Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 7 Juni 2021 amekutana na Jumuiya ya  "San Luigi dei Francesi". Maisha ya Kijumuiya na Changamoto zake! Baba Mtakatifu Francisko tarehe 7 Juni 2021 amekutana na Jumuiya ya "San Luigi dei Francesi". Maisha ya Kijumuiya na Changamoto zake! 

Papa Francisko Kuhusu Maisha ya Kijumuiya na Changamoto Zake!

Papa Francisko amegusia: Umuhimu wa Jumuiya kujikita katika tunu msingi za Kiinjili, Udugu na mshikamano. Mtakatifu Yosefu awe ni mfano bora wa ukarimu, upendo na sadaka Waepukane na kishawishi cha kuunda makundi na badala yake, wajisadake kwa ajili ya huduma na kwamba, wamependelewa na Mwenyezi Mungu hata akawateuwa na kuwaweka wakfu kuwa ni Mapadre!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Chuo Kikuu cha “San Luigi dei Francesi” inaundwa na mapadre pamoja na wanafunzi kutoka nchini Ufaransa wanaosoma mjini Roma na kufanya utume wao mjini Vatican. Kunako miaka 1400 watu wa Mungu kutoka nchini Ufaransa waliamua kununua ardhi kwa ajili ya matumizi ya raia wao wanapokuwa mjini Roma kwa shughuli mbalimbali kuanzia mwaka 1589. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 7 Juni 2021 amekutana na kuzungumza na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha “San Luigi dei Francesi”. Katika hotuba yake, amegusia umuhimu wa Jumuiya kujikita katika tunu msingi za Kiinjili, Udugu na mshikamano wa kibinadamu. Mtakatifu Yosefu awe ni mfano bora wa ukarimu, upendo na sadaka ya mtu binafsi. Waepukane na kishawishi cha kuunda makundi ndani ya jumuiya na badala yake, wajisadake kwa ajili ya huduma na kwamba, wamependelewa na Mwenyezi Mungu hata akawateuwa na kuwaweka wakfu kuwa ni Mapadre.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika ulimwengu mamboleo, ubinafsi, uchoyo na tabia ya watu kutaka “kujimwambafai” pamoja na kuwageuzia wengine kisogo, yamekuwa ni mambo ya kawaida kabisa. Lakini, Jumuiya ya Chuo Kikuu cha “San Luigi dei Francesi” iliyoko katikati ya mji wa Roma inapaswa kushuhudia tunu msingi za Kiinjili zinazofumbatwa katika udugu na mshikamano wa kibinadamu, hasa nyakati za shida na magumu ya maisha. Kwa njia ya maisha na wito wao wataweza kujisikia kuwa waaminifu kwa upendo wa Mungu pamoja na kuonja uwepo wake wa karibu. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu katika maisha na utume wake. Anasema Mtakatifu Yosefu alikuwa ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi.

Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa busara na haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa na Malaika wa Bwana. Mtakatifu Yosefu ni mtu wa imani thabiti, mpendelevu na kielelezo cha uaminifu, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Mungu katika maisha na historia yake. Waamini wanaalikwa kwa njia ya Mtakatifu Yosefu kurejea katika maisha ya kawaida kwa kujikita katika ukarimu, upendo na sadaka binafsi. Mapadre watambue udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu kama sehemu ya taalimungu. Mapadre wanaojigamba kwamba, wamesimama imara, mara nyingi wanaishia pabaya! Mapadre watambue mapungufu yao na kumshirikisha Kristo Yesu, ili aweze kuwatia nguvu ya kusimama na kuendelea na safari, hawa wanaweza “kupeta katika maisha”. Maisha ya kijumuiya mara nyingi yanakabiliwa na kishawishi cha baadhi ya wanajumuiya kuunda vikundi vinavyowafanya kujifungia katika ubinafsi wao; kwa kujitenga na wengine na hivyo kuanza kuwasema vibaya. Hivi ni vikundi vyenye tabia ya kuwakosoa wakuu wa Jumuiya na kukosa imani nao, kwa kudhani kwamba, wao ni wenye akili sana na uwezo mkubwa.

