Tafuta

Vatican News
Mfuko wa Centesimus Annus kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro ulianzishwa tarehe 5 Juni 1993 na Mtakatifu Yohane Paulo II, kumbukumbu endelevu tangu Papa Leo XIII alipochapisha Waraka wa Rerum Novarum. Mfuko wa Centesimus Annus kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro ulianzishwa tarehe 5 Juni 1993 na Mtakatifu Yohane Paulo II, kumbukumbu endelevu tangu Papa Leo XIII alipochapisha Waraka wa Rerum Novarum.  (Vatican Media)

Miaka 30 ya Mfuko wa Centesimus Annus wa Mt. Yohane Paulo II

Mfuko huu umeendelea kuwa nyenzo muhimu sana ya ushuhuda wa Kanisa katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu katika kipindi cha miaka 30 iliyopita! Mafundisho Jamii ya Kanisa ni muunganiko wa maisha na utume wake katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa ni: Mwalimu wa ukweli, imani na maadili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mfuko wa “Centesimus Annus” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, "CAPP", ulianzishwa rasmi tarehe 5 Juni 1993 na Mtakatifu Yohane Paulo II, kama kumbu kumbu endelevu tangu Papa Leo XIII alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Rerum Novarum” yaani “Mambo Mapya” msingi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa katika ulimwengu mambaoleo. Lengo la mfuko huu ni kufafanua na kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa katika uhalisia wa maisha ya watu, kwa kuwasaidia: wafanyabiashara na wataalam katika medani mbalimbali kufahamu shughuli zinazotekelezwa na Vatican katika kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kwa kujielekeza zaidi katika: Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mfuko huu umeendelea kuwa nyenzo muhimu sana ya ushuhuda wa Kanisa katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu katika kipindi cha miaka 30 iliyopita! Mafundisho Jamii ya Kanisa ni muunganiko wa maisha na utume wake katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa ni: Mama na Mwalimu wa ukweli, imani na maadili.

Ni katika muktadha wa Injili na Imani kwa watu kutokana na ukosefu wa haki, Kanisa haliwezi kujiweka pembeni katika masuala ya kijamii. Mamlaka fundishi ya Kanisa: “Magisterium” kwa nyakati mbalimbali katika maisha na historia yake yamefafanualia masuala jamii kwa kuzingatia Maandiko Matakatifu, Kanuni Maadili na Utu wema pamoja na Mapokeo ya Mama Kanisa. Hii ni sehemu ya mchakato unaopania kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa katika uhalisia wa maisha ya watu, kama sehemu ya imani tendaji! Kanisa linapania kutangaza yale yanayokubalika na kukataa yale yasiyofaa mintarafu: imani, maadili na utu wema. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanakita mizizi yake katika Mwanga wa Injili na yanaendelea kupyaishwa kwa kusoma alama za nyakati. Waraka wake wa Kitume “Rerum Novarum” yaani “Mambo Mapya” ulijielekeza zaidi katika kupembua kuhusu suala la ajira lililoibuka kutokana na kinzani kati ya mtaji na nguvukazi; hali duni ya maisha ya wafanyakazi; Umuhimu wa kazi kama kielelezo cha utu na heshima ya binadamu sanjari na utimilifu wake. Uligusia kuhusu mali na ushirikiano kati ya watu wa Mataifa. Yote haya ni kutaka kuonesha kwamba mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kukombolewa kwa Damu Azizi ya Kristo Yesu aliyomwanga Msalabani. Hapa mtu nafsi anakaziwa sana!

Mama Kanisa anaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 30 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka wake wa Kitume Centesimus Annus, Mei Mosi, 1991. Waraka huu ulikuwa ni kumbukumbu ya Miaka 100 tangu Papa Leo XIII alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Rerum Novarum” yaani “Mambo Mapya”. Mtakatifu Yohane Paulo II alikazia pamoja na mambo mengine kuhusu mambo msingi yaliyojadiliwa na “Rerum Novarum”, mambo mapya yaliyojitokeza baadaye kuhusu hali ya wafanyakazi; umuhimu wa kudumisha kanuni auni na mshikamano; utu, heshima na haki msingi za wafanyakazi pamoja na umuhimu wa vyama vya wafanyakazi katika kudai haki na kutekeleza nyajibu zao, kwani haki na wajibu ni chanda na pete. Mtakatifu Yohane Paulo II aligusia pia kuhusu mali binafsi na hatima ya mali katika ujumla wake; Serikali na tamaduni mbalimbali na kwamba, Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake.

Anna Maria Tarantola, Rais wa Mfuko wa “Centesimus Annus” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, "CAPP", anasema, Mtakatifu Yohane Paulo II anatoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu katika Waraka wake huo wa Kitume. Kanuni auni iongoze na kuratibisha ushirikiano na mshikamano kati ya nchi tajiri na maskini duniani. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanakita msingi wake katika Mwanga wa Injili, maadili na utu wema, daima Kanisa likiendelea kusoma alama za nyakati, kwa kuzingatia haki na msamaha; mambo yanayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Anna Maria Tarantola anasema, changamoto mamboleo katika Mafundisho Jamii ya Kanisa ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linaendelea kujipyaisha katika matumizi ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika ulimwengu wa kidigitali. Kanisa liendelee kujifunza faida na hasara za ulimwengu wa kidigitali, ili hatimaye kuangilia jinsi ambavyo Kanuni za Mafundisho Jamii ya Kanisa zinavyoweza kutoa huduma kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni wakati wa kujenga na kudumisha misingi ya usawa katika haki na ukweli. Baba Mtakatifu Francisko ni mfano bora wa kuìgwa katka medani mbali mbali za maisha.

Miaka 30 Centesimus Annus

 

06 May 2021, 14:56