Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anasema, vita kati ya Israeli na Palestina inayoendelea Ukanda wa Gaza ni hatari sana kwa usalama, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu katika nchi hizi mbili! Papa Francisko anasema, vita kati ya Israeli na Palestina inayoendelea Ukanda wa Gaza ni hatari sana kwa usalama, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu katika nchi hizi mbili!  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Vita Kati ya Palestina na Israeli ni Hatari Sana

Baba Mtakatifu Francisko kwa jina la Mwenyezi Mungu, aliyewaumba binadamu wote kwa sura na mfano wake; katika: usawa, haki, wajibu na utu sawa na kuwataka waishi kama ndugu wamoja; anawaomba viongozi na wahusika wote, warejeshe amani na utulivu kwa kusitisha mashambulizi ya silaha, tayari kujikita katika njia ya amani, kwa msaada wa Jumuiya ya Kimataifa! Vita ni Hatari!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, Jumapili tarehe 16 Mei 2021, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amesema kwamba, anafuatilia kwa umakini mkubwa hali tete ya machafuko ya kisiasa na mapigano ya kivita yanayoendelea kati ya Israeli na Palestina kwenye Ukanda wa Gaza. Mapigano haya yanaweza kupelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kuna watu wengi ambao wamejeruhiwa sana na kati yao wamo hata watoto wadogo. Inasikitisha kuona kwamba, watu wasiokuwa na hatia wamepoteza maisha. Haya ni matukio ambayo kamwe hayawezi kuvumiliwa. Vifo vya watu wasiokuwa na hatia ni alama kwamba, hakuna utashi thabiti wa kisiasa wa kutaka kuleta maendeleo kwa siku za usoni, bali wanataka kusababisha maafa. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, machafuko ya kisiasa na mapigano yanayoendelea kusambaa sehemu mbalimbali nchini Israeli ni “upanga wenye makali kuwili” unaotaka kuharibu: utulivu, mshikamano na udugu wa kibinadamu.

Itakuwa ni vigumu kuweza kurekebisha hali hii, ikiwa kama wadau wote wanaohusika hawatajizatiti katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kurejesha hali ya amani na utulivu. Chuki, uhasama na hali ya kulipizana kisasi ni hatari sana katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Haiwezekani kujenga msingi wa amani kwa kuwangamiza wengine! Baba Mtakatifu Francisko anawaomba wadau wote wanaohusika katika mgogoro na machafuko haya ya kivita kati ya Israeli na Palestina, kwa jina la Mwenyezi Mungu, aliyewaumba binadamu wote kwa sura na mfano wake; katika: usawa, haki, wajibu na utu sawa na kuwataka waishi kama ndugu wamoja; anawaomba viongozi na wahusika wote, warejeshe amani na utulivu kwa kusitisha mashambulizi ya silaha, tayari kujikita katika njia ya amani, kwa msaada wa Jumuiya ya Kimataifa.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili ya kuwaombea Waisraeli na Wapalestina, ili waweze kujielekeza na hatimaye kufanikiwa kupata njia ya majadiliano na msamaha, ili kwamba, waweze kuwa ni wajenzi wavumilivu wa haki na amani, ili hatua kwa hatua, waweze kupata matumaini, amani na utulivu ili waweze kuishi kama ndugu wamoja. Baba Mtakatifu, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, walisali na kuwaombea waathirika wa machafuko haya ya vita na hasa watoto. Bikira Maria Malkia wa amani, awaombee amani ya kweli!

Machafuko Nchi Takatifu

 

 

 

17 May 2021, 14:15