Tafuta

Papa Francisko anawahimiza Wakristo kujikita katika mchakato wa uekumene wa sala na huduma kwa watu wa Mungu. Papa Francisko anawahimiza Wakristo kujikita katika mchakato wa uekumene wa sala na huduma kwa watu wa Mungu. 

Papa: Dumisheni Mchakato wa Uekumene wa Sala na Huduma

Upendo ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaosimikwa katika uhalisia wa maisha ya watu, kwa kutambua kwamba, wao ni ndugu wamoja licha ya tofauti zao msingi. Wanaunganishwa na imani moja kwa Kristo Yesu hata kama wanashambuliwa na umaskini wa hali na kipato, jambo la msingi kwamba, wao ni ndugu wa Baba mmoja naye ndiye Mwenyezi Mungu. Uekumene wa Sala.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kikundi cha Wanaharakati cha "John 17 Movement" kilianzishwa na Joe Tosin ili kukoleza mchakato wa umoja na mafungamano ya Kikanisa kutoka katika sakafu ya nyoyo zao, kwa kuunganishwa na upendo wa dhati unaosimikwa katika mchakato wa upatanisho. Shughuli mbalimbali zinazofanywa na kikundi cha wanaharakati hawa zinapania kuwa ni ushuhuda wa umoja na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, kama kielelezo na mfano bora wa kuigwa. Kuna mambo mengi yanayowaunganisha Wakristo ikilinganishwa na yale yanayowagawa na kuwasambaratisha. Wanaharakati hawa wanataka kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa dhati kama ambavyo unafafanuliwa na Kristo Yesu katika sala yake ya Kikuhani anavyosali kwa kusema: “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi.”  Yn 17: 21-23.

Kristo Yesu ni kiungo muhimu sana kinachowafungamanisha watu wa Mungu, ili waweze kumwamini Kristo Yesu, aliyetumwa na Baba wa milele hapa duniani. Kikundi cha Wanaharakati cha "John 17 Movement" ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika sala na huduma makini kwa watu wa Mungu, kwa kusikilizana na kupendana kama Kristo Yesu alivyo waamuru wafuasi wake. Huu ni mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika upatanisho, ili wote wawe wamoja, kwa kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa upendo kati yao, unawaongoza na kuwaelekeza kumpenda Mungu na kumpatia kipaumbele cha kwanza. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 9 Juni 2021 amekiandikia Kikundi cha Wanaharakati cha "John 17 Movement" ujumbe wa matashi mema, akiwapongeza kwa kukutana na kusali pamoja kama Wakristo. Yesu katika sala yake ya Kikuhani anasema, “Na sasa naja kwako; na maneno haya nayasema ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao. Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.” Yn 17: 13-17.

Baba Mtakatifu anakaza kusema upendo ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaosimikwa katika uhalisia wa maisha ya watu, kwa kutambua kwamba, wao ni ndugu wamoja licha ya tofauti zao msingi. Wanaunganishwa na imani moja kwa Kristo Yesu hata kama wanashambuliwa na umaskini wa hali na kipato, jambo la msingi kwamba, wao ni ndugu wa Baba mmoja naye ndiye Mwenyezi Mungu. Hata kama taalimungu inahitajika ili kufafanua upendo, lakini, kimsingi upendo unamwilishwa katika uhalisia wa maisha na kuendelea kurutubishwa na urafiki wa kweli na udugu, chachu makini inayoweza kuleta mabadiliko ulimwenguni. Watu wanapokutana kama ndugu wamoja, huo unakuwa ni mwanzo wa mabadiliko yanayoanza kutoka katika undani wa watu wenyewe. Wakiwa wamezamisha maisha yao katika upendo, Wakristo wanaweza kuwa ni chachu ya mabadiliko kwa sababu Mungu ni upendo. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, watapata nafasi ya kukutana pengine kabla ya mwisho wa mwaka 2021. Tayari walikuwa wamekwisha kupanga kukutana, lakini kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 mkutano huo ukasogezwa mbele zaidi. Baba Mtakatifu anawahamasisha kutembea kwa pamoja, huku wakishirikishana maisha na upendo wa kidugu, kwa sababu mikutano ya namna hii, ni chemchemi ya furaha na matumaini. Kristo Yesu ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu kwa waja wake. Upendo unapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha.

Uekumene wa Sala

 

11 June 2021, 07:40