Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza waamini kutenga muda kwa ajili ya sala na tafakari ya Neno la Mungu, ili kuonja uwepo wa Mungu katika maisha yao! Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza waamini kutenga muda kwa ajili ya sala na tafakari ya Neno la Mungu, ili kuonja uwepo wa Mungu katika maisha yao! 

Papa Francisko: Tengeni Muda Wa: Sala na Tafakari ya Neno la Mungu

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa njia ya Sala na tafakari makini, waamini wanaweza kufanana na Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya waja wake kwa njia ya Roho Mtakatifu. Yesu ni lengo kuu la maisha ya waamini wake na chemchemi ya furaha ya daima. Sala na Tafakari ni muhtasari wa Ufunuo wa Mungu unaonafsishwa katika uhalisia wa maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 28 Aprili 2021 baada ya Katekesi yake kuhusu Fumbo la Sala; kwa kujiekeleza zaidi katika Sala kama Tafakari kwa Mkristo kwani huu ni muhtasari wa Ufunuo wa Mungu unaonafsishwa katika maisha ya mwamini. Amesema fikara hushughulisha wazo, dhana, hisi na tamaa. Msukumo huu ni wa lazima ili kunafsisha maswali ya imani, kuamsha wongofu wa moyo na hatimaye, kuimarisha utashi wa kumfuata Kristo Yesu: “Sequela Christi”. Na kwa njia ya Sala na tafakari makini, waamini wanaweza kufanana na Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya waja wake kwa njia ya Roho Mtakatifu. Kristo Yesu, ndiye lengo kuu la maisha ya waamini wake na chemchemi ya furaha ya daima.

Baba Mtakatifu amewakumbusha watu wa Mungu kutoka nchini Poland kwamba, tarehe 3 Mei 2021, nchini Poland wanaadhimisha Sikukuu ya Bikira Maria Malkia wa Poland. Hiki ni cheo ambacho watu wa Mungu nchini Poland wamempatia Bikira Maria Mama wa Mungu tangu kunako karne ya kumi na saba. Watu wa Mungu nchini Poland wanajiaminisha na kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, huku wakiendelea kujizatiti kikamilifu kuhudumia na kujenga Ufalme wa Mungu. Hii ni kumbukumbu ambayo Mababa wa Poland waliifanya kwa Bikira Maria Malkia wa Poland kwenye Madhabahu ya Jasna Gòra (Yasina Gura). Baba Mtakatifu anawaalika watu wa Mungu hata katika kipindi hiki chenye changamoto na matatizo mengi, waendelee kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria: “Lolote atakalowaambia Kristo Yesu, fanyeni”. Rej. Yn. 2:5.

Baba Mtakatifu anasema, Sala inamwezesha Kristo Yesu kuunganika tena na waja wake katika uhalisia wa maisha ya kila siku. anawaalika waamini kutenga muda kwa ajili ya sala na tafakari ya Mafumbo ya maisha ya Kristo Yesu hapa duniani. Ni kwa njia hii, wataweza kupyaisha na kuimarisha imani na matumaini yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake sanjari na kuwasha moto wa upendo. Tafakari ya Kikristo itawawezesha waamini kuzama zaidi katika mambo msingi ya imani na hivyo kupata mang’amuzi ya uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake. Kristo Yesu ni mahali pa wokovu na furaha ya kweli katika maisha.

Katika Kipindi hiki cha Pasaka waamini waendelee kujibidiisha kupyaisha ukarimu wa huduma kwa Mungu na jirani. Wazee, vijana, wagonjwa na wanandoa wapya wawe ni mashuhuda wa upendo wa Kristo Yesu Mfufuka na waendelee kujichotea neema na baraka kutoka katika Madonda yake matakatifu. Katika furaha ya Kristo Mfufuka, Baba Mtakatifu amewapatia waamini wote baraka za upendo wenye huruma unaobubujika kutoka kwenye Fumbo la Utatu Mtakatifu. Watambue kwamba, Roho Mtakatifu ni kisima cha neema, nguvu na faraja katika maisha ya mwamini.

Malkia wa Poland

 

 

 

28 April 2021, 14:59