Tafuta

Mwenyeheri Sr. Maria Laura Mainetti: Shuhuda wa Huduma ya Upendo Mwenyeheri Sr. Maria Laura Mainetti: Shuhuda wa Huduma ya Upendo 

Mwenyeheri Sr. Maria L. Mainetti : Shuhuda wa Huduma ya Upendo

Mwenyeheri Sr. Maria Laura Mainetti, aliuwawa kikatili kutokana na imani za kishirikina na vijana aliopenda kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao yao. Aliwapenda na kuwasamehe vijana hao waliokuwa wamefungwa katika gereza la ubaya na dhambi. Amana na utajiri ambao ameliachia Kanisa ni imani katika matendo kama chachu ya ari na mwamko wa maisha ya Kikristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, katika Sherehe ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Jumapili tarehe 6 Juni 2021 amemtangaza Mtumishi wa Mungu Sr. Maria Laura Mainetti wa Shirika la Mabinti wa Msalaba, “Congregazione delle Figlie della Croce” kuwa ni Mwenyeheri. Ibada hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa huko Chiavenna, Jimbo Katoliki la Como, Kaskazini mwa Italia. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amemkumbuka Mwenyeheri Sr. Maria Laura Mainetti, aliyeuwawa kikatili kutokana na imani za kishirikina. Inasikitisha kuona kwamba, aliuwawa na vijana aliopenda kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao yao. Aliwapenda na kuwasamehe vijana waliokuwa wamefungwa katika gereza la ubaya na dhambi. Amana na utajiri mkubwa ambao Mwenyeheri Sr. Maria Laura Mainetti ameliachia Kanisa ni imani katika matendo kama chachu ya ari na mwamko wa maisha ya Kikristo. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia imani, matumaini, ari na mwamko wa maisha ya Kikristo!

Mwenyeheri Sr. Maria Laura Mainetti alizaliwa tarehe 20 Agosti 1939. Tarehe 15 Agosti 1959 akaweka Nadhiri zake za Kwanza. Aliuwawa kikatili tarehe 6 Juni 2000 huko Chiavenna kutokana na imani za kishirikina na chuki dhidi ya imani “In Odium Fidei”. Mwenyeheri Sr. Maria Laura Mainetti alipokuwa kifoni, huku akisali, aliwasamehe watesi na wauaji wake. Katika kipindi cha miaka 21 tangu alipouwawa “Nyota angavu ya Sr. Maria Laura Mainetti inaendelea kuangaza, kiasi kwamba, imekuwa ni chemchemi ya toba na wongofu wa ndani kwa watesi na wauaji wake. Ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu uliomwilishwa katika huduma kwa maskini na hasa wale waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na ujinga, kwani Mwenyeheri Sr. Maria Laura Mainetti alikuwa ni Mwalimu aliyetoa huduma yake huko Vasto, Roma, Parma na Chiavenna (Sondrio), kiasi kwamba, hata leo hii wanafunzi wake wanamkumbuka kwa heshima na taadhima! Ni mtawa ambaye aliyapamba maisha yake kwa sala, tafakari ya Neno la Mungu na Ibada ya Misa Takatifu. Alinogesha sala na maisha yake kwa njia ya huduma kwa: watoto, vijana na watu waliokuwa na shida mbalimbali katika maisha.

