mwingiliano huu unaomuunda mtu mzima: kiroho na kimwili. Katika mapambano dhidi ya maambukizi makubwa ya Virusi vya Ugonjwa wa Korona, UVIKO-19, juhudi kubwa zimeelekezwa kwenye tiba ya mwili na kusahau akili na maisha ya kiroho pia yanapaswa kushughulikiwa kikamilifu kama sehemu ya mtu mzima: mwili na roho. Jambo la msingi hapa ni kwa wataalam kuendelea kufanya tafiti makini za kifalsafa na kitaalimungu ili kusaidia maendeleo makubwa yaliyopatikana kutokana na sayansi na teknolojia ya tiba ya afya ya binadamu.

Sayansi na Taalimungu imsaidie mwanadamu kupambana na shida, changamoto na fursa zinazojitokeza. Hii ni changamoto anasema Kardinali Gianfranco Ravasi, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Utamaduni. Ni katika muktadha huu, mkutano huu umewashirikisha wadau kutoka katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu, ili kuondokana na kishawishi cha kutaka kumgawa mwanadamu kwa kuangalia changamoto za kiafya peke yake! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa washiriki wa mkutano huu, amekazia kuhusu: Nafsi, Miili na Roho kama anavyofafanua Mtakatifu Paulo Mtume, 1The 5:23. Muungano huu ni sehemu ya imani ya Kanisa Katoliki mintarafu ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Anakiri pia mchango mkubwa ya sayansi ya tiba ya mwanadamu pamoja na kuonesha umuhimu wa sala na tafakari katika maisha ya mwanadamu. Sayansi ya tiba ya mwanadamu, tafiti za viini tete na maadili ni mambo yanayopaswa kwenda sanjari.

Baba Mtakatifu anasema, Nafsi, Mwili na Roho ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana katika uwepo wake. Milango ya fahamu inamwezesha mwanadamu kuguswa na mahangaiko ya jirani zake, kuwa na huruma, unyenyekevu na upole unaosimikwa katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kielelezo kwamba, mambo yote haya yanategemeana na kukamilishana. Mapokeo ya Wakristo na Wayahudi yanaonesha uwepo wa “Roho” Mwanadamu kwa kujaliwa roho isiyokufa, ni kiumbe peke yake duniani ambacho Mwenyezi Mungu amekitaka kwa ajili yake mwenyewe. Tangu kutungwa mimba kimekusudiwa na heri ya milele.

Kwa upande wake, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika ujumbe wake amekazia umuhimu unaozingatia masuala msingi ya ikolojia, uchumi na maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa ajili ya kuwekeza katika tiba na afya ya mwanadamu. Yote haya ni mambo yanayounganishwa na mtu nafsi ambao ni utambulisho wake. Ubinafsi na uchoyo ni mambo ambayo yamesababisha mateso na hali ya kukata tamaa katika maisha ya mwanadamu. Kuna baadhi ya watu wamejitwalia “ubabe” kwa kujipatia kipaumbele cha kwanza kwa kuwatweza binadamu wengine kama kwamba, “wao ni sawa na soli ya kiatu”. Uwezo wa mwanadamu kufikiri na kutenda unamtofautisha na viumbe wengine wote. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya tiba ya mwanadamu hayana budi pia kuzingatia maisha na afya ya viumbe hai wengine wote. Miundombinu ya kijamii na kitamaduni; kijiografia na kiuchumi ina athari kubwa katika maisha; kwa kufikiri na kutenda. Kanuni maadili, utu wema, upendo na mshikamano wa kweli ni mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa. Maisha ya kiroho yanapaswa kupewa msukumo wa pekee katika mchakato wa maendeleo ya binadamu.

Akili Mwili na Roho

 

 

16 June 2021, 15:55