Tafuta

Jubilei ya Miaka 900 tangu kuanzishwa kwa Abasia ya Prèmontrè. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Padre Jozef Wouters. Jubilei ya Miaka 900 tangu kuanzishwa kwa Abasia ya Prèmontrè. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Padre Jozef Wouters. 

Jubilei ya Miaka 900 ya Abasia ya Prèmontrè: Chombo cha Mageuzi

Katika barua hii, Baba Mtakatifu Francisko anabainisha mchango ulitolewa na Mtakatifu Norbert wa Xanten katika maisha na utume wa Kanisa. Shirika liendeleze: karama, amana na utajiri wa muasisi wa Shirika lao katika mchakato wa uinjilishaji mpya. Mageuzi haya ni chachu na mwamko mpya wa maisha na utume ndani ya Kanisa. Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha utume wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ili kuboresha maisha na utume wa Mapadre wa Jimbo, Mama Kanisa katika busara yake ya kichungaji alichochea karama na moyo wa kuanzisha Jumuiya ya Mapadre wa Jimbo waliokuwa wakisali Liturujia ya Sala za Kanisa na kutekeleza utume wao kwa pamoja na hasa katika Parokia za mijini ambako kuna utume wa kutosha. Mtindo huu wa maisha ulianza kushika kasi kunako karne ya XI. Mtindo huu wa maisha ulifuata kanuni ya Mtakatifu Agostino wa Hippo na kuitwa Wakanoni. Maarufu zaidi kati yao ni Mtakatifu Norbert wa Xanten (1075-1134), mwanzilishi wa Shirika la Wakanoni wa Waprémontré. Abasia ya Prémontré ilianzishwa na Mtakatifu Norbert wa Xanten (Anayefahamika pia kama Mtakatifu Norbert Gennep), mwaka 1120 na hatimaye kutabarukiwa kunako mwaka 1122. Abasia hii ikawa ni Nyumba Mama ya Shirika la Wakanoni wa Waprémontré. lililokuwa limeanzishwa hivi punde. Padre Jozef Wouters, Mkuu wa Shirika la Wakanoni wa Waprémontré ametangaza maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 900 tangu kuanzishwa kwa Abasia ya Prémontré iliyoko huko nchini Ufaransa.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia barua ya pongezi Padre Jozef Wouters, Mkuu wa Shirika la Wakanoni wa Waprémontré wakati huu wanapoadhimisha Jubilei ya Miaka 900 tangu kuanzishwa kwa Abasia ya Prémontré. Katika barua hii, Baba Mtakatifu anabainisha mchango ulitolewa na Mtakatifu Norbert wa Xanten katika maisha na utume wa Kanisa. Shirika liendeleze: karama, amana na utajiri wa muasisi wa Shirika lao katika mchakato wa uinjilishaji mpya. Mageuzi haya ni chachu na mwamko mpya wa maisha na utume ndani ya Kanisa. Papa Francisko anasema, Mtakatifu Norbert wa Xanten alizaliwa kunako mwaka 1075. Katika maisha na utume wake, aliwahi kuwa mshauri wa Mfalme Enrico V. Ni muasisi wa mabadiliko makubwa ya uteuzi wa Maaskofu na Maabate mintarafu; mwanga na tunu msingi za Kiinjili pamoja na utume wa Mapadre. Ni kiongozi aliyependa kuona kwamba, uteuzi wa viongozi wa Kanisa unatenganishwa na mambo ya kiulimwengu. Mwaka 1115 Mtakatifu Norbert wa Xanten, akafanya mageuzi makubwa katika maisha na utume wake kwa kuamua kumfuata Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kujiweka chini ya uongozi wa Askofu Federick wa Jimbo kuu la Colon nchini Ujerumani. Akapewa Daraja ya Ushemasi na siku hiyo hiyo akapewa Daraja Takatifu ya Upadre.

Tangu siku hiyo akaamua kuambata tunu msingi za Kiinjili mintarafu chachu za mageuzi zilizoletwa na kanuni ya Mtakatifu Augostino wa Hippo. Akaanza kuhubiri toba na wongofu wa ndani unaosimikwa katika: sala, kufunga na kujisadaka pamoja na kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, ingawa wakati ule, Mapadre hawakuwa na lazima ya kuadhimisha Ekaristi Takatifu kila siku. Hii ni changamoto kwa Shirika kuendeleza amana na utajiri waliorithishwa na Muasisi wa Shirika lao. Yaani kuendelea kuwa waaminifu katika tafakari ya Neno la Mungu, mahubiri pamoja na kuhakikisha kwamba, wanachota amana na utajiri wa maisha ya kiroho kutoka katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Alijitahidi katika maisha yake, kufuata nyayo za Mitume wa Yesu, akatangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Leo hii kuna haja kwa Mapadre kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kwa kujikita katika maisha ya binafsi yanayonogeshwa na maisha ya kijumuiya.

