Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Alhamisi Kuu, amebariki Mafuta Matakatifu na kukazia umuhimu wa kutangaza Habari Njema kwa njia ya ushuhuda wa maisha na kwamba, Msalaba ni sehemu ya wito na utume wao. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Alhamisi Kuu, amebariki Mafuta Matakatifu na kukazia umuhimu wa kutangaza Habari Njema kwa njia ya ushuhuda wa maisha na kwamba, Msalaba ni sehemu ya wito na utume wao.  (Vatican Media)

Juma Kuu: Alhamisi Kuu: Daraja Takatifu ya Upadre: Msalaba!

Papa Francisko katika Ibada ya Kubariki Mafuta Matakatifu katika mahubiri yake amejikita zaidi kuonesha mshangao na mashaka waliyokuwa nayo watu katika maisha na utume wa Kristo Yesu, kama alama ya kuanguka na kusimama kwa wengi. Habari Njema ya Wokovu inakwenda sanjari na dhuluma pamoja na Msalaba. Fumbo la Msalaba ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Alhamisi kuu, Mama Kanisa ameadhimisha Kumbukumbu ya kuwekwa kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu ya Upadre na huduma ya upendo kwa watu wa Mungu inayopaswa kutolewa kwa unyenyekevu, ari na moyo mkuu, kama alivyofanya Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi kuu, tarehe 1 Aprili 2021 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican pamoja na kubariki Mafuta Matakatifu. Haya ni Mafuta ya Wakatekumeni, Mafuta ya Wagonjwa na pamoja na Krisma ya Wokovu; mafuta yanayotumika kwa ajili ya kuwapaka waamini wakati wanapopokea Sakramenti ya Ubatizo, Kipaimara na Daraja Takatifu. Hii ni siku ambamo wakleri wamerudia tena ahadi za utii kwa Askofu mahalia. Alhamisi Kuu, Mama Kanisa ameadhimisha kumbukumbu endelevu ya siku ile Kristo Yesu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, kielelezo makini cha ushuhuda wa upendo wake, unaobubujika kutoka katika Ekaristi Takatifu. Hii ni kumbukumbu ya uwepo wake kati pamoja na waja wake. Kristo Yesu ndiye Mwanakondoo wa Mungu anayeichukua dhambi ya walimwengu. Kwa Mwili na Damu yake Azizi amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kristo Yesu aliteswa na kufa Msalabani kwa sababu ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu na sadaka yake Msalabani imekuwa ni chombo cha ukombozi wa binadamu wote!

Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Kubariki Mafuta Matakatifu katika mahubiri yake amejikita zaidi kuonesha mshangao na mashaka waliyokuwa nayo watu katika maisha na utume wa Kristo Yesu, kama alama ya kuanguka na kusimama kwa wengi. Habari Njema ya Wokovu inakwenda sanjari na dhuluma pamoja na Msalaba. Fumbo la Msalaba ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya watu. Huu ni Msalaba unao okoa. Maandiko Matakatifu yanaonesha jinsi watu walivyompokea Kristo Yesu katika maisha na utume wake alipoanza kuhubiri katika Galilaya. Wengi walistaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake. Lakini baadhi yao wakambeza wakisema, ni mwana wa Yusufu. Utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu ni chanda na pete cha uwepo wa Msalaba katika maisha ya Wakleri. Huyu siye Mwana wa Yusufu ni tungo tata inayoweza kuonesha furaha ya ndani, lakini kwa upande mwingine inaonesha dharau! Anadhani kwamba, Yeye ni nani? Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwenye Sikukuu ya Pentekoste, Mitume walipojazwa Roho Mtakatifu wakaanza kuzungumza kwa lugha nyingine kama Roho alivyowajalia kutamka. Wengine wakawadhihaki wakisema “wamelewa kwa mvinyo mpya”. Rej. Lk 2: 1-11. Haya ni maneno yaliyokuwa na “ukakasi ndani yake”, mwanzo wa dhuluma dhidi ya Kristo Yesu wakimtaka afanye miujiza kama alivyotenda Kapernaumu.

“Jiokoe” mwenyewe ni maneno yatakayomwandama Kristo Yesu hadi pale Msalabani, wakimtaka ajiokoe mwenyewe na kuwaokoa wale wanyang’anyi waliokuwa wametundikwa wote Msalabani. Kwa hakika hakuna nabii anayekubaliwa katika nchi yake mwenyewe. Ni katika muktadha huu, Kristo Yesu anakuwa ni ishara ya kusimama na kuanguka kwa wengi “semeion antilegomenon”. Rej. Lk 2: 34. Hiki ni kielelezo cha mapambano ya maisha ya kiroho kama ilivyo kwenye mfano wa ngano safi na magugu. Watu waliona na kushuhudia matendo ya huruma, lakini bado walikuwa na shingo ngumu. Ndiyo maana katika Heri za Mlimani anasema “Ole wenu”. Hapa ni mahali pa kufanya mang’amuzi na kuchua uamuzi wa dhati kabisa. Wakashikwa na hasira na kutaka kumuua, lakini Kristo Yesu akapita katikati yao na kwenda zake. Saa ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema inakwenda sanjari na dhuluma pamoja na Msalaba. Neno la Mungu linawaangazia waamini kuona ukweli na kuupokea au kuukataa. Mawazo haya anasema Baba Mtakatifu Francisko kwamba, ni ukweli ulio wazi katika Maandiko Matakatifu. Kama ilivyokuwa kwa mkulima aliyepanda mbegu bora, lakini usiku akaja adui yake akapandikiza magugu. Ndivyo ilivyokuwa kwa Baba mwenye huruma pale Mwana mpotevu aliporejea nyumbani akiwa mzima, lakini kaka mkubwa akasusia sherehe kwa shutuma ya maneno mazito mazito!

