Tafuta

Papa Francisko Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala: Kristo Yesu ni kieleleszo na roho ya kila sala! Papa Francisko Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala: Kristo Yesu ni kieleleszo na roho ya kila sala! 

Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala: Yesu Ni Kielelezo na Roho ya Sala

Maandiko Matakatifu yanaonesha jinsi ambavyo Yesu alivyotoa kipaumbele cha kwanza katika ujenzi wa mahusiano na wafuasi wake. Hata katika dhambi ya mauti, bado Kristo Yesu anaendelea kusali kwa ajili ya waja wake kama ushuhuda wa kazi ya ukombozi aliyoitekeleza kwa mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu. Hiki ni kiini cha upendo na usalama wa Kristo Yesu kwa waja wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Sala ni kuinua moyo kwa Mwenyezi Mungu au maombi ya mambo mema kwa Mungu. Sala inapaswa kububujika kutoka katika vilindi vya moyo mnyenyekevu ili kukoleza toba na wongofu wa ndani. Mwanadamu ni mwombaji mbele ya Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko bado anaendelea na Katekesi kuhusu Fumbo la Sala. Ameendelea kujikita katika: Sala na Utatu Mtakatifu kwa kujielekeza zaidi kwa Roho Mtakatifu anayewafunulia watu kumhusu Kristo Yesu. Roho Mtakatifu anao uwezo wa kuchunguza hata Mafumbo ya Mungu. Ni Mungu peke yake anayemjua Mungu kabisa. Kanisa linamsadiki Roho Mtakatifu kwa sababu ni Mungu na kamwe haliachi kutangaza imani kwa Mungu mmoja: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Kanisa ni Mama, Mwalimu na Shule ya Sala. Imani inapyaishwa kwa njia ya sala na kwamba, kuna mitindo mbalimbali ya sala, ili kuweza kuzungumza na Mwenyezi Mungu kuna: Sala ya Sauti, Sala Fikara au Tafakari na Taamuli. Baba Mtakatifu amekwisha kupembua kuhusu: umuhimu wa utume wa sala na changamoto zake. Kanisa lina dhamana ya kusali na kufundisha namna ya kusali vizuri zaidi. Kanisa ni shule kuu ya sala.

Baba Mtakatifu amekwisha kufafanua kuhusu: Sala ya Taamuli na Mapambano katika Sala ya Kikristo” na kwamba, Sala inataka moyo kwelikweli. Amekwisha kufafanua kuhusu: fadhaa, uzembe na ukavu katika maisha ya sala! Tumaini, Udumifu na Ujasiri katika sala ndiyo mada iliyonogesha Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi yake mara ya mwisho! Kristo Yesu ni kielelezo na roho katika sala ndiyo kauli mbiu iliyonogesha Katekesi yake Jumatano tarehe 2 Juni 2021 kwenye uwanja wa Mtakatifu Damas, mjini Vatican. Wakati wa Karamu ya Mwisho, Kristo Yesu aliwaambia Mitume wake “Nanyi ndinyi mliodumu pamoja nami katika majaribu yangu. Nami nawawekea ninyi ufalme, kama vile Baba yangu alivyoniwekea mimi” Lk 22: 28-29. Akasema, “Simon, Simon, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako” Lk 22: 31-32. Maandiko Matakatifu yanaonesha jinsi ambavyo Kristo Yesu alivyotoa kipaumbele cha kwanza katika mchakato wa ujenzi wa mahusiano na mafungamano na wafuasi wake. Hata katika dhambi ya mauti, bado Kristo Yesu anaendelea kusali kwa ajili ya waja wake kama ushuhuda wa kazi ya ukombozi aliyoitekeleza kwa mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu.

Hiki ni kiini cha upendo na usalama wa Kristo Yesu kwa waja wake. Kabla ya matukio makuu katika maisha na utume wake, Kristo Yesu alijitenga na kwenda faragha ili kusali, kama inavyojionesha kabla ya kuwachagua Mitume wake kumi na wawili, alijikita katika majadiliano na Baba yake wa mbinguni. Kwa uwepo wa Yuda Iskariote, inaweza kuonekana kana kwamba, uteuzi huu, ulikuwa na kasoro kubwa kwani Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti. Lakini, yote haya ni sehemu ya mpango wa Mungu, tangu milele yote. Sala ilikuwa ni njia ya kujenga na kuimarisha urafiki kati ya Kristo Yesu na marafiki zake. Alijifunua kama Mwalimu, rafiki wa kweli na mnyenyekevu wa moyo, daima alipenda kuona toba na wongofu wa ndani kutoka kwa Mitume wake kama alivyofanya kwa Mtakatifu Petro, Mtume. Akamwambia baada ya toba na wongofu wa ndani alipaswa kuwaimarisha ndugu zake katika imani.