Hiki ni kishawishi cha watu wote, lakini, kamwe hali hii haipaswi kuachwa iendelee kama ilivyo! Huu ni mwaliko wa kuwapokea na kuwakaribisha wengine katika maisha kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Udugu wa kibinadamu unapaswa kumwilishwa katika ukweli, kwenye mahusiano ya dhati na maisha ya sala, ili kujenga na kudumisha jumuiya inayosimika mizizi yake katika furaha na upendo wa Kiinjili. Wakeri wajenge tabia ya kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Baba Mtakatifu anawataka wanajumuiya hawa kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu furaha na mwanga wa Injili, ili kuwakirimia wengine, Injili ya matumaini. Masomo na majiundo makini kutoka vyuo mbali mbali mjini Roma ni sehemu ya mchakato wa maandalizi yao ya kuwa Mapadre, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha. Wajitahidi kusoma alama za nyakati kwa kuwa na harufu ya kondoo. Hawa ni viongozi wa Kanisa wenye uwezo wa kuishi vyema na waamini wao, tayari kufurahia wanapofurahia, kucheka wanapocheka; kulia na kulia na wale waoteseka. Mwenyezi Mungu na jirani wapewe kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wao. Dhana ya maisha na utume wa Kipadre hauna budi kwenda mintarafu mahusiano na watu wa Mungu katika ujumla wao. Wakumbuke daima chanzo cha historia ya wito na maisha yao ya Kikasisi!

Maisha yao yote yajielekeze katika huduma inayotolewa na Mama Kanisa. Wawe ni watu wanaothubutu katika maisha, kwani kwa njia ya Kristo Yesu wanaweza kufanya mambo makubwa katika maisha. Wawe ni watu wa shukrani kwa kuteuliwa na kuwekwa wakfu na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya huduma kwa jirani na kwa Mwenyezi Mungu. Wawe ni mafuta ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu waishi na kutenda kama Wafuasi wamissionari wa Kristo Yesu. Ucheshi wa Mapadre ni chemchemi ya utakatifu wa maisha. Katika maadhimisho ya Miaka 150 tangu Mtakatifu Yohane Maria Vianney alipofariki dunia, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akatangaza Maadhimisho ya Mwaka wa Mapadre Duniani. Huu ukawa ni muda wa kufanya tafakari ya kina kuhusu: Ukuu, Utakatifu, Wito na Maisha ya Kipadre ndani ya Kanisa. Mapadre walikumbushwa kwamba, utambulisho na uhuru wa wafuasi wa Kristo Yesu ni mambo makuu mawili yanayowawezesha hata Mapadre katika maisha na utume wao, kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani.

Katika Maadhimisho ya Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney, Baba Mtakatifu Francisko aliwaandikia Mapadre wote duniani, barua ya upendo na mshikamano wa kibaba, akiguswa na furaha ya huduma inayotolewa na Mapadre sehemu mbali mbali za dunia, kila kukicha! Hawa ni mapadre ambao wengine wamechoka na kudhohofu kwa afya mbaya na changamoto za maisha; kuna baadhi yao wametumbukia katika mateso na mahangaiko makubwa ya ndani kutokana na huduma yao kwa familia ya Mungu. Mapadre watambue karama na mapungufu yao katika maisha; magumu, changamoto na fursa mbalimbali zinazojitokeza katika maisha, huku wakionesha moyo wa upendo. Waendelee kuwasha moto wa matumaini katika maisha na utume wao. Wasikate tamaa wala kutumbukia katika upweke hasi. Baba Mtakatifu amewaomba wanajumuiya hawa kumkumbuka na kumwombea katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro! Hii ni dhamana na wajibu mzito kwa ajili ya Kanisa la Kristo. Ushuhuda wa maisha na utume wa Kipadre ni mambo msingi katika mchakato wa uinjilishaji. Mapadre wajitahidi kuwa ni watu wenye furaha, wadumifu katika maisha na utume wao; wajifunze kuishi na watakatifu na mashuhuda wa Injili bila kuwasahau wadhambi wanaowachangamotisha kuchchumilia na kuambata utakatifu wa maisha. Ili kwamba, wanapohimisha huduma yao mjini Vatican, wakumbukwe kwa ucheshi, uwepo na huduma yao makini inayosimikwa katika utakatifu wa maisha.

San Luigi

 

 

07 June 2021, 15:25