Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Chanjo ni sehemu ya utekelezaji wa mchakato wa ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kupambana na changamoto mamboleo. Papa Francisko: Chanjo ni sehemu ya utekelezaji wa mchakato wa ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kupambana na changamoto mamboleo.  (ANSA)

Papa: Chanjo ni Kielelezo cha Mshikamano wa Udugu!

Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya watu maskini 800 na wale wanaoishi katika mazingira magumu na tete wamekwisha kupewa chanjo awamu ya kwanza na kwamba, hadi kufikia Pasaka ya Bwana kwa Mwaka 2021, watu zaidi ya 1200 watakuwa wamepewa chanjo. Baba Mtakatifu amesalimiana na madaktari, wauguzi na watu waliokuwa wanasubiri kupewa chanjo. Mshikamano wa kidugu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, chanjo ni sehemu ya utekelezaji wa mchakato wa ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu. Kwa njia hii, watu wanajenga udugu na ujirani mwema kwa njia ya chanjo, ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza, ili hatimaye, kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani. Huu ni utamaduni unaosababisha maafa na utengano! Ujirani mwema ni dhana inayopaswa kufanyiwa kazi ili kujenga umoja na mafungamano ya kijamii, Kitaifa na ndani ya Kanisa katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba pamoja na tabia ya kutowajali wala kuwathamini wengine, umeendelea kukuzwa kutokana na maambukizi makubwa ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Maskini, wazee, wakimbizi na wahamiaji wameendelea kuteseka sana kutokana na ugonjwa wa UVIKO-19 sehemu mbalimbali za dunia. Ni katika muktadha huu, Ijumaa kuu, tarehe 2 Aprili 2021, Baba Mtakatifu ametembelea Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican kushuhudia jinsi Vatican inavyoendelea kutoa chanjo dhidi Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 kwa maskini na watu wanaoishi katika mazingira magumu. Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya watu maskini 800 wamekwisha kupewa chanjo awamu ya kwanza na kwamba, hadi kufikia Pasaka ya Bwana kwa Mwaka 2021, watu zaidi ya 1200 watakuwa wamepewa chanjo. Baba Mtakatifu amesalimiana na madaktari, wauguzi na watu waliokuwa wanasubiri kupewa chanjo.

Chanjo lazima ithibitishwe kuwa salama na yenye ufanisi kwa idadi kubwa ya watu kabla ya kuidhinishwa na kuingizwa kwenye programu za chanjo sehemu mbalimbali za dunia. Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa linasema ni wajibu wa kimaadili na kiutu kuhakikisha kwamba, chanjo zinazotengenezwa ni salama na zenye ufanisi. Chanjo hizi zitengenezwe kiasi kwamba, zinaweza kukubalika kutumiwa na watu hata kutoka katika Nchi zinazoendelea bila shaka wala wasi wasi. Bila chanjo hizi kuwafikia wananchi hawa, huu utakuwa ni mwelekeo wa ubaguzi na ukosefu wa haki katika matumizi ya rasilimali za dunia! Haki ya huduma bora ya afya, iwe ni kipimo cha upendo unaopaswa kushuhudiwa na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Chanjo Vatican

 

02 April 2021, 15:29