Tafuta

Papa Francisko amemwandikia barua Kardinali Reinhard Marx na kumtaka kuendelea na utume wake kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Papa Francisko amemwandikia barua Kardinali Reinhard Marx na kumtaka kuendelea na utume wake kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. 

Barua ya Papa Kwa Kardinali R. Marx: Chunga Kondoo wa Yesu

Kardinali Reinhard Marx anasema, amepokea kwa heshima na ametii kwa uhuru kamili, agizo la Baba Mtakatifu Francisko na sasa anaendelea kuwatumikia watu wa Mungu kwa ari na moyo mkuu. Hiki ni kipindi muafaka kwa watu wa Mungu Jimbo kuu la Munich na Freising, kukaa chini na kuanza kutafakari na kupembua makosa yaliyojitokeza katika historia na maisha ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Reinhard Marx, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Munich na Freising nchini Ujerumani aliyemwandikia Baba Mtakatifu Francisko barua na kutia nia ya kung’atuka, iliyoandikwa tarehe 21 Mei 2021 amejibiwa na Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake ya tarehe 10 Juni 2021 na kumtaka aendelee na utume wake wa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo kuu la Munich na Freising. Kwa upande wake, Kardinali Reinhard Marx, ambaye tayari alimekwisha kufunga vilago na kuanza kujiandaa kuandika ukurasa mpya wa maisha na utume wake, anasema, ameshangazwa sana na majibu yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu maisha na utume wake. Hakutegemea kuendelea tena na utume wake kama Mchungaji mkuu wa Jimbo kuu la Munich na Freising. Barua ya Baba Mtakatifu Francisko aliyomwandikia binafsi imemgusa sana kwa sababu inaonesha ule udugu, kwa kutambua nia yake njema ya kutaka kung’atuka madarakani kama sehemu ya uwajibikaji kwa nyanyaso za kijinsia zilizolikumba Kanisa nchini Ujerumani. Kardinali Reinhard Marx anasema, amepokea kwa heshima na ametii kwa uhuru kamili, agizo la Baba Mtakatifu Francisko na sasa anaendelea kuwatumikia watu wa Mungu kwa ari na moyo mkuu.

Hiki ni kipindi muafaka kwa watu wa Mungu Jimbo kuu la Munich na Freising, kukaa chini na kuanza kutafakari na kupembua makosa yaliyojitokeza katika historia na maisha ya Kanisa; kutubu na kuongoka na hivyo kuanza utekelezaji wa sera na mikakati mipya kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa zima. Lengo ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu kwa ari na moyo mkuu, tayari kuchangia mchakato wa kuendelea kulipyaisha Kanisa la Kristo katika ujumla wake. Barua ya Baba Mtakatifu Francisko inachambua kwa kina na mapana changamoto zilizojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Jimbo kuu la Munich na Freising, changamoto ambazo kwa sasa hazina budi kuvaliwa njuga, ili kupewa majibu muafaka na kuendelea kusoma alama za nyakati. Kardinali Reinhard Marx, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Munich na Freising amerejea tena katika utume, huku akisonga mbele kwa imani na matumaini. Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake kwa Kardinali Reinhard Marx, amempongeza kwa kuamua kuwajibika kama Askofu mkuu kutokana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo zilizofanywa Jimboni mwake. Kristo Yesu alifanya mageuzi makubwa katika historia ya mwanadamu kwa njia ya maisha na utume wake.

Mama Kanisa anatambua na kukiri udhaifu wa watoto wake, uliopelekea kutumbukia katika kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo na kwamba, kila mwamini ajifunge kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, anapambana kufa na kupona ili kamwe nyanyaso za kijinsia zisirejee tena katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anampongeza Kardinali Reinhard Marx kwa kuamua kuubeba Msalaba wa uwajibikaji kama kielelezo cha neema na baraka itakayozaa matunda kwa wakati wake. Kanisa Katoliki nchini Ujerumani limejikuta njia panda kutokana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ambazo zimechafua kwa kiasi kikubwa maisha na utume wa Kanisa nchini Ujerumani. Kashfa hii inapaswa kuchukuliwa katika misingi ya imani katika Fumbo la Pasaka, kwa kuuangalia ukweli jinsi ulivyo, tayari kuanza mchakato wa kumtafuta Mwenyezi Mungu na kutekeleza mapenzi yake. Ni mwaliko wa kuondokana na unafiki kwa kujikita katika maisha ya uwajibikaji, ambayo kimsingi ni neema, tayari kuibua sera na mbinu mkakati utakaoweza kukabiliana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Hii ni changamoto kwa Maaskofu kusoma alama za nyakati na kufanya maamuzi magumu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo.

Mama Kanisa anatambua udhaifu na mapungufu ya watoto wake. Katika maisha na utume wake, Kanisa limewahi kuomba msamaha kutokana na dhambi za watoto wake. Kanisa ni takatifu kwa sababu limeanzishwa na Kristo Yesu mwenyewe, lakini lina wadhambi ambao wanaelemewa na udhaifu wao. Katika nafasi zote hizi, Kanisa limetakiwa kufanya mageuzi makubwa! Lakini ikumbukwe kwamba, mageuzi yanaanza kutoka katika ngazi ya mtu mmoja mmoja na baadaye jamii nzima ya waamini kwa kumwachia Kristo Yesu kutenda kazi ndani mwao. Hapa kila mwamini anapaswa kuajibika. Kristo Yesu alifanya mageuzi makubwa katika maisha na histroria ya binadamu kwa: Maisha na mafundisho yake lakini zaidi kwa Njia ya Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko uletao uzima wa milele. Kardinali Reinhard Marx kwa upande wake, ilikuwa ni kung’atuka kutoka madarakani. Watu wa Mungu hawana budi kukiri kwamba, wamekosa na wametenda dhambi.

Ni wakati wa kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kupokea na kuambata neema na baraka zake zinazoganga, kuponya na kuokoa. Mwishoni mwa barua yake, Baba Mtakatifu Francisko anamwambia Kardinali Reinhard Marx, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Munich na Freising nchini Ujerumani kwa kufuata mfano wa Mtakatifu Petro Mtume, amekataa kukubali ombi lake la kutaka kungatuka kutoka madarakani na badala yake anamtaka kwenda kuchunga kondoo wa Kristo Yesu, Jimboni mwake!

Kardinali Marx

 

 

11 June 2021, 16:28