Papa Francisko:Hatuwezi kuwa wakristo wema ikiwa hatubaki na Yesu
Na Sr. Angela Rwezaula -Vatican.
Kabla ya sala ya Malkia wa Mbingu Dominika ya V ya Pasaka, tarehe 2 Mei 2021, Papa Francisko akiwa katika dirisha akiwageukia waamini na mahuji waliofika katika uwanja wa Mtakatifu Petro ametafakari Injili ya Siku. Papa Francisko amesema: Katika Injili ya Dominika ya V ya Pasaka, (Yh 15,1-8) Bwana anajionesha kuwa mzabibu wa kweli na anazungumza kuwa sisi ni matawi ambayo hayawezi kuishi bila kubaki yameungana na Yeye. Bwana amesema hivi: “Mimi ndimi mzabibu wa kweli na ninyi ni Matawi (Yh 15,5). Hakuna maisha bila matawi kwa maana yote yanategemeana. Matawi hayana nguvu kwa sababu yanategemea moja kwa moja kutoka mzabibu ambao ni chanzo cha kudumu kwake.
Bila kiini hakuna maisha:Mti na matawi vinahitajiana
Yesu anasisitiza neno la kukaa. Amerudia neno hilo mara saba katika kifungu cha Injili ya siku. Kabla ya kuacha ulimwengu huu na kwenda kwa Baba, Yesu anataka kuwahakikishia mitume wake ambao wanaweza kuendelea na muungano na Yeye. “kaeni ndani yangu nami ndani yenu ( Yhn 15, 4). Kukaa maana yake si kukaa bila kazi, kwa kulala ndani mwa Bwana, kuacha umbembelezwe na maisha. Hapana, siyo hivyo. Kubaki katika Yesu ambako Yesu anapendekeza kwetu, ni kubaki na uhai na kwa umoja. Kwa nini? Ni kwa sababu bila mzabibu hakuna maisha, haiwezekani kufanya lolote, kwa sababu kunahitaji kiini ili kukua na kuzaa matunda; lakini vilevile hata maisha yanahitaji mzabibu kwa sababu bila matunda kisiki cha mti hakiwezi kuwapo. Ni kuhitajiana, ni kubaki na muungano ili kutoa matunda. Ni kubaki katika Yesu na Yeye ndani mwetu. Awali ya yote sisi tunamwitaji Yeye. Bwana anataka kutwambia kuwa kabla ya kutimiza amri zake, kabla ya heri, kabla ya matendo ya huruma ni lazima kuungana na yeye, na kubaki na Yeye. Hatuwezi kuwa wakristo wema ikiwa hatubaki na Yesu. Na katika yeye tunaweza yote (Fil 4,13). Pamoja na Yeye tunaweza kufafanya kila kitu.
Yesu anahitaji ushuhuda wetu wa maisha ya kikristo
Papa Francisko amesema kuwa, lakini hata Yesu kama mti na matawi yake anahitaji sisi. Na labda inaweza kushangaza, kusema hivyo na kwa maana hiyo ni kujiuliza, ina maana gani kusema Yesu ana haja nasi? Yeye anahitaji ushuhuda wetu. Tunda mbalo tunapaswa kutoa kutoka kwetu ni ushuhuda wa maisha ya kikristo. Baada ya Yesu kupaa kwenda kwa Baba, ilibaki kazi ya wafuasi ambayo ni kazi yetu ya kuendelea kutangaza Injili, kwa maneno na matendo. Kwa kukaa karibu sana na Kristo, tunapokea zawadi za Roho Mtakatifuna kwa namna ambayo tunaweza kufanya vema kwa jirani na kwa jumuiya na Kanisa. Mti mwema unatambuliwa kwa matunda yake. Maisha Mema ya Kikristo yanatoa ushuhuda kwa Kristo. Na Je ni jinsi gani ya kuweza? Yesu anasema :“Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo nanyi mtatendewa” (Yh 15,7). Hiyo kweli ndiyo habari na uhakika kuwa kile abacho tutaomba tutapewa. Kuzaa matunda katika maisha yetu kunategemeana na sala.
Kupeleka ulimwenguni matunda ya upendo na amani
Tunaweza kuomba na kufikiria kama Yeye, kutenda kama Yeye, kutazama ulimwengu kama Yeye na kuwapenda kaka na dada, kunzia maskini na wanaoteseka kama alivyofanya Yeye na kuwapenda kama moyo wake na kutoa matunda mengi katika ulimwengu, ya wema, matunda ya upendo na matunda ya amani. Papa amehitimisha kwa kuomba kwa njia ya maombezi ya Bikira Maria. Yeye alibaki daima ameungana kabisa na Yesu na kutoa matunda mengi. Atusaidie Yeye kubaki katika Kristo, katika moyo wake , katika neno lake, kwa kushuhudia Bwana Mfufuka katika ulimwengu.