Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amemkaribisha rasmi Kardinali Mauro Gambetti, Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kumuaga Kardinali Angelo Comastri aliyemaliza muda wake. Baba Mtakatifu Francisko amemkaribisha rasmi Kardinali Mauro Gambetti, Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kumuaga Kardinali Angelo Comastri aliyemaliza muda wake. 

Pasaka ya Bwana: Shukrani kutoka Kwa Papa Francisko: Wahudumu!

Papa amemshukuru Kardinali Angelo Comastri aliyeng’atuka kutoka madarakani. Kwa muda wa miaka 16 Kardinali Comastri amekuwa mhudumu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ameonesha karama zake za shughuli za kichungaji, amewashirikisha tasaufi na kuhubiri bila kuchoka. Kardinali Comastri amekuwa ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko aliridhia ombi lililowasilishwa kwake na Kardinali Angelo Comastri, Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican la kutaka kung’atuka kutoka madarakani. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu akamteua Kardinali Mauro Gambetti, O.F.M, CONV., kuwa Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Sherehe ya Pasaka ya Bwana, tarehe 4 Aprili 2021 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ametoa shukrani zake za dhati kwa wale wote waliohusika kufanikisha maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kumkaribisha rasmi Kardinali Mauro Gambetti Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Amemshukuru kwa kukubali na utayari wake kwa ajili ya huduma kwa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Kanisa ambalo lina umuhimu wa pekee kwa Wakristo wote. Imekuwa ni nafasi kwa Baba Mtakatifu kumshukuru hadharani Kardinali Angelo Comastri aliyeng’atuka kutoka madarakani, kutokana na kufikia umri wa miaka 78. Kwa muda wa miaka 16 Kardinali Comastri amekuwa mhudumu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika kipindi chote hiki, ameonesha karama zake za shughuli za kichungaji, amewashirikisha watu wa Mungu tasaufi yake na kuhubiri bila kuchoka. Kardinali Angelo Comastri amekuwa ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, Yeye mwenyewe apende kumlipa kwa huduma hii makini. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru wote wanaofanya utume wao kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Papa Shukrani

 

04 April 2021, 14:25