Alikirimiwa kipaji cha kusikiliza kwa maskini na kutoa ushauri muafaka. Alibahatika kuwa na furaha ya ndani, ambayo aliwashirikisha pia jirani zake, kama kielelezo cha furaha ya Injili ya Kristo. Alipenda kuwaalika vijana kwenda Kanisa kusali, ili baada ya sala zao, waweze kupenda kwa dhati. Hii ndiyo njia inayoelekea kwenye upendo unaosimikwa katika msamaha wa kweli! Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu katika mahubiri yake amekazia kuhusu upendo wa kweli unaomwilishwa katika huduma makini kwa Mungu na jirani, kiasi hata cha mtu kuthubutu kuyamimina maisha yake. Huu ni upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu katika Sakramenti kuu ya Ekaristi Takatifu. Ni shuhuda na chombo cha upendo wa Kristo Yesu unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya mtu. Utakatifu wa maisha ni wito na mwaliko kwa kila mwamini! Upendo wa kweli anasema, Kardinali Marcello Semeraro unatoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu na jirani “Vera Caritas”. Matunda ya upendo ni furaha, amani na huruma; upendo unadai ukarimu na kuonyana kidugu; upendo ni wema; hukuza hali ya kupokeana, hubaki huru bila kujitafutia faida; ni urafiki na umoja.

Mwenyeheri Sr. Maria Laura Mainetti ni shuhuda wa upendo na imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kufia dini ni ushuhuda wa hali ya juu unaotolewa kwa kweli ya imani yaani ni ushuhuda hadi mauti. Mfiadini humshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ambaye ameunganika naye kwa upendo. Anaishuhudia kweli ya imani na mafundisho ya Kikristo. Anavumilia kifo kwa njia ya tendo la ujasiri. Rej. KKK 2471 – 2474. Kardinali Marcello Semeraro, amesema, Alhamisi Kuu, Mama Kanisa aliadhimisha Karamu ya Mwisho, Kristo Yesu, usiku ule alipotolewa, aliweka sadaka ya Ekaristi Takatifu ya Mwili na Damu yake Azizi, kama Sakramenti ya upendo, umoja, kifungo cha mapendo, Karamu ya Pasaka ambamo Kristo huliwa na roho hujazwa neema, na ambamo waamini wanapewa amana ya uzima wa milele. Ekaristi Takatifu ni muhtasari wa imani ya Kanisa katika kufikiri na kutenda! Hii ni kumbukumbu endelevu ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu.

Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya matumaini mapya katika maisha ya uzima wa milele. Wanaoshiriki Karamu ya Uzima wa Milele wanahamasishwa kuwa ni wajenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Mwenyeheri Sr. Maria Laura Mainetti ametambuliwa na Mama Kanisa kuwa ni kati ya Wenyeheri walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwanakondoo. Sala Kuu ya Baba Yetu inawahimiza waamini kuwasamehe wale wanaowaokosea na kuwatendea ubaya. Sr. Maria Laura Mainetti, kwa kusamehewa dhambi zake, akapata ujasiri wa kuwasamehe pia watesi wake. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12) anakazia kuhusu mwaliko wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo. Kristo Yesu anawaalika wote wanaoteseka au kudhulumiwa kwa ajili yake, kufurahi na kushangilia, kwani yeye ni chemchemi ya maisha na furaha ya kweli. Kristo Yesu anataka waja wake kuwa kweli ni watakatifu, mwaliko na changamoto inayojionesha katika sehemu mbali mbali za Maandiko Matakatifu.

Baba Mtakatifu anasema, lengo la wosia huu ni mwaliko wa kuwa watakatifu kila mtu kadiri ya hali na wito wake; kwa kutambua vizingiti, changamoto na fursa ambazo zinaweza kutumiwa na waamini kufikia utakatifu wa maisha. Kristo Yesu anawaalika waja wake ili wawe watakatifu, watu wasiokuwa na hatia mbele zake katika upendo. (Rej. Ef. 1:4). Utakatifu ni mapambano endelevu katika maisha sanjari na kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni mwaliko wa kupenda na kufanya unachotaka kufanya. Mtakatifu Augostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa anasema, “Dilige et quod vis fac” yaani “Penda na utende unachotaka”. Hata katika kukaa kimya, kaa katika upendo; ikiwa unaongea, Ongea katika upendo; ikiwa unakosoa, kosoa kwa upendo; unaposamehe, jitahidi kusaheme kwa upendo. Upendo uzamishe mizizi yake katika maisha ya waamini kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Sr Mainetti
06 June 2021, 16:41