Tafuta

Vatican News
Kumbukizi la Miaka 160 ya Gazeti la L'Osservatore Romano na Miaka 90 ya Radio Vatican, Papa Francisko anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano Vatican kuondoa urasimu na ukiritimba katika mawasiliano. Kumbukizi la Miaka 160 ya Gazeti la L'Osservatore Romano na Miaka 90 ya Radio Vatican, Papa Francisko anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano Vatican kuondoa urasimu na ukiritimba katika mawasiliano.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Ondoeni Urasimu na Ukiritimba Katika Mawasiliano

Changamoto kubwa ambayo amelitaka Baraza la Kipapa la Mawasiliano kuishughulikia ni pamoja na kuondoa ukiritimba na urasimu, ili watu waweze kufanya kazi kwa uhuru kamili na kufanya maamuzi kwa kuwajibika barabara, tayari kushirikisha karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Ukiritimba na urasimu ni hatari sana kwa ustawi na maendeleo ya taasisi yoyote ile.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Miaka 160 tangu kuanzishwa kwa Gazeti la L’Osservatore Romano na Miaka 90 tangu kuanzishwa kwa Radio Vatican, Jumatatu tarehe 24 Mei 2021 ametembelea Jumba la Mawasiliano ya Vatican. Amefanya mahojiano maalum na Radio Vatican na hatimaye, akazungumza na wafanyakazi wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano. Tukio hili limekuwa likirushwa mubashara kutoka Radio Vatican. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano kwa kazi kubwa linalofanya katika maisha na utume wa Kanisa. Hata hivyo, Baba Mtakatifu ameonesha wasiwasi kuhusu idadi ya watu wanaosoma Gazeti la L’Osservatore Romano, wale wanaosikiliza Radio Vatican pamoja na kusoma habari mbalimbali zinazoandikwa na kutundikwa kwenye mitandao ya kijamii ya Vatican News. Lengo kubwa la Kanisa kuwekeza katika tasnia ya mawasiliano ya jamii ni kuhakikisha kwamba, ujumbe unawafikia watu wa Mungu popote pale walipo.

Ni rahisi sana kuwa na taasisi nzuri na yenye vifaa bora lakini kama ujumbe wake hauwafikii walengwa, hii ni hatari sana. Baba Mtakatifu amewataka wafanyakazi katika sekta ya mawasiliano kujiuliza kila siku, Je, ni watu wangapi wanasikiliza na kusoma ujumbe wao. Habari Njema ya Wokovu inapaswa kuwafikia watu wote wa Mungu mahali walipo! Je, ni watu wangapi wanapata Habari Njema ya Injili kutoka kwenye Gazeti la L’osservatore Romano na Radio Vatican? Baba Mtakatifu anakaza kusema hili ni swali msingi sana. Kama sehemu ya mchakato wa mageuzi makubwa yanayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican, matunda yake yameanza kuonekana. Vatican News imekuwa ni msaada mkubwa kwa wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Licha ya mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano, radio bado inaendelea kuchukua kipaumbele cha kwanza. Kuna watu wengi wanasikiliza kwa hakika.

Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru wafanyakazi wa Radio Vatican kutoka katika Program 43, ikiwemo pia Idhaa ya Kiswahili. Baba Mtakatifu amelipongeza Baraza la Kipapa la Mawasiliano kwa ukarabati mkubwa uliofanyika na kwamba, madhari ya kazi ni mazuri na yanavutia. Changamoto kubwa ambayo amelitaka Baraza la Kipapa la Mawasiliano kuishughulikia ni pamoja na kuondoa ukiritimba na urasimu, ili watu waweze kufanya kazi kwa uhuru kamili na kufanya maamuzi kwa kuwajibika barabara, tayari kushirikisha karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Ukiritimba na urasimu ni hatari sana kwa ustawi na maendeleo ya taasisi yoyote ile. Watu wajenge utamaduni wa kufanya kazi kwa kujisadaka bila ya kujibakiza, kwa ubunifu, daima wakipania kuboresha zaidi shughuli zao. Ikiwa kama juhudi zote hizi zinafanywa, lakini walengwa hawapati Habari Njema ya Wokovu, anasema Baba Mtakatifu hapo kuna kasoro kubwa! Watu wawe huru kutekeleza vyema shughuli zao, kiasi hata cha kuthubutu kukosea, hali inayohitaji: moyo mkuu na ujasiri wa kutosha!

Papa Hotuba
24 May 2021, 15:34