Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asikitishwa na ajali iliyotokea huko Stress-Mottarone, na kusababisha watu 14 kupoteza maisha. Papa Francisko asikitishwa na ajali iliyotokea huko Stress-Mottarone, na kusababisha watu 14 kupoteza maisha.  (AFP or licensors)

Papa Francisko Asikitishwa na Ajali Iliyotokea Mottarone, Italia

Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya ajali iliyotokea huko Stressa-Mottarone, tarehe 24 Mei 2021 na kusababisha watu 14 kupoteza maisha. anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa sala kwa wale wote walioguswa na msiba huu mzito. Hawa ni watu waliokuwa wamekwenda kufurahia Injili ya Uumbaji, lakini wamekutana uso kwa uso na mauti RIP.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Vyombo vya ulinzi na usalama nchini Italia vinawashikilia watu watatu wanaoshutumiwa kuhusika na ajali ya chombo cha usafiri wa anga kinachotumia nyaya kusafirishia abiria huko Stressa-Mottarone na kusababisha watu 14 kupoteza maisha kwa kuporomoka kutoka juu na kuanguka ondeni. Kati yao kuna watoto wawili na mtoto mmoja hali yake bado ni tete amelazwa hospitalini huko Torino. Kati ya watu waliotiwa pingu ni mmiliki wa Kampuni ya Ferrovie Mottarone, srl. Njia hii ya usafiri ilikuwa na itilafu, ikafanyiwa matengenezo, lakini hayakukamilika, lakini wahusika wakaamuru chombo kiendelee kufanya kazi, huku wakifahamu fika kwamba, breki za dharura zilikuwa hazifanyi kazi na hiki ndicho kimekuwa ni chanzo cha ajali ambayo imesababisha majonzi makubwa nchini Italia, wakati huu watu wanapojaribu kuanza maisha mapya baada ya kuishi kwenye karantini kwa zaidi ya mwaka mmoja!

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu Franco Giulio Brambilla wa Jimbo Katoliki la Novara, anasema, amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya ajali iliyotokea huko Stressa-Mottarone, tarehe 24 Mei 2021 majira ya mchana. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa sala kwa wale wote walioguswa na msiba huu mzito. Hawa ni watu waliokuwa wamekwenda kufurahia Injili ya Uumbaji, lakini wamekutana uso kwa uso na mauti. Baba Mtakatifu anaendelea kusali ili kumwombea mtoto Eitan ambaye amelazwa na hali yake bado ni tete. Baba Mtakatifu anaungana na waamini wa Jimbo Katoliki la Novara na watu wa Mungu nchini Italia katika ujumla wao, kuwaombolezea wale wote waliofariki dunia kutokana na ajali hii. Anawaombea marehemu wote waweze kupata usingizi wa amani kwenye makao ya uzima wa milele. Mwishoni, amewapatia wote baraka zake za kitume!

Papa Rambirambi
26 May 2021, 15:07