Tafuta

Tarehe 26 Mei 2021 Mama Kanisa ameadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Filippo Neri Padre, Mlezi na chemchemi ya fura ya watu wa Mungu. Tarehe 26 Mei 2021 Mama Kanisa ameadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Filippo Neri Padre, Mlezi na chemchemi ya fura ya watu wa Mungu. 

Mtakatifu Filippo Neri, Padre, Mlezi na Furaha ya Watu wa Mungu

Mtakatifu Filippo Neri alikita maisha yake kwa kujenga mahusiano na mafungamano ya karibu na Yesu Kristo katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, aliyoiadhimisha kwa uchaji na ibada kuu. Alitumia muda mwingi kwa ajili ya Sakramenti ya Kitubio. Mara kwa mara alipenda kukutana na wale wote waliokuwa wanapata Sakramenti ya Kitubio na Ushauri wa kiroho kutoka kwake! Furaha

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi kuhusu Fumbo la Sala, Jumatano tarehe 26 Mei 2021 amewakumbusha waamini kwamba, Mama Kanisa alikuwa anaadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Filippo Neri, Padre. Kwa wengi anatambulikana kuwa ni “Mtakatifu wa furaha”. Furaha inayofariji ni zawadi kutoka kwa Mungu; kumbe iwaambate na kuwatajirisha waamini katika hija yao ya maisha. Mtakatifu Filippo Neri, Padre, Mlezi na Mwanaharakati alizaliwa tarehe 21 Julai 1515 Jimbo kuu la Firenze, Italia. Alipewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 23 Mei 1551 akiwa na umri wa miaka 18 tu! Papa Paolo V akamtangaza kuwa ni Mwenyeheri hapo tarehe 25 Mei 1615. Naye Papa Gregori XV tarehe 12 Machi 1622 akamtangaza kuwa ni Mtakatifu. Itakumbukwa kwamba, tarehe 26 Mei 2016, Mama Kanisa aliadhimisha Jubilei ya Miaka 500 tangu alipozaliwa. Tangu akiwa kijana, aliutumia muda wake mwingi kwa ajili ya kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa wa muda mrefu pamoja na kuwasaidia mahujaji maskini waliokuwa wanafanya hija ya kiroho mjini Roma, kiasi hata cha kuitwa kuwa ni “Mtume wa Roma”.

Ni Mtakatifu aliyeyakita maisha yake kwa kujenga mahusiano na mafungamano ya karibu na Yesu Kristo katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, aliyoiadhimisha kwa uchaji na ibada kuu. Alitumia muda mwingi kwa ajili ya Sakramenti ya Kitubio. Mara kwa mara alipenda kukutana na wale wote waliokuwa wanapata Sakramenti ya Kitubio na Ushauri wa kiroho kutoka kwake, kama sehemu muhimu ya katekesi na majiundo endelevu kwa waamini.  Ni muasisi wa vituo vya michezo “Oratorio” vinavyoongozwa na kuratibiwa na Mama Kanisa. Vituo hivi vilikuwa ni chemchemi ya sala, tafakari ya Neno la Mungu, mahali pa kusikiliza na kusikilizwa; mahali muafaka pa kujiandaa kwa ajili ya kupokea Sakramenti za Kanisa na majiundo makini kwa maisha ya Kikristo. Hii ilikuwa ni huduma ya upendo kwa maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Kutokana na utume wa Mtakatifu Filippo Neri, Kanisa likatoa kipaumbele cha pekee kwa ajili ya wokovu wa roho za watu, kwa kuwasaidia na kuwaongoza katika hija ya imani. Mtakatifu Filippo Neri akawa ni kiongozi wa waamini wengi waliojitosa kimasomaso kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo na wengine wakakumbatia maisha na utume wa Kipadre wakawa ni wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa.

Mtakatifu Filippo Neri alitoa kipaumbele cha kwanza kwa Sakramenti ya Upatanisho, akajitahidi kukaa katika kiti cha upendo na huruma ya Mungu hadi jioni kabisa. Lengo lilikuwa ni kuwasaidia waamini wake kufanya hija katika maisha ya Kikristo kwa kuwa na matumaini. Ni kiongozi aliyebahatika kuwa na karama nyingi, mtu wa watu, mwenye furaha, mpole na mkarimu; mambo ambayo yalipata chimbuko lake kutokana na umoja na mshikamano ambao aliouonesha na kuujenga na Kristo Yesu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Mtakatifu Filippo Neri alipenda kuwafundisha watu kusali kwa pamoja kama Jumuiya, akaonesha kwa mifano ya maisha yake maana ya kutubu na kufunga kama kielelezo cha furaha na amani ya ndani. Mtakatifu Filippo Neri, alikuwa ni mhubiri mahiri wa Neno la Mungu, aliyewaamini na kuwathamini watu, akawapatia nafasi ya kukua na kukomaa katika fadhila za Kikristo. Ni kielelezo makini cha utume endelevu wa Kanisa linalotumwa kushuhudia kwa wote upendo na huruma ya Mungu; mfano wa kuigwa katika maisha na utume wake wa Kipadre. Baba Mtakatifu Francisko katika kumbu kumbu ya miaka mia tano tangu alipozaliwa Mtakatifu Filippo Neri alibainisha kwamba, Mtakatifu Filippo Neri alikuwa ni mtu aliyependa kuishi katika ukweli na uhalisia wa mambo, akawafundisha watu umuhimu wa kumwilisha fadhila za Kikristo, nidhamu na dhamana ya kumpokea Yesu Kristo katika uhalisia wa maisha ya mtu.

Mtakatifu Filippo Neri alitambua kwamba, hija ya utakatifu wa maisha inajikita katika neema ya kubahatika kukutana na Yesu pamoja na watu wengine na kuwapokea kwa moyo wa ukarimu na mapendo. Baba Mtakatifu anawataka Watawa wa Shirika la Mtakatifu Filippo Neri kujifunza kutoka katika shule ya mwanzilishi wao, kwa kuwa ni watu wa sala na mashuhuda wanaowavuta wengine kwa Kristo. Vijana wa kizazi kipya wanahitaji kuona ushuhuda wa watu wanaosali na wanaofahamu kuwafundisha kusali vyema. Ni Mtakatifu aliyekuwa na Ibada ya pekee kwa Fumbo la Ekaristi Takatifu linalopaswa kuadhimishwa, kubudiwa na kumwilishwa katika maisha, kwani ni chemchemi inayobubujikia katika roho za watu. Kwa njia hii, Yesu Kristo anakuwa kweli ni chemchemi ya furaha na matumaini kwa waja wake. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaweka watawa na walei wote wa Shirika la Mtakatifu Filippo Neri chini ya ulinzi na tunza ya Maria, Bikira na Mama. Mtakatifu Filippo Neri alizoea kuwaambia vijana, kuweni wema mkitaka! “State buoni se potete”, hadi raha!

Mt. Filippo Neri
26 May 2021, 15:43