Papa Francisko anasema, Mtakatifu Norbert wa Xanten tangu alipotubu na kumwongokea Mungu, aliendelea kuwa ni Mtumishi mwaminifu wa Injili ya Kristo, akalipenda Kanisa na kuonesha utii kwa Baba Mtakatifu. Aliishi maisha yaliyokuwa na mvuto na mashiko kiasi kwamba, baadhi ya watu waliacha shughuli zao na kuanza kumfuata katika maisha kama ilivyokuwa kwa Ugo wa Fosses ambaye baadaye alichaguliwa kuwa ni Abate wa kwanza wa Abasia ya Prémontré. Mtakatifu Norbert wa Xanten alibahatika kuwa na karama ya kupunga pepo wachafu, akatambulikana na wengi kuwa ni mpatanishi na chombo cha amani na upendo uliokuwa unabubujika kutoka katika maisha ya sala. Kunako mwaka 1121 akaanzisha Shirika la Wakanoni wa Waprémontré ili kuendeleza mchakato wa toba na wongofu wa ndani. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wanashirika kuendeleza utume na kusali kwa ajili ya Kanisa. Mwanzo wa maisha ndani ya Abasia ya Prémontré yalikuwa kamayanavyosimuliwa kwenye Kitabu cha Matendo ya Mitume.

Walishikamana kwa maisha ya sala na Ibada. Wakajisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Mtindo huu wa maisha, ukaleta mvuto kwa watu wengi na baadhi ya jumuiya zilizokuwepo tangu awali zikajiunga na Mtakatifu Norbert wa Xanten. Abasia hii ikawa ni kituo kikuu cha ushauri wa maisha ya kiroho, chemchemi ya sala, toba na wongofu wa ndani pamoja na liturujia inayoadhimishwa kwa umakini mkubwa ili Mwenyezi Mungu aweze kutukuzwa na mwanadamu kutakatifuzwa. Kunako mwaka 1124 kulizuka mtafaruku mkubwa kuhusu uhalali wa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu iliyokuwa inaadhimishwa na “Mapadre waliokuwa na masuria”. Mtakatifu Norbert wa Xanten akasimama kidete kulinda, kutetea na kufafanua vyema mafundisho ya Kanisa kuhusu Ekaristi Takatifu. Katika mageuzi makubwa kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu, Mtakatifu Norbert wa Xanten anatajwa kuwa ni Mtume wa Ekaristi Takatifu. Daima amewahimiza Mapadre kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu na hasa nyakati za kinzani na migogoro mbalimbali na hata pale Padre anapokabidhiwa majukumu nyeti katika maisha na utume wake.

Kunako mwaka 1126 Papa Honorius II akamteuwa Mtakatifu Norbert wa Xanten kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu Katoliki la Magdeburg pamoja na kupitisha Katiba ya Shirika ambalo alikuwa amelianzisha. Akiwa Jimboni humo, alianzisha Jumuiya mbalimbali kwa ajili ya kujikita katika mchakato wa uinjilishaji ndani na nje ya Jimbo. Katika maisha na utume wake, akasimama kidete kumlinda na kumtetea Khalifa wa Mtakatifu Petro alipokumbana na kinzani mbalimbali katika maisha na utume wake. Akajitahidi kuhakikisha kwamba, uongozi wa Kanisa unajikita zaidi katika kanuni ya uhuru inayompatia nafasi Khalifa wa Mtakatifu Petro kuteuwa Mapadre kwa ajili ya nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Kanisa. Mwaka 1128 Mtakatifu Norbert wa Xanten akang’atuka kutoka madarakani na Ugo wa Fosses akachukua nafasi yake katika uongozi. Akafanikiwa kuunganisha Jumuiya mbalimbali na kuwa ni Shirika moja na lenye mkutano mkuu ambao ni kielelezo cha hali ya juu cha uongozi wa Shirika.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, imegota sasa miaka 900 tangu Mtakatifu Norbert wa Xanten aanzishe Abasia hii. Ni kiongozi wa Kanisa aliyebahatika kusoma alama za nyakati na kuwawezesha watawa wake kuendeleza utambulisho wao. Leo hii, kuna wanawake wengi wamejiunga pamoja kwa ajili ya maisha ya tafakari. Kuna makundi makubwa ya wanawake yanayoendelea kushiri kikamilifu katika tasaufi yao sanjari na kujisadaka kwa ajili ya watu wanaoishi katika mazingira magumu. Baba Mtakatifu anawahimiza kuendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma za kichungaji Parokiani, huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; amana na utajiri mkubwa kwa Kanisa. Mtakatifu Norbert wa Xanten amepitia hatua mbalimbali za maisha kama mhubiri, padre, mkuu wa jumuiya na Askofu mkuu. Katika hatua zote hizi, ameendelea kuongozwa na Injili, kwa kumsikiliza Mwenyezi Mungu pamoja na kusoma alama za nyakati bila kupoteza dira na mwelekeo wa maisha na utume wake.

Jubilei Miaka 900

 

 

 

08 June 2021, 15:25