Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa mwezi Juni 2021 anawaalika waamini kutafakari kuhusu uzuri wa ndoa. Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa mwezi Juni 2021 anawaalika waamini kutafakari kuhusu uzuri wa ndoa. 

Nia za Baba Mtakatifu Francisko Mwezi Juni 2021: Uzuri wa Ndoa!

Papa katika Nia zake za Jumla kwa Mwezi Juni 2021, anawaalika waamini kutafakari kuhusu “Uzuri wa Ndoa”. Baba Mtakatifu anasali na kuwaombea vijana wa kizazi kipya wanaojiandaa kuadhimisha Sakramenti ya Ndoa katika maisha yao, waendelee kutiwa shime na jumuiya ya Wakristo: ili waweze kukua na kukomaa katika upendo, ukarimu, uaminifu na uvumilivu kwani inalipa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, Agano la Ndoa ambalo kwa njia yake, mwanaume na mwanamke huunda kati yao jumuiya kwa maisha yote, kwa tabia yake ya asili liko kwa ajili ya manufaa yao na kwa ajili ya kuzaa na kulea watoto. Agano hili kati ya wabatizwa, limeinua na Kristo Bwana kwa hadhi ya Sakramenti. Wanandoa wanaendeleza upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu ambao unapaswa kujidhihirisha kwa kuzaa na kutunza uumbaji. Na Mwenyezi Mungu akawabarikia na kuwaambia: Zaeni mkaongezeke, mkajaze nchi na kuitiisha. Rej. Mwa. 1:27; 1 Yoh.4:8, 16. Huu ni umoja usiovunjika wa maisha ya wanandoa hawa wawili kwa sababu “Hata wamekuwa si wawili tena bali mwili mmoja”. Mt. 19:4. “Aliowaunganisha Mungu mwanadamu asiwatenganishe”. Mt. 19:6. Mema na matakwa ya Mapendo ya Ndoa yanadai: Umoja na kutovunjika; Uaminifu na upendo wa kweli sanjari na uwazi kwa uzazi na malezi ya watoto kama kielele cha taji lao kwa kukumbuka kwamba, watoto ni zawadi bora ya Ndoa na wanachangia sana kwa mema ya wazazi wenyewe. Uzazi wa mapendo ya ndoa hujieneza pia kwa matunda ya maisha adili, maisha ya kiroho na ya kimungu ambayo wazazi wanayarithisha kwa watoto wao kwa njia ya malezi na makuzi makini.

Wazazi ni walezi wakuu na wa kwanza wa watoto wao. Kwa maana hiyo kazi ya msingi ya ndoa na ya familia ni kuhudumia Injili ya uhai. Wanandoa ambao Mwenyezi Mungu hakuwajalia kupata watoto wanaweza, hata hivyo, kuwa na maisha ya ndoa kwa maana kamili, kibinadamu na kikristo. Ndoa yao yaweza kung’aa uzazi wa mapendo, ukarimu na sadaka. Na kwa njia hii, wakawa tayari kujenga familia kama Kanisa dogo la nyumbani “Ecclesia domestica”: jumuiya ya neema na sala, shule ya fadhila za kibinadamu na mapendo ya Kikristo. Rejea. KKK 1601-1666. Lengo kuu la Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” ni kama ifuatavyo: Ni kujitahidi kunafsisha furaha ya Injili katika uhalisia wa maisha ya waamini, tayari kujitoa na kujisadaka kuwa ni chemchemi ya furaha kwa ndugu, jamaa na jirani; zawadi kubwa kwa Mama Kanisa na jamii katika ujumla wake. Pili, hii ni fursa ya kutangaza na kushuhudia umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa familia kama shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Familia ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, kielelezo cha ukomavu wa imani.

Tatu, waamini wanakumbushwa kwamba, Sakramenti ya Ndoa inapyaisha upendo wa kibinadamu. Kumbe, Kanisa halina budi kuhakikisha kwamba, linatoa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wake kwa familia na vijana, kwa kukazia malezi na makuzi; katekesi na majiundo awali na endelevu kama sehemu ya mchakato wa ukomavu wa imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha na kutolewa ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaosimikwa katika ukweli, uzuri, utakatifu na changamoto za maisha ya ndoa na familia. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika Nia zake za Jumla kwa Mwezi Juni 2021 zinazosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kuhusu “Uzuri wa Ndoa”. Baba Mtakatifu anasali na kuwaombea vijana wa kizazi kipya wanaojiandaa kuadhimisha Sakramenti ya Ndoa katika maisha yao, waendelee kutiwa shime na jumuiya ya Wakristo: ili waweze kukua na kukomaa katika upendo, ukarimu, uaminifu na uvumilivu.

Baba Mtakatifu anasema, kuna baadhi ya watu wanao dai kwamba, vijana wa kizazi kipya hawataki kufunga ndoa hasa kutokana na matatizo, changamoto na ugumu wa maisha wanaokabiliana nao kila kukicha! Baba Mtakatifu anawaambia vijana kufunga Ndoa na kushirikishana maisha ni jambo jema sana. Hii ni safari ndefu inayobeba dhamana, changamoto na wajibu. Wakati mwingine, katika safari ya maisha ya Ndoa, kunajitokeza mipasuko na kinzani, lakini hata hivyo, inalipa sana ikiwa kama vijana watathubutu na kuamua kufunga ndoa. Katika hija hii ya maisha kati ya wana Ndoa, watambue kwamba, Kristo Yesu yuko na anaandamana pamoja nao. Ndoa si tendo la kijamii peke yake, bali ni wito unaopata chimbuko lake kutoka katika sakafu ya moyo wa mwanadamu; unaohitaji utambuzi makini siku zote za maisha na kwamba, maisha ya ndoa na familia yanahitaji maandalizi makini. Vijana wa kizazi kipya wasisahau kwamba, Mwenyezi Mungu ana ndoto kwa kila mmoja wao, anataka waamini wamwilishe fadhila ya upendo katika maisha yao. Upendo wao ndiyo ndoto kubwa ya Mungu katika maisha yao!

Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii, kuwakumbuka na kuwaombea vijana wanaojiandaa kwa ajili ya kufunga Ndoa, wapate msaada kutoka katika jumuiya ya Wakristo: ili waweze kukua na kukomaa katika upendo, ukarimu, uaminifu na uvumilivu. Kupenda kwa dhati anasema Baba Mtakatifu yataka moyo na uvumilivu mkubwa! Lakini inapendeza kwa vijana kufunga ndoa na kuachana na "uchumba sugu".

Nia za Juni 2021
01 June 2021, 16:00