Tafuta

Mshikamano wa Papa Francisko na Watu wa Mungu kutoka Mkoa wa Tigray kutokana na vita na baa la njaa. Mshikamano wa Papa Francisko na Watu wa Mungu kutoka Mkoa wa Tigray kutokana na vita na baa la njaa. 

Mshikamano wa Papa Francisko na Watu wa Tigray, Ethiopia: Njaa na Vita!

Baba Mtakatifu Francisko ni kusitisha mapigano kwani hivi ni vita isiyokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Ethiopia katika ujumla wake. Mkazo zaidi uelekezwe katika huduma ya uhakika na usalama wa chakula; afya sanjari na kurejeshwa tena kwa hali ya amani na utulivu, ili kuwapatia wananchi nafasi ya kujitafutia mahitaji msingi. No Vita!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 13 Juni 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican alipenda kuonesha uwepo wake wa karibu na mshikamano wa dhati kwa watu wa Mungu wanaoteseka kwenye Mkoa wa Tigray nchini Ethiopia. Hawa ni watu ambao wamekumbwa na vita iliyoanza kutimua vumbi mwanzoni mwa mwezi Novemba 2020. Haya ni mapambano kati ya Vikosi vya ulinzi na usalama vya Serikali pamoja vikosi maalum vya mkoa wa Tigray. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, kuna watu zaidi 353, 000 wanaokabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na tayari kuna watu wameanza kupoteza maisha yao.

Kuna wanawake na wasichana wanaotekwa nyara na watu wasiojulikana na hivyo kugeuzwa kuwa ni wahanga wa utumwa mamboleo na biashara ya binadamu, mambo yanayodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Inasemekana kwamba, zaidi ya watoto 300, 000 wamefariki dunia kutokana na utapiamlo wa kutisha. Shughuli za kilimo ambazo zingeweza kuwahakikishia watu wa Tigray uhakika na usalama wa chakula zimeathirika kutokana na mapigano yanayoendelea, kiasi kwamba, wakulima hawawezi kulima wala kuvuna mazao yao kwa wale waothubutu kwenda shambani wanakiona cha mtemakuni. Wachunguzi wa mambo wanasema, shughuli za kilimo kwa sasa zinaendeshwa usiku.

Mapigano kati ya Chama cha Ukombozi wa Tigray “Tigray People’s Liberation Front” na Serikali ya Ethiopia inayoongozwa na Waziri mkuu Abiy Ahmed yameathiri sana uzalishaji wa mazao ya chakula eneo hili. Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba, asilimia 13% ya watu milioni 5.2 wanahitaji msaada wa chakula cha dharura. Jambo la dharura kwa wakati huu anasema Baba Mtakatifu Francisko ni kusitisha mapigano kwani hivi ni vita isiyokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Ethiopia katika ujumla wake. Mkazo zaidi uelekezwe katika huduma ya uhakika na usalama wa chakula; afya sanjari na kurejeshwa tena kwa hali ya amani na utulivu, ili kuwapatia wananchi nafasi ya kujitafutia mahitaji msingi. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wale wote ambao wameendelea kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba wanasaidia kupunguza mateso na mahangaiko ya wananchi wa Mkoa wa Tigray.

Tigray Ethiopia

 

14 June 2021, 14:50