Baraza la Makardinali,mkutano wa mchakato wa kisinodi na usimamizi wa fedha
Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.
Umuhimu wa njia za sinodi katika majimbo ya ulimwengu, kuridhika na ripoti ya Moneyval na maendeleo katika usimamizi wa kifedha, usasishwaji wa habari kwa jumla juu ya hali halisi ya janga katika mabara mbali mbali ndizo zimekuwa hoja kuu zilizojitokeza kwenye mkutano wa Baraza la Makardinali washauri wa Papa ambalo limefanyika kwa njia ya mtandao tarehe 24 Juni 2021 alasiri, saa kumi jioni.
Wameunganishwa kutoka mabara yote
Kwa mujibu wa habari kutoka Ofisi ya Wanahabari Vatican, Papa alifuatilia shughuli hiyo kwa kuunganishwa kutoka Nyumba ya Mtakatifu Marta, wakati Katibu wa Vatican Kadinali Pietro Parolin hakuweza kushiriki kwa sababu alishiriki katika Tamasha la Ekolojia Jumuishi huko Montefiascone, huko Viterbo, Italia. Kutoka katika nchi zao wakiwa katika makazi yao, kazi hiyo ilifuatiliwa kwa ukaribu na makadinali Óscar A. Rodríguez Maradiaga, Reinhard Marx, Sean Patrick O'Malley, Oswald Gracias na Fridolin Ambongo Besungu. Kwa upande mwingine, Kardinali Giuseppe Bertello na katibu wa Baraza, Monsinyo Marco Mellino, waliunganishwa kutoka Vatican.
Ukaribu na Myanmar
Baada ya salamu za Baba Mtakatifu Francisko, makadinali walitoa michango mifupi kuwasilisha hali halisi pia hali ya janga la Covid-19, katika mabara mbalimbali. Katika muktadha huu, Kardinali Gracias amemshukuru Baba Mtaatifu Francisko kwa maneno na ukaribu alioonesha kwa hali hiyo chungu nchini Myanmar.
Michakato ya njia za kisinodi na ripoti ya Moneyval
Katika kutoa neno Papa amerudia kuelezea umuhimu wa mchakato wa njia za sinodi zilizopo katika ngazi ya jimbo na kitaifa na jinsi gani hizi zinapaswa kuoneshwa katika harakati kubwa ambayo Sekretarieti ya Sinodi ya Maaskofu imeanza katika wiki za hivi karibuni. Hatimaye kumekuwa na kuridhika kwa kuoneshwa kwa ripoti ya hivi karibuni ya Moneyval na kwa maendeleo kuhusu njia za usimamizi wa uchumi na kifedha wa Vatican. Mkutano ulimalizika saa 12 Jioni. Mkutano ujao umepangwa kufanyika mwezi Septemba.