Bila shaka waamini bado wanamkumbuka yule tajiri mwenye shamba la Mizabibu aliyewapatia wafanyakazi wake wote ujira sawa, licha ya kwamba, kuna baadhi yao walifanya kazi kwa masaa machache tu! Ukaribu, huruma na upendo wa Kristo Yesu, ulimwezesha kuwaokoa akina: Zakayo mtoza ushuru; Mwinjili Mathayo pamoja na yule Mwanamke Msamaria. Lakini bado aliendelea kushutumiwa na wale waliokuwa wanajihesabia haki. Kumbe, utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu daima unakwenda sanjari na Fumbo la Msalaba katika maisha. Hata katika maisha ya Mapadre ambao, Alhamisi Kuu wamekumbuka ile Siku ambayo Kristo Yesu alipoweka Sakramenti ya Daraja Takatifu, wanaendelea kukutana na Fumbo la Msalaba katika maisha yao. Kuna wakati ambapo hawaeleweki vyema mbele ya waamini wao; wengine wanakataliwa, wananyanyaswa na kudhulumiwa. Kamwe kwa Mapadre hili lisiwe ni jambo la kushangaza sana kwani Kristo Yesu alianza kubeba Msalaba wake tangu siku ile alipotumgwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, tumboni mwa Bikira Maria! Mahangaiko ya Mtakatifu Yosefu mtu wa haki; dhuluma na mauaji yaliyoletwa Mfalme Herode. Hata leo hii, kuna watu wanaokimbia familia na nchi zao ili kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi ugenini. Fumbo la Msalaba ni sehemu ya maisha ya mwamini na wala halitegemei hali na mazingira ya mtu. Kristo Yesu awe ni mfano bora wakuigwa katika mchakato wa kukumbatia Msalaba katika maisha.

Kristo Yesu alifanya hivi wakati wa Karamu ya mwisho; aliposalitiwa na Yuda Iskarioti, alipotelekezwa na Mitume wake waliokuwa wanaohofia kifo. Alikamatwa na kuhukumiwa kinyume cha sheria; akatemewa mate na kupigwa mijeledi, ushuhuda wa Saa yake ya neema na mateso; muda wa kukumbatia Msalaba unaookoa, kielelezo halisi cha maisha na wala hapo hakuna mjadala. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwa kusema kwamba, Msalaba ni sehemu ya vinasaba vya maisha, udhaifu na mapungufu ya binadamu. Kuna baadhi ya watu wanataka kugeuza Msalaba kuwa ni sehemu ya kashfa ya maisha ya Kipadre kwa kubeza huduma na sadaka ya upendo inayotolewa kwa ajili ya wengine. Na katika muktadha huu, sumu kali ya Shetani, Ibilisi inaendelea kusema, “Jiokoe mwenyewe”. Lakini, mwisho wa siku, utukufu wa Mungu utang’aa! Huu ni mwaliko kwa wakleri kumwomba Mwenyezi Mungu neema na baraka ya kuweza kupokea Msalaba wakati wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa kutambua kwamba, Msalaba unaokoa. Damu Azizi ya Kristo iliyomwagika pale Msalabani ni ushindi wa kishindo dhidi ya Shetani, Ibilisi.

Kristo Yesu awe ni ngome yao katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Hakuna sababu ya kuogopa kashfa ya Msalaba, bali iwe ni kichocheo cha kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu kwa maskini. Yesu hakuona kuwa ni kashfa kwa kuwaganga na kuwatibu wagonjwa; kwa kuwafungulia wafungwa na wote waliosetwa na kinzani za kisheria, kimaadili na hata pengine Kikanisa, pale alipokuwa anajaribu kutenda mema. Yesu alipania kuwaokoa watu katika shida na mahangaiko yao na akasimamia ukweli huu. Leo hii, magazeti yangelimpamba kwa kashfa kubwa kwenye kurasa zao za mbele! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wakleri kujichotea nguvu ya Msalaba katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na wala wasiogope kashfa ya Msalaba kwani hii ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wao. Watangaze Fumbo la Msalaba wa Kristo kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa kuvumilia dhuluma na mateso yanayotokana na Injili ya Kristo. Wasijihubiri wao wenyewe bali Kristo Yesu kwa kuwa ni Bwana na apewe kipaumbele cha kwanza, kwa sababu wao ni watumishi kwa ajili ya Kristo Yesu.

Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko amewashikirisha waamini ushuhuda wa neema na baraka ambazo Mwenyezi Mungu alimkirimia wakati fulani, alipokuwa akitembea kwenye giza na bonde la mashaka. Lakini Mwenyezi Mungu anatoa baraka na neema hizi kadiri ya wema, huruma na upendo wake na wala si kadiri ya matakwa ya mtu binafsi. Hii inatokana na ukweli kwamba, Msalaba ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Mapadre. Msalaba ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, hadi tone la mwisho la maisha!

Papa Alhamisi Kuu
01 April 2021, 16:54