Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 14 Mei 2021 amewaambia washiriki wa mkutano wa Jukwaa la Vyama vya Kifamilia Nchini Italia kwamba, watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu na matumaini ya taifa! Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 14 Mei 2021 amewaambia washiriki wa mkutano wa Jukwaa la Vyama vya Kifamilia Nchini Italia kwamba, watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu na matumaini ya taifa! 

Papa Francisko: Watoto ni Zawadi ya Mungu na Matumaini ya Taifa!

Papa Francisko anasema, inasikitisha kuona kwamba, wanawake wajawazito hawana nafasi katika ulimwengu wa wafanyakazi. Watoto ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kumbe, wanapaswa kuthaminiwa, ili kukuza mwingiliano kati ya kizazi kimoja na kingine. Amekazia pia umuhimu wa elimu na mshikamano katika kukuza na kudumisha sera za maisha ya familia! Watoto

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Jukwaa la Vyama vya Kifamilia Nchini Italia, Ijumaa tarehe 14 Mei 2021 limefanya mkutano wa siku moja ili kupembua kuhusu hali ya jumla ya uzazi nchini Italia kwa kujielekeza zaidi katika mada zilizogusia kuhusu: kiwango cha uzazi chenye mvuto; vizazi vipya ni chanzo kizuri cha uwekezaji na kwamba, watoto ni uzuri unaopaswa kusimuliwa! Mkutano huu umefunguliwa na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Prof. Mario Draghi, Waziri mkuu wa Italia. Mkutano umeratibiwa na Bwana Gigi de Palo, Rais wa Jukwaa la Vyama vya Kifamilia Nchini Italia “Forum delle Associazioni Familiari” na viongozi mbalimbali wa Italia, wamechagia mawazo yao. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amejielekeza zaidi kuhusu: Misigano inayojitokeza kwenye familia, nyumbani na maeneo ya kazi. Inasikitisha kuona kwamba, wanawake wajawazito hawana nafasi katika ulimwengu wa wafanyakazi. Watoto ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kumbe, wanapaswa kuthaminiwa, ili kukuza mwingiliano kati ya kizazi kimoja na kingine. Amekazia pia umuhimu wa elimu na mshikamano katika kukuza na kudumisha sera za maisha ya familia.

Italia katika miaka ya hivi karibuni anasema Baba Mtakatifu Francisko imejikuta ikiwa na idadi ndogo sana ya watoto wanaozaliwa na matokeo yake, idadi ya wazee nchini Italia inazidi kuongezeka maradufu. Idadi ya watoto waliozaliwa kwa Mwaka 2020 imekuwa ni chini sana ikilinganishwa na miaka mingine. Hii si kwa sababu ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, peke yake, bali ni ukame ambao umeanza kuonesha makali yake katika maisha ya watu. Baba Mtakatifu anawaalika watu wa Mungu nchini Italia kuwekeza katika watoto, kwani watoto ni kumbukumbu inayoielekeza jamii kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Misigano inayotokea maeneo ya kazi, majumbani na shule kwa upande wa watoto, wanaookoa jahazi ni babu na bibi! Kumbe, kuna haja ya kuwekeza katika familia, kwa kuhakikisha kwamba, vijana wanapata fursa za ajira, ili waweze kuanzisha na kuzitegemeza familia zao. Umefika wakati wa kuondokana na vitendo vinavyowatweza wanawake wenye mimba katika ulimwengu wa wafanyakazi.

Watoto ni amana na utajiri wa jamii, kumbe, familia zinapaswa kuwezeshwa kiuchumi. Familia inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa sasa na kwa siku za usoni, ili kufufua hali ya Italia katika sekta mbalimbali za maisha. Baba Mtakatifu anasema, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kupokelewa kwa moyo wa shukrani na hivyo kuijengea mazingira ya kuweza kuwarithisha wengine. Wazazi wanapaswa kuwa na subira ya kupata mtoto na kumpenda kadiri ya uwezo wao! Idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa ni dalili za uchoyo na ubinafsi na matokeo yake, ni idadi ya wazee kuongezeka maradufu. Watu wajenge utamaduni wa kuthamini maisha zaidi na wala si vitu! Watoto ni amana na utajiri wa jamii, kumbe, kuna haja ya kuwa na ujasiri wa kuchagua Injili ya uhai. Maisha ni zawadi ya kwanza kabisa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kuna haja ya kujenga mafungamano endelevu kati ya vizazi, kwa kuwajengea vijana imani na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi, kwa kubadili hali na mtazamo kuhusu familia.

Mafungamano endelevu ni mchakato unaowajibisha ili kujenga madaraja yanayowakutanisha watu na ukuaji wao. Shule ni mahali ambapo wanafunzi kwa kukutana na wengine wanakuza na kudumisha madaraja yanayowakutanisha watu. Hapa ni mahali pa makuzi ya kiroho na kiakili; ujasiri na moyo wa kujitoa sadaka, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengine. Kwa bahati mbaya kuna watu wanadhani kwamba, lengo la elimu bora ni kupata fedha na mafanikio makubwa katika maisha. Mwelekeo wa namna hii kuhusu elimu ni saratani inayoipekenya jamii katika ulimwengu mamboleo. Kuna haja ya kujenga na kudumisha mshikamano wa miundombinu, ili kupambana na umaskini pamoja na kuzijengea uwezo familia. Mchakato huu unawezekana ikiwa kama kuna sera bora na uchumi ambao ni rafiki kwa familia, hali ambayo itasaidia kuchochea watoto kuzaliwa ndani ya familia. Familia inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya Kitaifa. Vijana wajengewe uwezo wa kupata ajira, makazi, usalama na uhakika wa maisha yao kwa sasa na kwa siku za usoni. Ili kufikia lengo hili, kuna haja kwa Serikali kujenga mazingira bora zaidi yatakowavuta wafanyabiashara kuwekeza zaidi, ili kutengeneza fursa za ajira na hivyo kuendeleza maisha.

Wafanyakazi walipwe ujira wanaostahili, ili kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa na familia katika ujumla wake. Hii ni changamoto kubwa si tu kwa Italia bali kwa nchi nyingi duniani, ambazo zina rasilimali nyingi lakini maskini wa kutupwa katika matumaini. Mshikamano unapaswa kuoneshwa katika huduma ya mawasiliano ya jamii, ili kusaidia mchakato wa makuzi ya binadamu. Watu wajifunze kuheshimiwa na kuthaminiana; walinde na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Uchu wa mali, madaraka na mafanikio ya chapuchapu ni hatari kwa mafao ya wengi ndani ya familia. Mchakato wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu umwilishwe katika: michezo, sanaa na utamaduni, ili kusaidia kunogesha upendo ndani ya familia ili hatimaye, kuweza kupata watoto. Utamaduni wa mazuri yajayo mbeleni unajengeka katika misingi ya umoja, uzuri wa sadaka na majitoleo na wala si katika: uchoyo na ubinafsi; mahitaji na haki binafsi.

Papa Familia
15 May 2021, 07:43