Tafuta

Papa Francisko akizungumza na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S wakati alipotembelea Radio Vatican tarehe 24 Mei 2021 Papa Francisko akizungumza na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S wakati alipotembelea Radio Vatican tarehe 24 Mei 2021 

Miaka 160 ya L'Osservatore Romano na Miaka 90 ya R. Vatican!

Baba Mtakatifu amevutwa sana na hisia aliposikiliza wafanyakazi kutoka Msumbiji, Vietnam na China walipokuwa wanajitambulisha mmoja mmoja. Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili, amemwomba Baba Mtakatifu kubariki Sanamu ya Mt. Yosefu, kama sehemu ya kumbukumbu ya ujio wake Radio Vatican sanjari na maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi la Miaka 160 tangu kuanzishwa kwa Gazeti la L’Osservatore Romano na Miaka 90 tangu kuanzishwa kwa Radio Vatican, Jumatatu tarehe 24 Mei 2021 ametembelea Jumba la Mawasiliano ya Vatican. Hii imekuwa ni fursa ya kukutana na kuzungumza na wafanyakazi mmoja baada ya mwingine sanjari na kubadilishana nao maneno “mawili, matatu”. Alipowasili amelakiwa na viongozi wakuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya jamii chini ya uongozi wa Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano. Ametembelea Gazeti la L’Osservatore Romano, akasikiliza historia, mchakato wa uzalishaji pamoja na waandishi wa habari wanaohusika katika uzalishaji wake. Baadaye, ametembelea Kikanisa cha Bikira Maria Kupashwa habari “La Cappella dell'Annunciazione” na hapa amesimama na kusali kwa kitambo kidogo katika ukimya mbele ya Tabernakulo. Baadaye, amesali sala aliyotunga kwa ajili ya Ujumbe wa Siku ya 55 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni iliyoadhimishwa na Mama Kanisa Jumapili, tarehe 16 Mei 2021 sanjari na Sherehe ya Bwana Kupaa Mbinguni na kunogeshwa na kauli mbiu “Njoo uone” Yn. 1:46.

“Bwana utufundishe kutoka katika ubinafsi wetu, tayari kuondoka na kwenda kutafuta ukweli. Utufundishe kwenda na kuangalia; utufundishe kusikiliza na kuondokana na maamuzi mbele, ili kutofanya maamuzi ya haraka kupita kiasi. Utufundishe kwenda mahali ambapo, hakuna mtu mwingine anapenda kwenda; utusaidie kuwa na muda wa kuweza kufahamu hayo yanayoendelea, kwa kutoa kipaumbele kwa mambo msingi na kamwe tusipoteze mwelekeo kwa mambo ya juu juu. Utujalie mwanga wa kutofautisha kile kinachoonekana na kuvutia kwa macho, kinyume kabisa cha ukweli. Utujalie neema ya kufahamu mahali unapoishi katika ulimwengu mamboleo, tayari kuambata ukweli na kusimulia kile tulichoona! Akiwa njiani kwenda kwenye Studio za Radio Vatican kwa mahojiano maalum, Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kukutana na kusalimiana na wafanyakazi wa Radio Vatican.

Baba Mtakatifu amevutwa sana na hisia aliposikiliza wafanyakazi kutoka Msumbiji, Vietnam na China walipokuwa wanajitambulisha mmoja mmoja. Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili, amemwomba Baba Mtakatifu kubariki Sanamu ya Mtakatifu Yosefu, kama sehemu ya kumbukumbu endelevu ya ujio wake Radio Vatican sanjari na maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu yaliyozinduliwa hapo tarehe 8 Desemba 2020 na yanatarajiwa kufungwa kwa kudemka hapo tarehe 8 Desemba 2021. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anapenda kuwahamasisha waamini kukuza na kudumisha Ibada kwa Mtakatifu Yosefu. Baba Mtakatifu ametembelea Idara ya Ufundi na Teknolojia. Hapa ni mahali ambapo kuna wataalam wa teknolojia ya mawasiliano wanapofanyia shughuli zao, ili kuhakikisha kwamba, kile kinachozalishwa na L’Osservatore Romano, Radio Vatican, Kituo cha Televisheni cha Vatican pamoja na Wavuti ya Vatican kinawafikia walengwa!

Papa Radio Vatican
24 May 2021, 15:13