Tafuta

Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo ndani ya Familia yanogeshwe na: sala, tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisha na Matendo ya Huruma Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo ndani ya Familia yanogeshwe na: sala, tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisha na Matendo ya Huruma 

Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia: Umuhimu wa Sala!

Sala imepewa kipaumbele kama sehemu ya maandalizi na maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo ndani ya Familia. Mang’amuzi ya upendo yanayopata chimbuko lake katika maisha ya familia yanakuwa ni wito wa kila mtoto anayezaliwa na hivyo kuwa ni dira na mwelekeo wa utakatifu wa maisha. Sala ni kiungo muhimu sana cha mahusiano na mafungamano ya kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Miaka 5 tangu Baba Mtakatifu Francisko achapishe Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2021, Mama Kanisa amezindua Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia: “Famiglia Amoris Laetitia” yatakayofikia kilele chake wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani kuanzia tarehe 22 hadi 26 Juni 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”. Furaha inayopata chimbuko lake ndani ya familia ni furaha ya Kanisa pia na kwamba, tamko la Kikristo kuhusu familia ni Habari Njema kweli! Rej. AL 1. Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” unakwenda sanjari na maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu. Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, akiwasilisha Sala ya maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia kwa kushirikiana na Jimbo kuu la Roma, anasema, Sala imepewa kipaumbele cha pekee kama sehemu ya maandalizi na maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo ndani ya Familia.

Lengo ni kuwasaidia waamini kutambua umuhimu wa tukio hili katika maisha na utume wa Kanisa na ushiriki wao kiroho. Mang’amuzi ya upendo yanayopata chimbuko lake katika maisha ya familia yanakuwa ni wito wa kila mtoto anayezaliwa na hivyo kuwa ni dira na mwelekeo wa utakatifu wa maisha. Sala ni kiungo muhimu sana cha mahusiano na mafungamano ndani ya familia kila kukicha. Wito na Utakatifu wa maisha ni chemchemi ya upendo wa dhati katika maisha ya ndoa na familia, yanayowawezesha wanandoa kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa mbalimbali zinazojkitokeza katika maisha yao. Sala ni kiungo muhimu sana kinachowawezesha wanandoa kuishi kikamilifu Sakramenti ya Ndoa katika maisha yao. Sala inawapatia wanandoa nafasi ya kupyaisha Neema waliyopokea ili hatimaye, kukabiliana na mapambano pamoja na majukumu yao ya kila siku. Changamoto ya utakatifu wa maisha inapata chimbuko lake kwanza kwa mtu binafsi, familia na hatimaye, wanandoa katika ujumla wao, kiasi hata cha utakatifu huu, kuwaambata majirani zao. Wito wa utakatifu wa maisha ni changamoto inayotolewa kwa watu wote wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Vijana wana ndoto ya kuona watakatifu wanaowafunda watakatifu wengine, kwani utakatifu ni sura pendevu ya Kanisa! Kwa hakika, vijana wanataka kusikia lugha ya utakatifu wa maisha ambao ni wito wa kwanza kwa kila mwamini kama wanavyokaza kusema, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Kwa njia ya Utakatifu wa maisha, Kanisa linaweza kupyaisha ari ya maisha ya kiroho na utume wake. Mafuta ya utakatifu yanaweza kulisaidia Kanisa kuganga na kutibu majeraha ya watoto wake na walimwengu katika ujumla wao, kwa kuonesha utimilifu wa upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu! Kumbe, kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu” inapania kuwasaidia watu wa Mungu kutambua wito wao katika maisha na utume wa Kanisa.

Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma anasema, wanandoa wanahimizwa kukita maisha yao katika upendo wa familia, kwani hiki ni kiini cha wito wao, unaowaelekeza katika mchakato wa utakatifu wa maisha. Katika historia na maisha ya Kanisa kuna watakatifu na wenyeheri ambao ni wanandoa na hawa wanaweza kuwa ni waombezi wazuri kwa familia. Mama Kanisa anaweka mbele ya waamini mfano wa wazazi wa Mtakatifu Thérèse wa Lisieux, au wanandoa Beltrame Quattrocchi. Hawa ni waamini waliokubali kupokea shida, magumu na changamoto za maisha kwa moyo wa imani na matumaini thabiti, wakagundua na kuonja uwepo endelevu wa Mungu katika maisha yao. Matumaini ya waamini kwa Mwenyezi Mungu ambaye daima ni mwaminifu yanawawezesha kutangaza na kushuhudia Injili ya familia “kama njia ya Kanisa” mahali ambapo miito mipya inachipua na kurutubishwa!

Familia

 

15 June 2021, 16:09