Hata baada ya Mtakatifu Petro “kupepetwa kama ngano”, lakini upendo wa Kristo Yesu, uliendelea kudumu na kuimarika, kwa sababu Kristo Yesu aliwataka wafuasi wake kutoa kipaumbele cha kwanza katika fumbo la maisha ya sala. Sala ya Yesu ilikuwa inawafikia walengwa kwa wakati muafaka. Alipenda kujitenga na kuingia faraghani katika undani wa maisha yake ili kuweza kusali. Ni katika muktadha wa utambulisho wake, baada ya kusali kwa faragha, Mtakatifu Petro anajibu swali na kushuhudia kwamba, Yesu ndiye Kristo wa Mungu. Kristo Yesu akaonesha kwamba, angeteswa na kuuwawa lakini atafufuka siku ya tatu. Rej. Lk 9: 18-21. Kwa hakika matukio muhimu katika maisha na utume wa Kristo Yesu, yalinogeshwa na muda wa sala na tafakari ya kina. Kielelezo muhimu cha sala inayopyaisha imani na mwanzo wa maisha na utume wa wafuasi wa Kristo Yesu. Baada ya sala Kristo Yesu aliwafunulia kuhusu mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu! Sala ni chemchemi ya mwanga na nguvu katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini wajenge na kudumisha utamaduni wa kusali daima, wakati wa raha na shida!

Baada ya Kristo Yesu kutangaza kuhusu: mateso, kifo na ufufuko wake baada ya siku nane, aliwatwaa Petro, Yohane na Yakobo akapanda mlimani ili kuomba na katika kusali kwake, akang’ara mbele ya Mitume wake na kuonesha utukufu wa Mwana mpendwa wa Mungu, kielelezo cha mshikamano na mahusiano ya dhati kabisa na Baba yake wa mbinguni. Kristo Yesu alionesha wazi kwamba, yuko tayari kutekeleza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni yaani kukamilisha kazi ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Katika undani na uzito wa sala hii “Sauti ikatoka katika wingu, ikisema, “Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye” Lk 9:35. Yote haya yanadhihirisha kwamba, Kristo Yesu anaendelea kusali na kuwaombea wafuasi wake, kumbe, waendelee kumtumainia na kujiaminisha kwake. Mababa wa Kanisa wanasema, Sala ya Kristo Yesu huifanya sala ya Kikristo kuwa ombi linalofaaa. Yeye ni kielelezo chake, husali ndani yetu na pamoja nasi. Kwa kuwa moyo wa Mwana hutafuta kile tu kinachompendeza Mungu Baba, sala ya wale waliofanywa wana inawezaje kugandamana na zawadi kuliko na Mtoaji? Rej. KKK 2740.

Kristo Yesu husali pia kwa ajili ya watu wa Mungu, badala yao kwa manufaa yao. Maombi yao yote yalikusanywa mara moja tu kwa daima ndani ya kilio chake Msalabani na kusikilizwa na Mungu Baba Mwenyezi katika Ufufuko wake. Ndiyo maana hakomi kuwaombea mbele ya Baba yake wa mbinguni. Kama sala yao imeungana kwa uthabiti na ile ya Yesu, katika matumaini na ujasiri wa kimwana, watapata kile wanachoomba kwa jina lake na hata zaidi ya hiki au kile wanachoomba: Roho Mtakatifu mwenyewe aliye na zawadi zote. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha Katekesi yake kuhusu Kristo Yesu kielelezo na roho katika sala kwa kusema kwamba, hata kama waamini watakuwa wanamung’unya maneno, hata kama sala yao itakuwa haina msingi thabiti wa imani, kamwe wasisite kujiaminisha mbele ya Kristo Yesu. Sala za waamini zikiungana na Sala ya Yesu zinapaa kwenda mbinguni kama moshi wa ubani!

Papa Fumbo la Sala
02 June 2021, 15:48