Tafuta

Papa Francisko tarehe 21 Juni 2021 amekutana na kuzungumza na kikundi cha wafungwa na viongozi wao mjini Vatican. Papa Francisko tarehe 21 Juni 2021 amekutana na kuzungumza na kikundi cha wafungwa na viongozi wao mjini Vatican. 

Papa Akutana na Kuzungumza na Wafungwa wa Rebibbia Roma

Katika ujenzi wa utu na udugu wa kibinadamu, Papa Francisko, Jumatatu tarehe 21 Juni 2021 amekutana na kuzungumza na vikundi cha wafungwa pamoja na viongozi wao, kutoka Gereza Kuu la Rebibbia lililoko mjini Roma, waliomtembelea kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha iliyoko mjini Vatican. Baadaye, wafungwa hao wamekwenda kutembelea Jumba la Makumbusho ya Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kwa nafasi mbalimbali amekuwa akiwahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kulitafakari Fumbo la Msalaba katika maisha ya wafungwa magerezani, kwa kutambua kwamba, Msalaba ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu. Kuna umuhimu wa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wafungwa magerezani, kwa kutambua kwamba, Askari magereza ni vyombo na mashuhuda wa Injili sanjari na kuwa na ujasiri wanapotekeleza dhamana na utume wao miongoni mwa wafungwa. Baba Mtakatifu anawapongeza Askari magereza kila wakati wanapotekeleza dhamana na utume wao kwa ajili ya ulinzi na usalama kwa maskini na wanyonge zaidi katika jamii, yaani wafungwa, ili kuhakikisha kwamba, haki, amani, ulinzi na usalama vinatawala ndani ya jamii.

Hii ni dhamana inayowataka siku kwa siku kuwa ni wajenzi wa haki na wajumbe wa amani kwa kuwakumbuka wafungwa hao waliofungwa kana kwamba wamefungwa pamoja nao na kama wanadhulumiwa, basi hata wao wahisi haya madhulumu mwilini wao. Gereza ni mahali pa mahangaiko ya binadamu. Askari magereza wanatumia muda mrefu kuwa magerezani, ili kulinda na kudumisha ulinzi na usalama, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinalindwa barabara. Askari magereza wawe ni walinzi wa ndugu zao wafungwa, wawe ni madaraja kati ya magereza na jamii katika ujumla wake kwa kuonesha upendo unaowawajibisha, ili kuondoa wasiwasi na kashfa ya kutowajali wengine. Baba Mtakatifu anawataka Askari magereza kutambua uzito wa kazi na wajibu wao kwa wafungwa pamoja na familia zao wenyewe. Kumbe, inawapaswa kusaidiana na kushikamana ili kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa zinazopatikana kutokana na kazi yao.

Ni katika muktadha huu wa kujenga na kudumisha utu na udugu wa kibinadamu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 21 Juni 2021 amekutana na kuzungumza na kikundi cha wafungwa pamoja na viongozi wao, kutoka Gereza Kuu la Rebibbia lililoko mjini Roma, waliomtembelea kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha iliyoko mjini Vatican. Baadaye, wafungwa hao wamekwenda kutembelea Jumba la Makumbusho ya Vatican. Kufurika kwa wafungwa magerezani nchini Italia ni kati ya changamoto changamani kwa wakati huu, hali ambayo inachangia pia kudhohofisha maisha ya Askari magereza, kiasi hata cha kukosa imani. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, wafanyakazi na wafungwa wanaishi maisha yenye hadhi na utu wa kibinadamu, vinginevyo magereza yatageuka kuwa nyumba cha chuki na uhasama badala ya kuwa ni mahali pa kurekebisha tabia na mwenendo wa wafungwa. Baba Mtakatifu Francisko anawataka wadau wa huduma mbali mbali magerezani kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili, tayari kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza. Wanapokumbana na umaskini wa wafungwa magerezani, watambue kwamba, hawa ni watu wanaohitaji kwanza kabisa msamaha na huruma ya Mungu. Wawe na ujasiri wa kusamehe kama mashuhuda waaminifu wa msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu; wawe ni watu wa faraja na kamwe wasimwache mtu hata mmoja kutumbukia katika upweke hasi, unaoweza kusababisha watu kumezwa na utamaduni wa kifo.

Baba Mtakatifu anawataka wafanyakazi magerezani kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuokoa maisha ya wafungwa kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika maisha ya Zakayo Mtoza ushuru. Wawe na ujasiri unaobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo zao na kamwe wasiruhusu kugubikwa na giza totoro katika maisha na nyoyo zao. Katika shida na mahangaiko ya ndani, wamkimbilie Kristo Yesu chini ya Msalaba na kumwelezea mahangaiko yao katika ukweli na uwazi. Msalaba ni chemchemi ya ujasiri, amani na utulivu wa ndani. Kamwe wasikubali kuzima utambi wa matumaini katika maisha yao. Hii ni dhamana na wajibu wa watu wote. Haki, matumaini, upatanisho pamoja na mchakato wa wafungwa kurejea tena katika maisha ya kawaida ndani ya jamii ni mambo msingi yanayotegemeana na kukamilishana. Wadau katika huduma ya wafungwa magerezani wasikubali kujifungia katika gereza lisilokuwa na matumaini katika maisha. Kila mtu anayo haki ya matumaini na haki ya kuanza kuandika tena ukurasa wa maisha yake kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Wafungwa
21 June 2021, 14:48