Tafuta

Bikira Maria Mfungua Mafundo: Fungua mafundo yote ya kiroho, kimwili, kijamii, kiuchumi na kisiasa. Bikira Maria Mfungua Mafundo: Fungua mafundo yote ya kiroho, kimwili, kijamii, kiuchumi na kisiasa. 

B. Maria Mfungua Mafundo: Fungua Mafundo: Kiroho na Kimwili

Baba Mtakatifu amemwomba Bikira Maria Mfungua Mafundo, awaombee waamini kwa Mwanaye Kristo Yesu, ili aweze kuwaonea huruma na hatimaye, kuwaondolea janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambalo limepelekea maafa makubwa kwa watu. Awawezeshe kuanza tena upya na hatimaye, kuendelea na maisha yao ya kila siku katika hali ya amani na usalama.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Katika maadhimisho ya Sikukuu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeth, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 31 Mei, Baba Mtakatifu Francisko amefunga pia Mwezi wa Rozari Takatifu. Hii imekuwa nafasi kwa Baba Mtakatifu kuungana na waamini kutoka sehemu mbalimbali za dunia, kwa ajili ya kufunga Mwezi wa Rozari Takatifu, kwenye Bustani za Vatican. Kwa muda wa Mwezi mzima, waamini wameungana na Baba Mtakatifu Francisko kusali Rozari wakiomba ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mfungua Mafundo dhidi ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Mama Kanisa anatambua kwamba, Madhabahu ni mahali muafaka pa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni mahali pa toba na wongofu wa ndani, unaomwezesha mwamini kuchuchumilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha, kama chachu ya utimilifu na utakatifu wa maisha. Katika kipindi cha mwezi mzima, waamini kutoka katika madhabahu 30 yaliyoko sehemu mbalimbali za dunia, wameshiriki katika Ibada ya Rozari takatifu kwa kupokezana.

Picha ya Bikira Maria Mfungua Mafundo kutoka Jimbo Katoliki la Augsburg, Ujeruman iliyochorwa na Ana Maria Berti ndiyo iliyotumika wakati kusali na kutafakari Mafumbo ya Rozari Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Katika sala yake ya utangulizi, Baba Mtakatifu amemwomba Bikira Maria Mfungua Mafundo, awaombee waamini kwa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, ili aweze kuwaonea huruma na hatimaye, kuwaondolea janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambalo limepelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao. Awawezeshe kuanza tena upya na hatimaye, kuendelea na maisha yao ya kila siku katika hali ya amani na usalama. Baba Mtakatifu amemwomba Bikira Maria Mfungua Mafundo awafungulie watu wa Mungu mafundo yanayokwamisha maisha na shughuli zao za kila siku. Lakini zaidi, afungue mafundo ya uchoyo na ubinafsi; hali ya kutowajali wala kuwathamini wengine. Afungue mafundo ya kiuchumi na kijamii; ghasia na vita, ili hatimaye, asaidie kuimarisha imani, ili waamini waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu amemwomba Bikira Maria Mfungua Mafundo, awafungulie mafundo yanayokwamisha mahusiano na mafungamano ya kijamii katika ngazi mbalimbali, ili kukoleza na kudumisha furaha ya maisha ya kijumuiya, ili kuvuka vikwazo vya ubinafsi na hali ya kutojali! Waamini wamemwomba Bikira Maria awafungulie fundo la ukosefu wa fursa za ajira na asaidie mwanzo wa mchakato wa upyaishaji wa maisha ya kijamii na kiuchuni. Nyanyaso, dhuluma na vipigo vya majumbani ni kati ya mafundo yanayogumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Yote haya yanapelekea kinzani, mipasuko ya kijamii, ukosefu wa haki jamii pamoja na mshikamano. Baba Mtakatifu amemwomba Bikira Maria afungue hata na haya mafundo, ili kweli familia iweze kuwa ni shule ya haki, amani, upendo na maridhiano ya kweli. Magonjwa na hasa yale ya muda mrefu, wasiwasi, hofu na mashaka ni kati ya mafundo yanayowapekenya watu wa Mungu, kiasi hata cha kuwanyima: furaha, amani na utulivu wa ndani.

Bikira Maria afungue mafundo haya, kwa kuwajalia waamini na watu wote wenye mapenzi mema, afya njema na mshikamano wa hali na mali kwa wanasayansi wanaofanya tafiti mbalimbali za magonjwa ya binadamu, ili waweze kufanikisha nia hii njema. Baba Mtakatifu Francisko amemwomba Bikira Maria afungue mafundo ya shughuli za kichungaji, ili kupata ari na mwamko mpya katika shughuli za kichungaji tayari kuzama katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda. Bikira Maria awasaidie wanandoa watarajiwa, kujiandaa vyema kama ilivyo hata kwa vijana wa katekesi, waweze kujiandaa vyema kuadhimisha Sakramenti za Kanisa zinazonafsishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Waamini wawe ni jasiri na mashuhuda wa Injili ya huruma na mapendo, ili kukutana na kuwakirimia wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Bikira Maria Wa Mafundo
01 June 2021, 13:56