Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Yerusalemu unapaswa kuwa ni Mji mkuu wa Amani, Sala na Kitovu cha ujenzi wa umoja na mshikamano wa kidugu Papa Francisko: Yerusalemu unapaswa kuwa ni Mji mkuu wa Amani, Sala na Kitovu cha ujenzi wa umoja na mshikamano wa kidugu  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Yerusalemu ni Kitovu cha Amani, Sala na Udugu!

Mji wa Yerusalemu uendelee kubaki na kuheshimiwa kuwa ni Mji Mtakatifu wa Sala na Mahali pa watu kukutana ili kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu.. Mambo haya yakizingatiwa kwa dhati, Yerusalemu utakuwa ni mji wa udugu wa kibinadamu. Vita inachochea majanga. Umefika wakati wa kusitisha ghasia na kuacha amani iweze kuchukua mkondo wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mji wa Yerusalemu kimsingi ni kwa ajili ya mafao ya Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni Mji Mtakatifu unaoheshimiwa na waamini wa dini ya Kiyahudi, Kikristo na Kiislam. Kumbe, kwa waamini wa dini hizi, huu ni Mji mkuu wa maisha ya kiroho na kitovu cha majadiliano ya kidini, upatanisho na amani huko Mashariki ya Kati! Ili kuweza kupata ufumbuzi wa kudumu, kuna haja pia ya kuzingatia maoni ya viongozi wa kidini badala ya kujikita katika maamuzi ya kisiasa peke yake! Utakatifu, asili na tunu msingi za Mji wa Yerusalemu vinapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wengi. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu, Jumapili tarehe 9 Mei 2021, akiwa kwenye uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ameyaekeza mawazo yake kwenye mgogoro unaoendelea kufuka moshi mjini Yerusalemu. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, anafuatilia matukio yote haya kwa wasiwasi na hofu kubwa, ili kweli Mji wa Yerusalemu uendelee kubaki na kuheshimiwa kuwa ni Mji Mtakatifu wa Sala na Mahali pa watu kukutana ili kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu.

Yerusalemu ni mahali pa amani na sala kwa waamini wa dini mbalimbali duniani. Mambo haya yakizingatiwa kwa dhati, Yerusalemu unageukwa kuwa ni mji wa udugu wa kibinadamu. Vita inachochea vita na majanga katika maisha ya mwanadamu. Umefika wakati wa kusitisha ghasia na kuacha amani iweze kuchukua mkondo wake! Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Morocco, Jumamosi, tarehe 30 Machi 2019 pamoja na Mfalme Mohammed VI wa Morocco walitia sahihi kwenye Tamko la Mji Mtakatifu wa Yerusalemu na Mahali Pa Kuwakutanisha watu! Viongozi hawa wanatambua utakatifu, ukuu na umuhimu wa Mji wa Yerusalemu katika maisha ya kiroho ya waamini wa dini hizi tatu zinazomwabudu Mungu mmoja. Huu ni mji wa wa amani, amana na urithi wa binadamu wote, hususan waamini wa dini hizi tatu.

Ni mahali pa watu kukutana na kwamba, Yerusalemu ni mji wa amani, mahali ambapo watu wanapaswa kuishi kwa utulivu, kwa kuheshimiana na kuthaminiana ili kukuza na kudumisha majadiliano. Ni katika muktadha huu wa maisha ya kiroho na utambulisho wa kitamaduni, Mji Mtakatifu wa Yerusalemu unapaswa kulindwa na kuendelezwa. Ni matumaini ya viongozi hawa kwamba, Mji Mtakatifu wa Yerusalemu, utakuwa huru kwa waamini wa dini hizi tatu kuwa na uhakika wa kuendesha Ibada zao, ili Sala na sadaka zinazotolewa mahali hapa ziweze kumfikia Mwenyezi Mungu, Muumbaji, kwa ajili ya amani na udugu duniani!

Ghasia Yerusalemu
09 May 2021, 15:17