Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 12 Mei 2021 ametafakari kuhusu vikwazo vinavyoweza kujitokeza katika maisha ya sala na kwamba, sala ni mapambano makubwa. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 12 Mei 2021 ametafakari kuhusu vikwazo vinavyoweza kujitokeza katika maisha ya sala na kwamba, sala ni mapambano makubwa. 

Papa Francisko Fumbo la Sala: Vikwazo Vya Maisha ya Sala!

Papa Francisko: Kama yalivyo maisha ya Kikristo ndivyo ilivyo hata Sala ya Kikristo, si lele mama wala maji kwa glasi, yataka moyo! Haya ndiyo yanayobainishwa na waamini ambao wamekuwa ni mifano bora ya kuigwa katika maisha ya sala kutoka katika Maandiko Matakatifu na historia ya Kanisa. Kwa hakika hawa ni watu waliopambana sana na hali yao, hadi kikaeleweka katika Sala.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko bado anaendelea na Katekesi kuhusu Fumbo la Sala. Ameendelea kujikita katika: Sala na Utatu Mtakatifu kwa kujielekeza zaidi kwa Roho Mtakatifu anayewafunulia watu kumhusu Kristo Yesu. Roho Mtakatifu anao uwezo wa kuchunguza hata Mafumbo ya Mungu. Ni Mungu peke yake anayemjua Mungu kabisa. Kanisa linamsadiki Roho Mtakatifu kwa sababu ni Mungu na kamwe haliachi kutangaza imani kwa Mungu mmoja: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Kanisa ni Mama, Mwalimu na Shule ya Sala. Imani inapyaishwa kwa njia ya sala na kwamba, kuna mitindo mbalimbali ya sala, ili kuweza kuzungumza na Mwenyezi Mungu kuna: Sala ya Sauti, Sala Fikara au Tafakari na Taamuli. Baba Mtakatifu amekwisha kugusia kuhusu umuhimu wa utume wa sala na changamoto zake. Kanisa lina dhamana ya kusali na kufundisha namna ya kusali vizuri zaidi. Kanisa ni shule kuu ya sala. Mwishoni alihitimisha kwa kufanya tafakari kuhusu Sala ya Taamuli.

Baba Mtakatifu katika Katekesi yake, Jumatano tarehe 12 Mei 2021 kwenye Uwanja wa Mtakatifu Damas, ndani ya viunga vya mji wa Vatican, ametafakari kuhusu “Mapambano katika Sala ya Kikristo” na kwamba, sala si lelemama yataka “kifua kweli kweli”. Baba Mtakatifu amefurahia kukutana na umati wa waamini waliofika mjini Vatican kusikiliza tafakari yake. Katekesi ni muda wa waamini kukutana na kuonana na Khalifa wa Mtakatifu Petro, kusali na kuombeana daima! Tafakari hii imenogeshwa na Zaburi isemayo: “Ee Bwana, kwanini wasimama mbali? … BWANA, uondoke, Ee Mungu, uuinue mkono wako, Usiwasahau wanyonge. Kwani mdhalimu kumdharau Mungu. Akisema moyoni mwake, Hutapatiliza? Umeona, maana unaangalia madhara na jeuri, Uyatwae mkononi mwako. Mtu duni hukuachia nafsi yake, Maana umekuwa msaidizi wa yatima.” Zab. 10: 1. 12-14.

Baba Mtakatifu anasema kama yalivyo maisha ya Kikristo ndivyo ilivyo hata Sala ya Kikristo, si lele mama wala maji kwa glasi, yataka moyo! Haya ndiyo yanayobainishwa na waamini ambao wamekuwa ni mifano bora ya kuigwa katika maisha ya sala kutoka katika Maandiko Matakatifu na historia ya Kanisa. Kwa hakika hawa ni watu waliopambana sana na hali yao, hadi kikaeleweka katika Sala. Kwa hakika, Sala inampatia mwamini amani na utulivu wa ndani, lakini baada ya mapambano makali ya maisha na wakati mwingine, mapambano haya yanadumu kwa muda mrefu zaidi katika maisha. Kusali si jambo la rahisi, kwani mara nyingi mwamini anapoanza kujielekeza katika Sala, kuna mambo mengine yanayoingilia kati kutaka kumvuruga na kuonekana kana kana kwamba, ni mambo muhimu na yanayostahili kupewa kipaumbele cha kwanza. Huu ndio ushawishi wa Shetani, Ibilisi.

