Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amewatumia watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Morondova nchini Madagascar kwa kutabaruku Kanisa kuu na kuliweka chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi. Baba Mtakatifu Francisko amewatumia watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Morondova nchini Madagascar kwa kutabaruku Kanisa kuu na kuliweka chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi.  (Vatican Media)

Ujumbe wa Papa Francisko Jimbo Katoliki la Morondava, Madagascar

Baba Mtakatifu Francisko analipongeza Jimbo Katoliki la Morondova kwa kujielekeza zaidi katika kutoa elimu makini kwa vijana wa kizazi kipya; kwa kilimo cha umwagiliaji, ili kuweza kuwa na uhakika na usalama wa chakula sanjari na shughuli mbalimbali za kijamii na kidini kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo la Morondava. Mt. Yosefu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, Mei Mosi, 2021 ameungana na watu wa Mungu, Jimbo Katoliki la Morondava, nchini Madagascar, kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya Kutabaruku Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Morondava, ambalo limewekwa chini ya ulinzi na usimamizi wa Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi. Baba Mtakatifu analipongeza Jimbo hili kwa kujielekeza zaidi katika kutoa elimu makini kwa vijana wa kizazi kipya; kwa kilimo cha umwagiliaji, ili kuweza kuwa na uhakika na usalama wa chakula sanjari na shughuli mbalimbali za kijamii na kidini kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo la Morondava. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa njia ya video, anamwomba Mtakatifu Yosefu, awalinde na kuwategemeza na hatimaye, amewapatia baraka zake za kitume, kwa ajili ya kutabaruku Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu, Jimbo Katoliki la Morondava.

Kwa upande wake, Askofu Marie Fabien Raharilamboniaina wa Jimbo Katoliki la Morondava katika mahubiri yake, amekiri kwamba, Kanisa hili limejengwa na wafanyakazi zaidi ya 200 na kwamba, wananchi wanajisikia kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu. Ujenzi wa Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu Jimbo la Morondava ni matunda ya maadhimisho ya Sinodi ya Jimbo, iliyofanyika miaka 5 iliyopita. Lengo ni kuendelea kuinjilisha kwa ushuhuda wa maisha yanayosimikwa katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi. Askofu Marie Fabien Raharilamboniaina anasema, Mashirika mengi ya kitawa na kazi za kitume, yameitikia wito wa Baba Mtakatifu Francisko wa kutoka huko yalikokuwa yamejifungia, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mungu nchini Madagascar. Idadi kubwa ya Mashirika haya ya kitawa, inaliwezesha Kanisa kujielekeza zaidi katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvutoa na mashiko sanjari na kuwa karibu zaidi na waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Kuna idadi kubwa ya watoto wanaopata elimu yao ya msingi kutoka katika shule zinazoendeshwa na kusimamiwa na Jimbo. Kuna idadi kubwa ya watu wanaomwongokea Kristo Yesu na Kanisa hatua kwa hatua.

Sinodi ya Jimbo imelichangamotisha Jimbo kujenga nyumba ya Jimbo, Seminari Ndogo, Kituo cha Vijana na Kituo cha Katekesi. Ili kuwafikia watu wengi kwa mara moja, Jimbo Katoliki la Morondava limeanzisha pia Kituo cha Radio Katoliki. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 6-8 Septemba 2019 nchini Madagascar ilinogeshwa na kauli mbiu “Mpanzi wa amani na matumaini”, imekuwa ni kichocheo kukubwa kwa maendeleo fungamani nchini Madagascar. Mwamini mmoja kwa heshima ya Mtakatifu Yosefu ameliachia Kanisa urithi wake. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu akisema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Sherehe hii imehudhuriwa pia na Askofu mstaafu Donald Joseph Pelletier ambaye Mwezi Juni 2021 anasherehekea Miaka 90 ya kuzaliwa. Yote haya ni matukio ambayo yananogeshwa katika maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu.

Madagascar Ujumbe

 

03 May 2021, 14:06