Tafuta

Papa Francisko Fumbo la Sala: Roho Mtakatifu anawaimarisha waamini katika imani na kuwategemeza katika sala. Papa Francisko Fumbo la Sala: Roho Mtakatifu anawaimarisha waamini katika imani na kuwategemeza katika sala. 

Roho Mtakatifu Anaimarisha Imani na Kuwategemeza Katika Sala!

Roho Mtakatifu anaimarisha imani sanjari na kutegemeza sala za waamini. Huu ni mwaliko wa kuendelea kurejea mara kwa mara katika ile Sala ya Baba Yetu, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu ambayo aliwafundisha wafuasi wake, akiwataka kumwomba Mwenyezi Mungu ili “daima mapenzi yake yaweze kutendeka ndani mwao”, na wala si kama wanavyotaka wao! Roho Mt.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mama Kanisa katika Kanuni ya Imani anakiri na kufundisha kwamba, Roho Mtakatifu ni Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana: aliyenena kwa vinywa vya Manabii. Pentekoste ni siku ambayo Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume; mwanzo wa maisha na utume wa Kanisa, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia kwa kumtangaza Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Hii ni Sherehe ya waamini walei wanaohimizwa na Mama Kanisa kutoka kifua mbele, ili kuyatakatifuza malimwengu kwa karama na matunda ya Roho Mtakatifu. Waamini walei watambue kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 26 Mei 2021 amewakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, Kanisa Jumapili tarehe 23 Mei 2021 limeadhimisha Sherehe ya Pentekoste, zawadi ya Baba na Mwana kwa Kanisa lake.

Roho Mtakatifu anaimarisha imani sanjari na kutegemeza sala za waamini. Huu ni mwaliko wa kuendelea kurejea mara kwa mara katika ile Sala ya Baba Yetu, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu ambayo aliwafundisha wafuasi wake, akiwataka kumwomba Mwenyezi Mungu ili “daima mapenzi yake yaweze kutendeka ndani mwao”. Mapenzi ya Mwenyezi Mungu na wala si kama wanavyotaka wao! Waamini wawe na uhakika na matumaini kwamba, Mwenyezi Mungu anawasikiliza katika sala zao na atawajibu kwa muda muafaka. Baba Mtakatifu amewatakia wote furaha na amani kutoka kwa Kristo Yesu. Bikira Maria ni mfano wa utimilifu wa Kanisa katika maisha na utakatifu wake na kwamba, Bikira Maria ni ishara na matumaini thabiti na faraja kwa taifa la Mungu linalosafiri huku bondeni kwenye machozi! Mama Kanisa ameutenga Mwezi Mei kwa ajili ya kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kukimbilia chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria na hasa akina Mama wajawazito wanaotarajia kujifungua hivi karibuni.

Kwa ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu, awaombee kwa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, ili awakirimie neena na baraka ili waweze kupata mahitaji yao msingi. Abariki familia zao, shughuli zao za kimama na kitaaluma. Bikira Maria awe ni faraja na chemchemi ya matumaini kwa wale wote wanaoteseka na kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha. Waamini wajitahidi kujiaminisha kwa Bikira Maria kila siku ya maisha yao! Bikira Maria aliendelea kuandamana na Kanisa la Mwanzo katika sala wakati Mitume wakisubiria ujio wa Roho Mtakatifu, kumbe, Bikira Maria Mama wa Kanisa ni mfano bora wa sala. Roho Mtakatifu aendelee kuwahamasisha waamini kujenga utamaduni na moyo wa sala, kwa kuomba na kushukuru kwa neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Iwe ni fursa kwa waamini kumwachia nafasi Roho Mtakatifu aweze kutenda kama anavyotaka na waamini wawe tayari kutenda mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko amewapatia baraka zake za Kitume: wazee, vijana, wagonjwa na wanandoa wapya. Amewataka kujenga utamaduni wa kusali, ili kunogesha imani yao ili kuweza kuona na kupokea changamoto mamboleo kwa jicho la imani na matumaini.

Roho Mtakatifu

 

 

26 May 2021, 15:19