Watu wote wa Mungu katika hija ya maisha ya Sala wameonja furaha, amani na utulivu wa ndani katika sala, lakini pia wamekumbana na vizingiti katika kusali. Hii imekuwa ni fursa ya kupambana katika fadhila ya imani kwa njia ya Sala. Kuna baadhi ya watakatifu wamepambana katika sala kwa muda wa miaka mingi, bila kupata mafanikio yaliyokusudiwa, kiasi cha kudhani kwamba, Sala haina umuhimu wowote katika maisha kama mambo ndivyo yalivyokuwa! Mambo muhimu katika Sala ni: Ukimya, Sala yenyewe pamoja na kuzama katika maisha ya Sala na hata wakati mwingine, hali ya mwili inamfanya mtu kutojisikia kusali vyema zaidi. Wakati mwingine mazingira hayawavuti watu kusali vyema. Kuna watu ambao hawapendi hata kidogo kukaa peke yao Kanisani huku wakisali, wangependa kuwa nje ya Kanisa na huko wanajisikia vizuri zaidi. Kwa waamini wanaotaka kusali vyema watambue kwamba, imani si mchezo, kwani wakati mwingine wanaweza kujikuta wamepoteza mwelekeo wa maisha bila hata kuwa na mahali pa kufanyia rejea!

Mababa wa Kanisa wanataja vizuizi vya Sala pamoja na kuondokana na dhana potofu ya sala. Kuna uwezekano wa kufikia utupu wa kiakili na wengine wanadhani kwamba, sala ni hali za kimwili na maneno ya kiibada na kuna Wakristo ambao hawana muda hata kidogo kwa ajili ya Sala. Kuna watu wanaomtafuta Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sala, lakini wanavunjika moyo upesi kwa sababu hawajui kwamba, sala pia hutoka kwa Roho Mtakatifu, na wala si kutoka kwao peke yao. Kuna watu ambao hawawezi kukesha katika sala, wengine wanataka kuhakiki ukweli wa mambo kwa akili na sayansi na kusahau kwamba, hili ni fumbo linalopita ufahamu wa binadamu. Kuna baadhi ya waamini wanaipatia Sala thamani na kama haizai basi haina thamani. Sala lazima iwe ni kwa ajili ya Utukufu wa Mungu aliye hai na kweli na wala si kwa ajili ya kuyakimbia malimwengu. Kuna watu wanakatishwa tamaa kutokana na ukavu wakati wa sala na uchungu wa kutojiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu kutokana na: dhambi, kiburi na unyonge wa mwanadamu. Ili kushinda vizuizi vya Sala kuna haja ya kupambana kwa unyenyekevu, matumaini na udumifu. Rej. KKK 2726-2728.

Baba Mtakatifu anasema, Kitabu cha Mazoezi ya Kiroho cha Mtakatifu Inyasi wa Loyola, kimesheneni hekima na busara na kinamwezesha mwamini kuratibu vyema maisha yake. Ikumbukwe kwamba, wito wa maisha ya Kikristo ni mapambano endelevu yanayomtaka mwamini kubaki mwaminifu chini ya bendera ya Kristo Yesu Mfufuka! Shetani, Ibilisi daima yuko tayari kuwaangusha waamini ikiwa kama hawatajishikamanisha na Kristo Yesu. Waamini wakumbuke daima kwamba, katika mapambano ya maisha ya kiroho, Kristo Yesu yuko daima pamoja nao wala hawana sababu ya kujikatia tamaa! Kuna watakatifu kama Anthony Abate, Mtakatifu Athanasi, Askofu wa Alexandria, wanelezea kwa kina na mapana mapambano ya sala katika maisha ya Kikristo. Maisha ya Kikristo na Sala ni mapambano na hasa pale, mwamini anapokumbana na matatizo na changamoto za maisha! Sala na imani thabiti inaweza kufanya miujiza katika maisha ya mwanadamu. Kumbe, kuna haja kwa waamini kupambana kufa na kupona dhidi ya vikwazo vya sala, ili kupata neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Waamini wasitarajie mafanikio ya papo hapo, lakini daima wawe ni watu wa matumaini na kwamba, Mwenyezi Mungu atawatendea kadiri ya wema na huruma yake kwa muda anaoufahamu Mungu mwenyewe.

Vikwazo vya Sala
12 May 2021, 15:06

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >