Tafuta

Mtakatifu Theresa wa Avila, Bikira na Mwalimu wa Kanisa ni mwanamke wa kwanza kutangazwa kuwa Mwalimu wa Kanisa kutokana na moyo wake wa sala, mafundisho, umoja na udugu wa kibinadamu. Mtakatifu Theresa wa Avila, Bikira na Mwalimu wa Kanisa ni mwanamke wa kwanza kutangazwa kuwa Mwalimu wa Kanisa kutokana na moyo wake wa sala, mafundisho, umoja na udugu wa kibinadamu. 

Mtakatifu Theresa wa Avila, Bikira na Mwalimu wa Kanisa! Sifa Zake!

Baba Mtakatifu amekazia wito wa utakatifu wa maisha, utamaduni wa sala kwa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwaletea mageuzi ya maisha ya ndani pamoja na kuendeleza kipaji cha ubunifu na upyaisho wa maisha. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema kwamba, watu wote wanaitwa kuwa wakamilifu, kama Baba yao wa Mbinguni alivyo mkamilifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mtakatifu Paulo VI, tarehe 27 Septemba 1970, alimtangaza Mtakatifu Theresa wa Avila kuwa ni Mwalimu wa Kanisa. Sifa kuu za Mtakatifu Theresa wa Avila kama Mwalimu wa Kanisa ni kwamba, ni mtawa aliyebahatika kuwa na mwanga angavu wa hekima inayosimikwa katika utakatifu wa maisha, ukweli na imani thabiti, zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu. Mtakatifu Theresa wa Avila, alikirimiwa nguvu na upendo wa ajabu unaojionesha katika sala na maandiko yake. Kwa hakika alikuwa ni “mwanamke wa shoka katika maisha ya: Sala, Liturujia ya Kanisa na Mafundisho yake, kiasi cha kujisikia kuwa pamoja na Kanisa, kama shuhuda na chombo cha upatanisho na mageuzi makubwa ndani ya Kanisa. Utume wake katika maisha ya kiroho, ni amana na utajiri mkubwa kwa Kanisa unaowafanya waamini wote kujisikia kuwa ni sehemu ya watoto wa Mungu na Kanisa. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko ameandika ujumbe kwa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Avila, kinapoadhimisha Kongamano la Kimataifa, kama sehemu ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Mtakatifu Theresa wa Avila, Bikira atangazwe kuwa ni Mwalimu wa Kanisa. Kongamano hili limeanza tarehe 12 na limehitimishwa Alhamisi tarehe 15 Aprili 2021. Mtakatifu Paulo VI alimtaja Mtakatifu Theresa wa Avila kuwa ni “Mwanamke wa shoka” kutokana na moyo wake wa sala, utekelezaji wa maisha na utume wake ndani ya Kanisa, kwa kujinyenyekeza kwa Fumbo la Utatu Mtakatifu katika upendo thabiti.

Akatangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya maisha yake. Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanamwachia Roho Mtakatifu ili aweze kuugeuza uso wa nchi. Kimsingi ni kwa njia ya ushuhuda wa watakatifu wa Mungu, ulimwengu unaweza kufikia utimilifu wake. Katika ujumbe wake, Baba Mtakatifu amekazia wito wa utakatifu wa maisha, utamaduni wa sala kwa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwaletea mageuzi ya maisha ya ndani pamoja na kuendeleza kipaji cha ubunifu na upyaisho wa maisha. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema kwamba, watu wote wanaitwa kuwa wakamilifu, kama Baba yao wa Mbinguni alivyo mkamilifu. Waamini wote huitwa kufikia utimilifu wa maisha ya Kikristo na ukamilifu wa upendo kwa njia ya utakatifu wa maisha, watumie nguvu zao kadiri ya kipimo cha kipawa cha Kristo Yesu, wafuate nyayo na mfano wake, wawe watii kwa mapenzi ya Mungu na wajisadake kwa huduma kwa jirani. Kwa njia hii, utakatifu wa watu wa Mungu utazaa matunda tele kama historia ya Kanisa inavyoshuhudia kwa njia ya maisha ya watakatifu wengi. Rej. LG, 40.

Watakatifu wanawahamasisha na kuwachangamotisha watu wa Mungu kuwa watakatifu, lakini kila mtu anaweza kuwa mtakatifu kadiri ya wito na maisha yake, kwa kukutana na Kristo Yesu katika maisha. Baba Mtakatifu anasema, Mtakatifu Theresa wa Avila alikuwa anawahimiza watawa wake kujenga moyo wa sala kama njia ya kuungana na Kristo katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao. Hiki kilikuwa ni kielelezo cha ndoa ya maisha ya kiroho inayonogeshwa kwa maisha ya sala. Sala ni tiba ya maisha ya kiroho inayorutubishwa kwa kufunga, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini. Kumbe, utamaduni wa sala ni amana na utajiri mkubwa kutoka kwa Mtakatifu Theresa wa Avila, na hasa zaidi wanaojisikia kuwa ni wadhambi na wadhaifu wanaohitaji huruma na upendo wa Mungu unaoganga, kuponya na kuokoa. Huruma na upendo wa Mungu unavuka mipaka yote ya ubaya anaoweza kutenda mwanadamu na kwamba, Mwenyezi Mungu hachoki kusamehe na kusahau. Jambo la msingi ni kwa waamini kukimbilia msamaha wa Mungu katika hija ya maisha yao ya kila siku. Mtakatifu Theresa wa Avila anasema daima ataimba na kutangaza huruma ya Mungu katika maisha yake.

Baba Mtakatifu anahitimisha sifa za Mtakatifu Theresa wa Avila kwa kusema kwamba, kwa hakika alikuwa ni mwanamke wa pekee sana, aliyekirimiwa kipaji cha ubunifu, alichokitumia kupyaisha maisha ya kijumuiya. Aliwataka watawa wake kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika upendo, urafiki na kusaidiana katika hali zote, huku wakitambua kwamba, wao ni wachumba wa Kristo Yesu Mfufuka. Aliwataka watawa wake kuifanya sala kuwa ni chemchemi ya matumaini. Katika kipindi hiki cha utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, watu wanahitaji kuwa na marafiki wa kweli. Watu wanaoweza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya jirani zao na hivyo kuondokana na uchoyo na ubinafsi. Sala inawawezesha waamini kutambua ukuu wa Mungu anayetembea na waja wake katika maisha. Uwepo wa Mungu unawawezesha kukabiliana na changamoto na matatizo mbalimbali ya maisha.

Mt. Theresa wa Avila
16 April 2021, 15:42