Tafuta

Sala ya Malkia wa Mbingu Sala ya Malkia wa Mbingu 

Papa:Ukristo si mafundisho tu ni kuwa na uhusiano halisi na Bwana Mfufuka!

Sura ya kiinjili ya Dominika ya tatu ya Pasaka,ina vitenzi vitatu ambavyo vinatafakarisha katika maisha yetu binafsi na jumuiya;ni kutazama,kugusa na kula.Ni matendo ambayo yanaweza kutoa fursa ya mkutano wa kweli na Yesu aliye hai.Ni katika tafakari ya Papa kwa waamini na mahujaji waliofika katika kiwanja cha Mtakatifu Petro kuzalia sala ya Malkia wa Mbingu ambapo amehimiza ukaribu na Bwana ili kuweza kukaribia wengine.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa tafakari ya Neno la Mungu kabla ya sala ya Malkia wa Mbingu, kwa waamini na mahujaji hatimaye katika uwaja wa Mtakatifu Petro, tarehe, 18 Aprili 2021, kwa kungozwa na Injili ya Dominika ya tatu ya Pasaka (Luka 24,35-48), ameanza kusema: “Katika Dominika ya tatu ya Pasaka, tunarudi Yerusalemu, katika karamu kuu, kama tunavyo ongozwa na mitume wawili wa Emau, ambao walikuwa wamesikiliza kwa shauku kubwa maneno ya Yesu wakiwa njiani na baadaye wakamtambua “wakati wa kuumega mkate!( Lk 24, 35). Na sasa katika karamu kuu, Kristo Mfufuka alisimama  katikati ya kikundi cha wafuasi na kuwasalimu akisema “Amani iwe kwenu”(Lk 24, 36). Lakini wao walishutuka, wakaogopa sana wakidhani ya kwamba wanaona kuvuli cha roho, Injili inasema. Kwa maana hiyo Yesu aliwaonesha majeraha yake katika mwili wake na kusema “tazameni mikono yangu na miguu yangu, madonda yangu. “Nishikeni, shikeni. Na ili kuwaaminisha wao aliwaomba chakula na kula mbele yao wakiwa na  mitazamo na  kustaabu” (Lk 24, 41- 42).

Mshangao unakwenda zaidi ya shauku

Papa Francisko amesema hata hivyo “Kuna maelezo hapa, kwa namna ya pekee katika ufafanuzi huu wa Injili ambayo inasema kwamba Mitume kwa furaha kubwa waliyokuwa nayo bado hawakuamini”. Hiyo ndiyo furaha waliyokuwa nayo hata hawakuweza kuamini kama ni kweli. Na maelezo ya pili: walishangaa, na kustaajabu; kushangaa kwa sababu ya kukutana na Mungu,  siku zote huongoza kwenye mshangao daima  na huenda zaidi ya shauku, zaidi ya furaha, ni uzoefu mwingine. Na hawa walifurahi, lakini ni furaha iliyowafanya wafikiri kwamba hapana, hii haiwezekani kuwa kweli! ... Ni mshangao wa uwepo wa Mungu” …Papa Francisko kwa kusistiza zaidi ameongeza “ Msisahau hali hii ya akili, ambayo ni nzuri sana”. Sura hii ya kiinjili Papa Francisko ameendelea kufafanua, ina tabia ya maneno matatu ya dhati, ambayo yanatafakarisha kwa namna fulani maisha yetu binafsi na jumuiya: ni kutazama, kugusa na kula. Ni matendo ambayo yanaweza kutoa fursa ya mkutano wa kweli na Yesu aliye hai.

Neno la kwanza ni Kutazama:tuwe na karibu na kuacha sintofahamu

Papa Francisko akiendelea na tafakari hii amesema “Tazameni mikono yangu na miguu yangu”, anasema Yesu. Kutazama siyo tu kuona, ni zaidi yake, hupelekea hata umakini na pia utashi. Kwa maana hiyo ni moja ya maneno ya upendo. Mama na baba wanapomtazama mtoto wao, wapendwa hao utazamana nyuso zao pamoja; aidha, daktari mzuri, umwangalia mgonjwa kwa umakini… Kutazama ni hatua mojawapo dhidi ya kutojali, dhidi ya kishawishi cha kugeuza sehemu nyingine mbele ya matatizo na mateso ya wengine. Kuangalia. Je! Mimi namwona au ninamtazama Yesu?

