Tafuta

2020.10.14 La Madonna che scioglie i nodi (Knotenlöserin) 2020.10.14 La Madonna che scioglie i nodi (Knotenlöserin) 

Bikira Maria Mfungua Mafundo Utuombee Sisi Wanao!

Waamini wanamwomba Bikira Maria afungue mafundo yanayokwamisha mahusiano ya kijamii; mafundo ya upweke hasi yanayowafanya watu kuchungulia kaburi kwa kukata tamaa! Afungue mafundo ya watu kutowajali jirani zao kwa kuwageuzia kisogo! Bikira Maria afungue mafundo ya ukosefu wa ajira unaowatumbukiza vijana katika ujambazi na ukosefu wa maadili na utu wema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema, ikiwa kama watu watasahau mema, nyoyo zao, zitasinyaa na “kunyauka kama kigae”. Lakini kama Bikira Maria, wakikumbuka matendo makuu ya Mungu katika maisha yao, hata walau mara moja kwa sikuwanakuwa wanasali, sala ya kumsifu Mungu, nyoyo zao zipapanuka na furaha ya ndani kuongezeka maradufu! Tarehe 31 Mei ya Kila Mwaka, Kanisa linaadhimisha Sikukuu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeth. Bikira Maria ni Sanduku la Agano Jipya na la milele anaondoka kwa haraka kwenda kumtembelea binamu yake Elizabeth. Na kupokelewa kama Mama wa Mungu Rej. Lk 1:36, 39-56. Huu ni ushuhuda wa fadhila; ni mkutano kati ya Agano la Kale na Agano Jipya; huruma na upendo wa Mungu unaookoa, unaoganga na kuponya. Huu ni ushuhuda wa Injili ya upendo na matumaini, kwa watu wa Agano la Kale na kama ilivyo kwa watu wa ulimwengu mamboleo! Huu ni mwendelezo wa utenzi wa sifa, shukrani na furaha ya ujio wa Masiha, Mkombozi wa Ulimwengu unaotambuliwa na Yohane Mbatizaji anayeruka kwa furaha tumboni mwa Mama yake.

Ni Mama wa Mkombozi anayekwenda kumtembelea Elizabeth. Hapa wanawake wawili wanaohifadhi ndani mwao Injili ya uhai wanakutana. Bikira Maria ni mtumishi wa Bwana na Elizabeth ni kielelezo cha matumaini mapya kwa Waisraeli. Bikira Maria anakwenda kwa haraka kumsalimia Elizabeth, kielelezo makini cha huduma ya upendo kwa jirani na mfano wa kuigwa hasa katika ulimwengu mamboleo unaogubikwa na ubinafsi na uchoyo wa kutisha! Na kwa Sikukuu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeth, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanamwomba Bikira Maria afungue mafundo yanayokwamisha mahusiano na mafungamano ya kijamii; mafundo ya upweke hasi yanayowafanya watu kuchungulia kaburi kwa kukata tamaa! Afungue mafundo ya watu kutowajali jirani zao kwa kuwageuzia kisogo! Bikira Maria afungue mafundo ya ukosefu wa fursa za ajira zinazowafanya vijana wengi kutumbukia katika ujambazi na ukosefu wa maadili na utu wema.

Bikira Maria afungue mafundo ya kinzani, vipigo na ukatili wa kijinsia ndani ya familia ili familia ziweze kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani. Bikira Maria asaidie kufungua fundo la umaskini, ili kukoleza utu, heshima na haki msingi za binadamu. Afungue sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, ili watu waweze kuwa na ari na mwamko mpya wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kama chemchemi ya furaha, imani, matumaini na mapendo!

Bikira Maria

 

 

31 May 2021, 15:56