Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema, utunzaji bora wa mazingira ni dhamana na wajibu wa kila mtu kadiri ya nafasi yake katika jamii; utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Papa Francisko asema, utunzaji bora wa mazingira ni dhamana na wajibu wa kila mtu kadiri ya nafasi yake katika jamii; utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. 

Papa Francisko: Utunzaji Bora wa Mazingira ni Dhamana ya Wote!

Papa Francisko kwa UNESCO: Kimsingi, ongezeko la joto duniani linaendelea kusababisha madhara makubwa kwa maskini, jambo linalohitaji jibu makini ili kukabiliana na athari za kijamii na uharibifu wa mazingira, ili kwa pamoja kuweza kujizatiti katika kulinda na kutunza mazingira, ili kuboresha maisha, afya, mawasiliano, usalama wa nishati pamoja na kutengeneza fursa za ajira.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, bayianuai ni muhimu sana katika mchakato wa maboresho ya ekolojia. Kumbe, kuna haja ya kuunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa kwa kulinda asilimia 30% ya dunia kama hifadhi maalum hadi kufikia mwaka 2030, ili kuondokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na kupotea kwa bayianuai. Mkutano wa Kunming, China (Cop15) unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 17 hadi 30 Mei 2021, unapaswa kuwa ni kielelezo makini kitakachoiwezesha dunia kuwa ni mahali pa binadamu kupata utimilifu wa maisha kadiri ya mapenzi ya Mungu. Haki ikiwa kichwani mwa binadamu, binadamu anaweza kuisaidia dunia kuboreka zaidi. Watu mahalia walindwe dhidi ya makampuni makubwa yanayoendelea kufaidika kwa: utajiri wa madini, mafuta ghafi, mbao na mazao ghafi ya kilimo. Utawala thabiti wa sheria kitaifa na kimataifa unahitajika ili kudhibiti ukwapuaji mkubwa wa rasilimali na madini pamoja na kuhakikisha kwamba, haki inatendeka kwa wale wote wanaoathirika na vitendo hivi.

Ni katika muktadha huu, hivi karibuni Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, kama sehemu ya maadhimisho ya “Jubilei ya Miaka 50 ya Programu ya Binadamu na Uso wa Dunia”, liliandaa jukwaa la majadiliano miongoni mwa wadau mbalimbali. Maadhimisho haya yamenogeshwa na kauli mbiu “Sayari Yetu, Na Siku Zetu Zijazo, Miaka 50 ya Programu ya Binadamu na Uso wa Dunia”. Mkutano huu umefanyika kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kumtumia ujumbe maalum Bi Audrey Azoulay Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, uliosomwa kwake na Monsinyo Francesco Follo, Mwakilishi wa Vatican kwenye Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO. Huu ni mchango wa Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote dhidi ya athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi zinazoendelea kusababisha umaskini mkubwa sehemu mbalimbali za dunia. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kukabiliana na changamoto hizi kwa kujikita katika kanuni maadili, utu wema na uwajibikaji wa kisayansi.

Katika mchakato huu, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, ili kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ili kuweza kufikia lengo hili, Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna haja kuzingatia kanuni maadili yanayokita mizizi yake katika mshikamano na sera ya upendo, ili kulinda na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa upendo ambako hakuna “virusi” vya utandawazi usiowajali wengine au matumizi mabaya ya rasilimali za dunia! Kimsingi, ongezeko la joto duniani linaendelea kusababisha madhara makubwa kwa maskini, jambo linalohitaji jibu makini ili kukabiliana na athari za kijamii na uharibifu wa mazingira, ili kwa pamoja kuweza kujizatiti katika kulinda na kutunza mazingira, ili kuboresha maisha, afya, mawasiliano, usalama wa nishati pamoja na kutengeneza fursa za ajira. Makubaliano ya Mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2015, Cop21 uliofanyika nchini Ufaransa yanapaswa kutekelezwa kwa dhati, ili kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazotokana na kuongezeka kwa hewa ya ukaa na joto duniani.

Hii ni changamoto ya kimaadili zaidi kuliko hata inavyodhaniwa kujikita katika taaluma, kwa kuwekeza zaidi katika elimu ili kuwasaidia vijana wa kizazi kipya kufanya mabadiliko katika mtindo wa maisha yao, kwa kuheshimu mazingira nyumba ya wote, ambayo hadi wakati huu, yametumiwa vibaya! Vijana wafundwe kutunza mazingira, kuwaheshimu watu wengine na kuanza kujielekeza kuwa na mfumo mpya wa maisha mintarafu uzalishaji na ulaji. Baba Mtakatifu anaishukuru UNESCO kwani haya ni kati ya mambo ambayo yamejadiliwa pia katika jukwaa hilo la UNESCO, kwa kuwashirikisha wataalam zaidi. Mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi yanapaswa kuwashirikisha watu wote, kwa kufanya upembuzi yakinifu kuhusu mfumo wa maendeleo kwa nyakati hizi, kwa kuonesha ujasiri wa kurekebisha pale ambapo inakwenda kombo! Ni wakati wa kutoa majibu muafaka kuhusu athari za ongezeko la joto duniani, kwani hii ni dhamana ya kimaadili. Bila kutekeleza maazimio haya kwa vitendo, Nchi na watu maskini wataathirika zaidi. Mapambano haya yavishirikishe vyama vya kiraia, sekta binafsi, wanafunzi wa vyuo vikuu, wataalam na wanayasansi, ili wote kwa pamoja waweze kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kundi hili ni lile la watu wanaoguswa zaidi, kiasi hata cha kutafuta njia mpya na endelevu zitakazosaidia kuleta mfumo mpya wa ulaji, kielelezo makini cha watu wanaosikiliza na kujibu “Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini”. Mchango wao unapaswa kuthaminiwa na kutekelezwa na wanasiasa ikiwa kama maamuzi yao ni ya haki na ya muda mrefu zaidi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, muda unaendelea kuyoyoma kwa kasi kwa Jumuiya ya Kimataifa kutafuta suluhu ya kudumu kuhusu janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Hii ni changamoto inayoiwajibisha Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na ustawi, mafao na maendeleo ya binadamu wote. Majukwaa ya namna hii, yasaidie kuleta mabadiliko yanayokusudiwa katika mchakato wa mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, sanjari na kupigana vita dhidi ya umaskini, ili hatimaye, kunogesha maendeleo fungamani ya binadamu!

Papa UNESCO
11 April 2021, 14:38