Tafuta

Maadhimisho ya Juma Kuu: Ijumaa Kuu, Mama Kanisa anatafakari na kuadhimisha mateso na kifo cha Kristo Yesu kinacholeta wokovu! Maadhimisho ya Juma Kuu: Ijumaa Kuu, Mama Kanisa anatafakari na kuadhimisha mateso na kifo cha Kristo Yesu kinacholeta wokovu! 

Ijumaa Kuu: Udugu wa Kibinadamu Mintarafu Fumbo la Msalaba!

Kardinali Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa, amefafanua maana ya udugu wa kibinadamu mintarafu Fumbo la Msalaba. Udugu miongoni mwa Wakatoliki na Wakristo kwa ujumla umejeruhiwa kutokana na misimamo ya kisiasa na kiitikadi. Udugu wa kibinadamu unasimikwa katika: utu, heshima na haki msingi za binadamu mintarafu Injili ya Kristo Yesu Mfufuka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Ijumaa Kuu ni siku ya toba, kufunga, kusali na kutafakari Maandiko Matakatifu, ili kushiriki Njia ya Msalaba na hatimaye, kusimama chini Msalaba ili kuadhimisha: mateso na kifo cha Kristo Msalabani kinacholeta wokovu kwa binadamu. Ni siku ya kumwabudu Kristo aliyeteswa na hatimaye kulazwa Msalabani kwa ajili ya wokovu wa binadamu. Ni siku ya kuonesha mshikamano wa udugu wa upendo kwa: wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa na kutelekezwa pembezoni mwa jamii. Ni siku ya kuwakumbuka wahanga wa vita, ghasia na watoto waliotolewa mimba. Mbele ya Msalaba wa Kristo Yesu, waamini wanahimizwa kuwakumbuka na kuwaombea, wale wote wanaoelemewa ni Misalaba ya maisha, ili waweze kuonja huruma na faraja kutoka kwa Kristo Yesu.

Malengo ya Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni: Kuhamasisha ujenzi wa mshikamano wa kidugu unaoratibiwa na kanuni auni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni dhana inayokumbatia maisha ya kifamilia, kijamii, kitaifa na kimataifa. Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya kujenga na kudumisha tasaufi ya udugu wa kibinadamu kama chombo cha kufanyia kazi katika medani za kimataifa, ili kusaidia kupata suluhu ya matatizo yanayoikumba Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni msaada mkubwa katika kupambana na changamoto mamboleo kama vile: Vita na kinzani mbali mbali; baa la njaa na umaskini duniani pamoja na athari za uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Kipaumbele cha kwanza ni ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, mshikamano wa kidugu usaidie ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya Jumuitya ya Kimataifa kama ilivyo pia miongoni mwa wananchi wenyewe. Ujasiri na ukarimu ni mambo yanayohitajika ili kufikia malengo ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kardinali Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa katika maadhimisho ya Liturujia ya Neno, Ijumaa kuu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 2 Aprili 2021, ameongozwa na sehemu ya Maandiko Matakatifu isemayo “Ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi” Rum 8:29. Amefafanua maana ya udugu wa kibinadamu mintarafu Fumbo la Msalaba. Udugu miongoni mwa Wakatoliki na Wakristo kwa ujumla umejeruhiwa kutokana na misimamo wa kisiasa na kiitikadi. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” umepata umaarufu kwa muda mfupi kabisa, kiasi kwamba, familia ya Mungu na taasisi mbalimbali zinajitahidi kuhakikisha kwamba, zinamwilisha malengo yaliyobainishwa na Baba Mtakatifu katika Waraka wake wa Kitume, “Fratelli tutti” ambao kwa sasa kwa lugha ya Kilatini unajulikana kama “Fratres Omnes”. Uhalisia na udugu wa kibinadamu unapata chimbuko lake katika utu, heshima na haki msingi za binadamu kama zinavyofafanuliwa katika Injili ya Kristo Yesu.

Jambo la msingi ni mahusiano na mafungamano ya kijamii yanayoibuliwa baada ya kukutana na Fumbo la maisha kutoka kwa Kristo Yesu. Maadhimisho ya Ijumaa kuu ni changamoto ya kutafakari udugu wa kibinadamu uliozinduliwa kwa mateso na kifo cha Kristo Yesu kiletacho wokovu pale Mlimani Kalvari. Agano Jipya linatumia neno “adelfos” maana yake “ndugu wa damu moja”, watu wa taifa moja na Mtakatifu Paulo anasema kuna ndugu na jamaa zake kwa jinsi ya mwili, ambao ni Waisraeli. Rej. Rum 9:3. Ndugu ni neno linalowajuisha watu wote bila ubaguzi wa kijinsia. Wakati mwingine lina maanisha jirani na wale wote wenye uhitaji. Na kwa Kristo Yesu, ndugu ni wafuasi wake wote, wanaokubali mafundisho yake, imani, Roho Mtakatifu sanjari na mwelekeo mpya wa maisha ya Kristo Mfufuka. Siku ile ya kwanza ya Juma, Kristo Mfufuka alipokutana na Maria Madgalene, alimtuma akawaambie ndugu zake kwamba, anapaa kwenda kwa Baba yake, kwa Mwenyezi Mungu ambaye pia ni Baba na Mungu wao! Rej. Yn 20:17. Mwandishi wa Waraka kwa Waebrania anasema, Kristo Yesu ndiye anayetakasa na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii, haoni haya kuwaita ndugu zake. Rej. Ebr. 2:11.

