Tafuta

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican Jumapili tarehe 16 Mei 2021 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kumshukuru Mungu kwa Padre Francis Maria wa Msalaba Jordan kutangazwa kuwa ni Mwenyeheri. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican Jumapili tarehe 16 Mei 2021 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kumshukuru Mungu kwa Padre Francis Maria wa Msalaba Jordan kutangazwa kuwa ni Mwenyeheri. 

Mwenyeheri Padre Francis Maria wa Msalaba Jordan: Uinjilishaji

Ni Muasisi wa Shirika la Wasalvatoriani: Mapadre na Mabruda; Watawa na Waamini walei. Alikuwa Padre hodari katika kutangaza na kushuhudia Injili, kwa njia ya matendo ya huruma. Awe ni mfano na kiongozi bora kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaotumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo wa Mungu katika medani mbalimbali za maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kardinali Angelo Di Donatis, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 15 Mei 2021 amemtangaza Mtumishi wa Mungu Padre Francis Maria wa Msalaba Jordan kuwa ni Mwenyeheri. Ibada hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Lateran. Mwenyeheri Padre Francis Maria wa Msalaba Jordan katika maisha na utume wake alikazia mambo yafuatayo: Tafakari ya kina ya Maandiko Matakatifu; Kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa ajili ya wokovu wa watu wote; Wakristo wote wanaitwa na kuhimizwa kujenga umoja na mshikamano wa kitume ili kutangaza na kushuhudia matendo makuu katika maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, tarehe 16 Mei 2021 amewapongeza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema walioshiriki katika Ibada ya kumtangaza Mtumishi wa Mungu Padre Francis Maria wa Msalaba Jordan kuwa ni Mwenyeheri. Huyu ni Muasisi wa Shirika la Wasalvatoriani: Mapadre na Mabruda; Watawa na Waamini walei.

Mwenyeheri Padre Francis Maria wa Msalaba jordan alikuwa kwa hakika Padre hodari katika kutangaza na kushuhudia Injili, kwa njia ya matendo ya huruma. Awe ni mfano na kiongozi bora kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaotumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo wa Mungu katika medani mbalimbali za maisha. Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumapili, Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, tarehe 16 Mei 2021 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, mahali ambapo Mwenyeheri Padre Francis Maria wa Msalaba Jordan alikwenda kusali ili kujipatia utakatifu, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa Padre Francis Maria wa Msalaba Jordan kutangazwa Mwenyeheri. Kardinali Parolin katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa tafakari ya Neno la Mungu katika maisha waamini ili kuweza kumfahamu vyema Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu. Wajenge na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Wito wa Mwenyeheri Padre Francis Maria wa Msalaba Jordan ulisimikwa katika tunu msingi za Kiinjili!

Kardinali Pietro Parolin anasema, Mama Kanisa anaendelea kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kulijalia Kanisa wenyeheri na watakatifu wapya, wanaowachangamotisha waamini kujikita katika kulisoma, kulitafakari na hatimaye kulimwilisha katika uhalisia wa maisha yao kama chemchemi ya utakatifu na maisha ya uzima wa milele. “Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.” Yn. 17:3. Neno la Mungu linawajalia waamini maarifa ya kumfahamu Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai na Ukweli wenyewe. Huu ni mwaliko wa kulisoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha katika uhalisia wa maisha tayari kulitangaza na kulishuhudia. Mwenyeheri Padre Francis Maria wa Msalaba Jordan alipenda daima kuwahimiza waamini kusoma na kuyatafakari Maandiko Matakatifu, kama silaha madhubuti na ngome ya usalama wa maisha yao. Ni katika muktadha huu, Neno la Mungu linakuwa ni taa na dira ya maisha ili kupambana na kashfa na changamoto za Fumbo la Msalaba kama ilivyokuwa kwa wale Wanafunzi wa Emau waliobahatika kuandamana na Kristo Yesu katika safari yao ya matumaini ya Kikristo bila kumtambua kwani macho yao yalikuwa yamefumbwa!

Lakini, wakamtambua Yesu wakati wa kuumega mkate na hapo hapo akatoweka tena machoni pao! Nao wakaambiana, Je, mioyo yetu haikuwaka ndani yetu pale alipokuwa akizungumza na kufafanua Maandiko Matakatifu? Wanafunzi wa Emau walikuwa na majonzi makubwa mioyoni mwao kwani Fumbo la Msalaba, yaani mateso na kifo cha Kristo Yesu liliwaachia machungu makubwa kwani liliyeyusha matumaini na maisha yao; wakaonekana kushindwa vita hata kabla ya kuianza. Neno la Mungu anasema Kardinali Pietro Parolin linapaswa kuwa ni chemchemi ya matumaini mapya, dira na mwongozo katika sera na mikakati ya maisha na utume wa Kanisa, daima waamini wakijitahidi kuwa wamoja kama kielelezo cha Fumbo la Utatu Mtakatifu. Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Kristo Yesu anakaza kusema, “Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo.” Yn. 17: 11. Huu ni umoja na mshikamano unaosimikwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu kupendana na hatimaye, kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema sababu ya kwanza ya mchakato wa uinjilishaji ni upendo wa Yesu walioupokea, uzoefu wa ukombozi unaowasukuma daima kumpenda Kristo Yesu kwa upendo mkubwa zaidi, unaomfanya Kristo aweze kujulikana na kupendwa zaidi na watu. Huu ndio upendo unaobubujika kutoka katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Kichocheo bora kabisa kwa ajili ya kuwashirikisha wengine Injili kinatokana na kuitafakari Injili yenyewe kwa upendo kwa kuisoma kwa upendo. Hiki ndicho kiini cha tasaufi ya Biblia kinachomfunda mwamini ili kuishi na kufanya mapenzi ya Mungu kama ilivyokuwa kwa Mwenyeheri Padre Francis Maria wa Msalaba Jordan. Wasalvatorian katika maisha na utume wao sehemu mbalimbali za dunia, wazingatie wosia wa Mwenyeheri Padre Francis Maria wa Msalaba Jordan: “Bakini waaminifu na wana watiifu wa Mama yetu, Kanisa Takatifu la Roma. Fundisheni kile anachofundisha; aminini kile anachoamini; kataeni anachokataa. Pendaneni katika Roho Mtakatifu. Upendo wenu na uonekane kwa wote. Mnajua nimewapenda sana. Nawataka mpendane. Mjitakatifuze. Kueni na kuenea duniani kote mpaka mwisho wa nyakati.”

Kwa upande wake, Mheshimiwa Padre Milton Zonta, Mkuu wa Shirika la Wasalvatorian, amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya wito na utakatifu wa Mwenyeheri Padre Francis Maria wa Msalaba Jordan, chachu ya upyaisho wa karama, ili kuweza kujikita zaidi katika mchakato wa utume wa uinjilishaji. Ni mwaliko wa kuendeleza Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na maisha ya sala pamoja na kujiaminisha kwa nguvu tendaji za Roho Mtakatifu. Ibada hii ya Misa Takatifu, limekuwa ni tukio la kiekumene, kwa kuwashirikisha pia waamini kutoka katika Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo. Shirika la Wasalvatorian kwa sasa linajiandaa kuadhimisha Mwaka wa Mwenyeheri Padre Francis Maria wa Msalaba Jordan, changamoto ya kuendelea kuwa ni Wamisionari Mitume wa Yesu na mashuhuda wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa.

Padre Francis
16 May 2021, 16:23