Tafuta

Umoja wa Vijana wa Skauti nchini Ufaransa "Scouts Unitaires de France" wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya ushuhuda wa imani na mshikamano wa umoja wa udugu wa kibinadamu. Umoja wa Vijana wa Skauti nchini Ufaransa "Scouts Unitaires de France" wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya ushuhuda wa imani na mshikamano wa umoja wa udugu wa kibinadamu. 

Jubilei ya Miaka 50 ya Umoja wa Vijana wa Skauti Nchini Ufaransa

Papa Francisko anawashukuru na kuwapongeza wanandoa, wanaoendelea kushuhudia uzuri, ukuu na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia. Chama cha Skauti, kimsingi ni kwa ajili ya huduma ya upendo kwa jirani na kulisaidia Kanisa, kutangaza na kushuhudia ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika udugu, kiielelezo cha imani, chachu muhimu sana inayoweza kupyaisha jamii! Skauti

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa limewekeza sana katika Umoja wa Vijana wa Skauti nchini Ufaransa, “Scouts Unitaires de France” kwa kutambua kwamba, Vijana wa Skauti ni wadau wakuu katika mchakato wa uinjilishaji na ujenzi wa jamii unaofumbatwa katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Ili Kanisa liweze kuwa na vijana wanaojipambanua katika mchakato wa uinjilishaji mpya, wanapaswa mbele yao kuwa na mifano bora ya watu watakaowapatia imani, matumaini na habari muhimu wanazohitaji katika safari ya maisha yao. Leo hii kutokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 kuna hatari kwamba, vijana wakakosa fursa za kuweza kukutana ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu pamoja na kuanzisha urafiki mpya na vijana wengine. Vijana wa Skauti wamekuwa ni mfano bora wa kuigwa katika malezi na majiundo muhimu ya vijana wa kizazi kipya, kwani hapa vijana wanapewa mwaliko wa kuwa na ndoto na namna ya kutekeleza ndoto hii; kwa kuwa na ujasiri na matumaini kwa siku za usoni. Vijana wa Skauti wanajifunza kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja; tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ulinzi wa ndugu zao wadogo, ili kuwasaidia kwa uvumilivu mkubwa kutambua na hatimaye, kuziwezesha karama na mapaji yao kuzaa matunda yanayokusudiwa.

Kimsingi, Vijana wa Skauti wanaonesha kwamba, kuna umuhimu wa watu kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii yanayosimikwa katika utu na heshima ya binadamu na wala si tu kwa njia ya mitandao ya kijamii, bali katika uhalisia wa maisha. Jambo hili ni muhimu sana katika majiundo ya mtu binafsi pamoja na tabia yake. Hayo yameelezwa na Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa, tarehe 14 Mei 2021 alipokutana na kuzungumza na Umoja wa Vijana wa Skauti nchini Ufaransa, “Scouts Unitaires de France” wakati huu, Umoja huu unapoadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wanandoa, wanaoendelea kushuhudia uzuri, ukuu na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia. Chama cha Skauti, kimsingi ni kwa ajili ya huduma ya upendo kwa jirani na kulisaidia Kanisa, kutangaza na kushuhudia ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika udugu wa kibinadamu. Hili ni lengo wanalopaswa kulishuhudia mahali popote pale wanapokwenda na kama kielelezo cha imani, chachu muhimu sana inayoweza kupyaisha jamii mamboleo.

Baba Mtakatifu anawataka Vijana wa Skauti kuwa na nguvu na waaminifu, kwa kujielekeza zaidi katika kutafuta na kumwilisha tunu msingi za kiutu na Kiinjili; wazi kwa ajili ya kushirikiana na kushikamana na vijana wengine. Kwa njia hii Skauti itaweza kuleta mabadiliko makubwa katika jamii wanamoishi. Baba Mtakatifu anawapongeza Skauti kwa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Kwani uhusiano mwema na mazingira unadai kutokudhohofisha nyanja ya kijamii ya kuwa wazi kwa wengine na kwa namna ya pekee kabisa wanao wajibu wa kuwa wazi mbele za Mwenyezi Mungu. Rejea Laudato si, 119. Vijana wanatakiwa wasikate tamaa na hatimaye kumezwa na malimwengu, bali wawe ni vijana wenye mawazo na ndoto muhimu katika maisha yao. Watambue kwamba, wanaitwa na kutumwa kwenda kutangaza Habari Njema ya Wokovu, hasa miongoni mwa vijana wenzao, kwenye “vijiwe vyao” na katika ulimwengu wa michezo na sanaa; wanapokuwa wanavinjari na wenzao au wanapokuwa kazini. Kote huku, ni mahali muafaka pa kushirikishana furaha ya Injili inayowauhisha.

Kristo Yesu anawataka vijana ili wawe ni wafuasi wake, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya Matumaini, kwa sababu anategemea sana nguvu na ujasiri, ari na mwamko wao wa ujana.  Vijana wajitahidi kuhakikisha kwamba, Skauti ya Kikatoliki inakuwa ni jukwaa la kupandikiza matumaini sanjari na kugundua tena umuhimu wa maisha ya kijumuiya. Baba Mtakatifu anaushukuru Umoja wa Vijana wa Skauti nchini Ufaransa, “Scouts Unitaires de France” kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Miaka yote hii, imekuwa ni ushuhuda wa huduma kwa ndugu zao na Kanisa katika ujumla wake kwa njia ya sala. Jubilei, kiwe ni kipindi cha kupyaisha tena dhamana na wajibu wao kama sehemu ya urithi kutoka kwa watangulizi wao. Skauti isaidie kuwajengea vijana uhuru kamili na unaowawajibisha, kwa kuwaheshimu na kuwathamini jirani zao pamoja na mazingira wanamoishi.

Skauti Ufaransa
15 May 2021, 09:01