Baada ya Pasaka, neno ndugu linatumika kama Jumuiya ya waamini na wamoja katika Damu Azizi ya Kristo Yesu. Wote ni wamoja kwa sababu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni wamoja kwa Damu Azizi ya Kristo kwa sababu binadamu wote wamekombolewa kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kwa wafu! Kardinali Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa anakaza kusema, udugu wa kibinadamu unawabidiisha Wakristo kutafuta, kujenga na kudumisha haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Ni udugu unaohamasisha mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene. Lakini huu pia ni udugu unaowaunganisha waamini wote wa Kanisa Katoliki. Makanisa yamegawanyika, ndiyo maana mchakato wa majadiliano ya kiekumene bado unaendelea kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko, ili siku moja wote wawe wamoja. Kanisa ni moja, takatifu, katoliki na la mitume.

Hii ni sehemu ya imani ya Kanisa Katoliki ambalo udugu wake umejeruhiwa. Si kwa sababu ya mafundisho tanzu ya Kanisa au maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa kwa ajili ya wokovu wa watu. Bali ni majeraha yanayotokana na sera na mifumo ya kisiasa. Udugu na umoja wa Kanisa Katoliki umejeruhiwa kutokana na misimamo na ushabiki binafsi wa kisiasa. Hii ni dhambi katika msingi wake. Waamini wanapaswa kuchunguza dhamiri zao, kutubu na kumwongokea Mungu, ili kujenga na kudumisha udugu na umoja wa Kanisa Katoliki. Kinzani na mipasuko ni kazi ya Shetani, Ibilisi. Hata nyakati za Kristo Yesu kulikuwepo na mifumo pamoja na misimamo mbalimbali ya kisiasa na kijamii. Walikuwepo: Mafarisayo, Masadukayo, Waherodiani na Wazeloti, yaani waamini wenye ari waliopambana kutaka kuwang’oa Warumi.

Kati yao, wote, hakuna kikundi hata kimoja, ambacho Kristo Yesu alijishikamanisha nacho! Waamini wa Kanisa la Mwanzo wakafuata msimamo huu pia. Viongozi wakuu wa Kanisa, wakawa ni mfano bora wa kuigwa, kwa kuwachunga kondoo wote na wala si sehemu tu ya kondoo wa Kristo. Viongozi wa Kanisa wanapaswa kuchunguza dhamiri zao na kuona ikiwa kama wanawaongoza waamini wao kadiri ya matamanio halali ya Kristo Yesu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walitoa kipaumbele cha kwanza kwa waamini walei kuhakikisha kwamba, wanayatakatifuza malimwengu kwa uwepo na ushiriki wao mkamilifu katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Dhamana na wajibu huu, wanautekeleza kwa kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha yao, kwa kusoma alama za nyakati, kwa kuheshimu mazingira na kwamba, wajibu huu utekelezwe kwa njia ya amani.

Kanisa Katoliki linayo dhamana ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kujenga umoja wa Makanisa. Kanisa liwe mstari wa mbele kulinda na kutetea wanyonge na wale wote wanaodhulumiwa na kunyanyaswa; waathirika wa vita na mauaji ya kimbari. Kanisa liwe ni sauati ya watu wasiokuwa na sauti ndani ya jamii, ili hatimaye, Kanisa liwe ni chombo cha matumaini na wokovu wa binadamu wote. Khalifa wa Mtakatifu Petro anahimizwa na Kristo Yesu mwenyewe kuwaimarisha ndugu zake katika imani. Huu ni wajibu unaotekelezwa kwa njia ya hija za kitume, kama ile ambayo imetekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq. Kristo Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani ni chombo cha umoja wa watoto wa Mungu waliotawanyika sehemu mbalimbali za dunia. “Ee Bwana Yesu Kristo, uliyewaambia Mitume wako: nawaachieni amani, nawapeni amani yangu: usizitazame dhambi zetu ila tu imani ya Kanisa lako: ulijalie amani na umoja kama yalivyo mapenzi yako. Unayeishi na kutawala, daima na milele”. Amina.

Ijumaa kuu
02 April 2021, 18:20