Tafuta

Papa Francisko amefafanua kuhusu matumaini ya Kikristo katika shida na mahangaiko ya binadamu. Papa Francisko amefafanua kuhusu matumaini ya Kikristo katika shida na mahangaiko ya binadamu. 

Papa Francisko Fadhila ya Matumaini ya Kikristo katika Shida!

Hija ya mwaka 2021 imenogeshwa na kauli mbiu “Ninapokuona wewe, ninaona matumaini.” Hija hii ya maisha ya kiroho, kwa mara nyingine tena imeadhimishwa kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii kama sehemu ya utekelezaji wa itifaki dhidi ya maambukizi ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Matumaini ya Kikristo katika shida na mateso.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Matumaini ni fadhila ya Kimungu inayowawezesha waamini kutamani heri ya Ufalme wa mbinguni na uzima wa milele kwa kutumainia ahadi za Kristo Yesuna kutegemea, siyo nguvu zao wenyewe, bali msaada wa neema ya Roho Mtakatifu kwa sababu Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu katika utekelezaji wa ahadi zake. Kwa njia ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, waamini wanaweza kuhesabiwa haki kwa neema yake ili wapate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama tumaini lao. Fadhila ya matumaini inajibu tamaa ya heri ilivyowekwa na Mungu katika moyo wa kila mtu. Yachota matumaini yanayovuvia matendo ya watu. Huyatakasa ili kuyapanga kwa ajili ya Ufalme wa mbinguni nyakati za upweke. Hufungua moyo katika kungoja heri ya milele. Akielekezwa na matumaini anakingwa na ubinafsi na anaongozwa kwenye furaha itokanayo na mapendo. Matumaini ya Kikristo yanakita mizizi yake katika Heri za Mlimani ambazo kimsingi ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wanafunzi wake. Matumaini ni “nanga ya roho”, hakika na thabiti; ni silaha inayowalinda waamini katika mapambano ya wokovu.

Matumaini ni fadhila ya Kikristo inayojikita katika unyenyekevu na nguvu ya kuweza kusonga mbele katika safari ya maisha, licha ya vikwazo na magumu yaliyopo. Matumaini kwa Mwenyezi Mungu kamwe hayawezi kumdanganya mwamini kwani Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu katika kutekeleza ahadi zake. Mungu ni chemchemi ya furaha na amani mioyoni mwa waja wake. Rej. KKK 1817-1821. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 11 Juni 2021 amewapigia simu washiriki wa maandamano ya Hija ya 43 ya Matembezi ya Miguu kutoka Macerata hadi Loreto, nchini Italia ili kuwatia shime katika hija yao! Hili ni tukio ambalo limefanyika mara tu baada ya kuwasili Mwenge wa Amani alioubariki mwenyewe mara baada ya katekesi yake, Jumatano tarehe 9 Juni 2021 kwenye Uwanja wa Mtakatifu Damas. Hija ya mwaka 2021 imenogeshwa na kauli mbiu “Ninapokuona wewe, ninaona matumaini.” Hija hii ya maisha ya kiroho, kwa mara nyingine tena imeadhimishwa kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii kama sehemu ya utekelezaji wa itifaki dhidi ya maambukizi ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ni hija inayotafakari kuhusu fumbo la maisha ya binadamu! Swali msingi ambalo kila mwamini anapaswa kujiuliza ni ikiwa kama anafanya hija ya maisha yanayosimikwa katika fadhila ya matumaini, au mwamini anatembea pasi kujua mwelekeo au dira sahihi ya maisha yake! Maisha hayana budi kuwa na: dira, wongozo na lengo linalopaswa kufikiwa! Ikumbukwe kwamba, kamwe matumaini hayawezi kumdanganya mtu. Siri kubwa ya kuweza kutembea katika mwanga wa matumaini ni kujenga umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu; kwa kusaidiana wakati wa shida na taabu; kwa kushuhudia Injili ya matumaini kwa wale waliokata na kujikatia tamaa ya maisha. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini kwa wale wasiokuwa na matumaini tena katika maisha. Baba Mtakatifu amewaombea ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Loreto katika safari yao ya maisha, daima wakijisadaka bila ya kujibakiza: mwili na roho. Kamwe wasikate wala kujikatia tamaa! Haya ni matumaini hata kwa wafungwa ambao wanaendelea kutumikia adhabu yao magerezani. Matumaini kwa watu walioshambuliwa na UVIKO-19 na pengine familia nzima kuteketea kabisa!

Umuhimu wa Injili ya matumaini unatokana na maafa makubwa yaliyosababishwa na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambalo limesababisha watu wengi kupoteza maisha katika kipindi cha mwaka mmoja. Takwimu zinaonesha kwamba, hadi kufikia tarehe 12 Juni 2021 maambukizi mapya nchini Italia yalikuwa yamefikia wagonjwa 1, 723. Watu waliofariki kwa UVIKO-19 ni 52. Asilimia ya maambukizi ya UVIKO-19 yamepungua hadi kufikia asilimia 0,81%. Haya yote ni mafanikio ya chanjo dhidi ya UVIKO-19 ambayo imepewa kipaumbele cha kwanza kitaifa. Sasa Italia wameanza kuwachanja wanafunzi ili waweze kufanya mitihani yao wakiwa madarasani kwa kuzingatia usalama wa maisha yao. Maandamano ya Hija ya 44 ya Matembezi ya Miguu kutoka Macerata hadi Loreto yataadhimishwa Jumamosi tarehe 11 Juni 2022, kwa kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Loreto, daima wakiendea kuboresha na kupyaisha imani, matumaini na mapendo!

Fadhila ya Matumaini
13 June 2021, 15:24