Neno la pili kugusa: mfano wa kuwa msamaria

Neno la pili ni kugusa. Yesu akiwaalika wafuasi wake kumshika, shika, ili kuweza kutambua kuwa siyo roho, ‘nishikeni’, anawaelekeza wao pia  sisi kuwa uhusiano na Yesu na ndugu zetu hauwezi kubaki  na umbali, hakuna ukristo wa umbali, hakuna ukristo tu bali juu ya mpango wa mtazamo. Upendo unaomba kutazama na kuomba hata ukaribu, unaomba kugusa, kushirikishana maisha. Msamaria mwema hakubaki kutazama tu yule mtu aliyemkuta njiani nusu mfu. Yeye alisimama na akainama, alimfunga majeraha, alimbeba juu ya farasi wake na kumpeleka kwenye nyumba ya wageni. Na hivyo ndivyo Yesu. Kumpenda maana yake ni kuingia katika muungano hai, wa kweli  wa maisha na  muungano na yeye.  

Neno la tatu ni kula:Kuwa Mkristo si mafundisho tu ni uhusiano wa kuishi na Bwana

Papa Francisko amejikita kueleza  neno la tatu, ambalo linahusu kula katika Injili ya siku na ambalo amesema kwamba linaelezea wema wa ubinadamu wetu, katika hali yake ya asili ya mahitaji yake yaani mahitaji ya kula ili kuweza kuishi. Lakini tendo la kula, hasa tunapofanya kwa pamoja, ndani ya familia au kati ya marafiki, linakuwa pia kielelezo cha upendo, kielelezo cha muungano na sikukuu.  Papa Francisko amebainisha kwamba “ni mara ngapi Injili zimetuwakilisha Yesu ambaye anaishi katika hali hii ya sherehe ya pamoja ya kula!  Hata akiwa Mfufuka na wanafunzi wake. Kwa hali hiyo, Chakula cha Ekaristi kimegeuka kuwa ishara kuu ya jumuiya ya kikristo. Kula pamoja Mwili wa Kristo, ndiyo kiini cha maisha ya kikristo. Kwa kuhitimisha, Papa Francisko amesema sura hii ya Kiinjili inatuambia kuwa Yesu sio kivuli cha roho, bali ni Mtu anayeishi; kwamba wakati Yesu anatukaribia yeye hutujaza furaha, hadi kufikia hatua ya kutoamini, na anatuacha tukishangaa, na ni mshangao huo ambao kwa uwepo tu  wa Mungu anautoa, kwa sababu Yesu ni Mtu aliye hai. Kuwa Mkristo awali ya yote sio  mafundisho au maadili bora, ni uhusiano wa kuishi naye, na Bwana Mfufuka: tunamtazama, tunamgusa, tunalishwa na tukibadilishwa na upendo wake, tutaangalia, tutagusa na kuwalisha wengine kama kaka na dada. Bikira Maria atusaidie kuishi uzoefu huu wa neema”.

18 April 2021, 13:52

Sala ya Malkia wa Mbingu ni nini?
 

Utenzi wa Malkia wa Mbingu ni kati ya tenzi nne za Bikira Maria (nyingine ni:Tunakimbilia Ulinzi wako,  Salam Malkia wa Mbingu, Salam Malkia). Kunako mwaka 1742, Papa Benedikto XIV alipoandika kwamba, waamini wasali Sala ya Malkia wa Mbingu wakiwa wamesimama, kama alama ya ushindi dhidi ya kifo, wakati wa Kipindi cha Pasaka, yaani kuanzia Domenika ya Ufufuko wa Bwana hadi Sherehe ya Pentekoste. Hii ni Sala ambayo husaliwa mara tatu kwa siku kama ilivyo pia Sala ya Malaika wa Bwana: Asubuhi, Mchana na Jioni ili kuweka wakfu Siku kwa Mwenyezi Mungu na Bikira Maria.

Utenzi huu kadiri ya Mapokeo ulianza kutumika kunako karne ya VI au Karne X, lakini kuenea kwake kunaanza kujitokeza katika nyaraka mbali mbali kati kati ya Karne ya XIII, ilipoingizwa kwenye Kitabu cha Sala za Kanisa cha Wafranciskani. Hii ni Sala inayoundwa na maneno mafupi manne yanayohitimishwa na Alleluiya na sala ya waamini wanaomwelekea Bikira Maria, Malkia wa mbingu, ili kufurahia pamoja naye kuhusu Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu.

Papa Francisko tarehe 6 Aprili 2015 wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, siku moja baada ya Sherehe ya Pasaka, aliwashauri waamini kuwa na moyo wa furaha wanaposali sala hii. “Tunamwendea Bikira Maria, tukimwomba afurahi, kwa sababu yule Mwanaye mpendwa aliyekuwa amemchukua mimba amefufuka kweli kweli kama alivyosema; tunajiaminisha kwa sala na maombezi ya Bikira Maria. Kimsingi furaha yetu ni mwangi wa furaha ya Bikira Maria kwani ndiye aliyetunza na anaendelea kutunza matukio mbali mbali ya maisha ya Yesu. “Tusali sala hii kwa furaha ya kuwa waana wa Mungu ambao wanafurahi kwa sababu Mama yao anafurahi”

 

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >