Tafuta

Vatican News
Tarehe 13 Aprili 2021 Mama Kanisa anaadhimisha Kumbukizi la Miaka 35 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Sinagogi la Wayahudi mjini Roma, Tukio la kihistoria. Tarehe 13 Aprili 2021 Mama Kanisa anaadhimisha Kumbukizi la Miaka 35 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Sinagogi la Wayahudi mjini Roma, Tukio la kihistoria. 

Kumbukizi Miaka 35: Yohane Paulo II Kutembelea Sinagogi la Roma

Mama Kanisa anaadhimisha kumbukumbu ya Miaka 35 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Sinagogi la Wayahudi mjini Roma. Alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na viongozi na waamini wa dini ya Kiyahudi mjini Roma: 13 Aprili 1986. Alikazia: Ushuhuda; Urithi wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican; Ushirikiano, mahusiano na mafungamano kati ya waamini wa dini hizi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mama Kanisa katika maisha na utume wake, ataendelea kujizatiti katika mchakato wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbalimbali duniani, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, maridhiano, ushirikiano na udugu wa kibinadamu. Mashambulizi pamoja na vitendo vya kigaidi, kamwe visiwe ni kikwazo cha majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbalimbali. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukazia majadiliano ya matumaini kati ya waamini wa dini mbali mbali ili kweli dini ziweze kuwa ni kikolezo cha amani, upendo, maridhiano na ujenzi wa udugu wa kibinadamu unatoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu! Adui mkubwa wa mchakato wa majadiliano ya kidini ni: imani na misimamo mikali ya kidini, woga na wasiwasi usiokuwa na msingi pamoja na maamuzi mbele. Haya ni mambo yanayochangia kiasi kwamba, waamini wa dini mbalimbali wanashindwa kufahamiana na hatimaye kuishi kwa amani, umoja na udugu wa kibinadamu kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kiasi kwamba, tofauti zao msingi ni amana na utajiri unaopaswa kudumishwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, yaliweka msingi wa mahusiano kati ya Wakatoliki na Wayahudi, katika harakati za majadiliano ya kidini, udugu wa kibinadamu na urafiki, hija ambayo imeendelea kuimarika hasa baada ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Ni katika muktadha huu, Mama Kanisa anaadhimisha kumbukumbu ya Miaka 35 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Sinagogi la Wayahudi mjini Roma. Alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na viongozi na waamini wa dini ya Kiyahudi mjini Roma, tarehe 13 Aprili 1986. Katika hotuba hiyo, alikazia umuhimu wa ushuhuda katika uhalisia wa maisha. Urithi wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican; Ushirikiano, mahusiano na mafungamano kati ya Wakristo na Wayahudi na changamoto wanazopaswa kwa pamoja kuzivalia njuga mjini Roma. Mtakatifu Yohane alitumia fursa hii, kuwashukuru viongozi na waamini wa dini ya Kiyahudi mjini Roma. Viongozi hawa waliwahi kukutana na kuzungumza na Mtakatifu Paulo VI, Yohane wa XXIII pamoja na Papa Pio XII.

Ushuhuda ambao umeacha chapa ya kudumu ni pale ambapo Rabbi Elio Toaff, Mkuu wa Sinagogi la Wayahudi wa Roma, akiwa ameambatana na waamini wa dini hii, walipokwenda kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican katika mkesha wa kifo cha Mtakatifu Yohane XXIII, ili kusali na kumwombea Papa Yohane XXIII kama walivyofanya waamini wengine. Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yameweka msingi thabiti wa majadiliano ya kidini. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika tamko lao kuhusu majadiliano ya kidini kwa watu wa nyakati hizi: “Nostra Aetate” wanakazia pamoja na mambo mengine dhamana ya Kanisa katika kuhamasisha umoja na upendo kati ya watu wa mataifa; kwa ajili ya mafao ya wengi, ili kusimama kidete kutangaza na kushuhudia pamoja utu na heshima ya binadamu. Kanisa Katoliki linatambua mambo ya kweli na matakatifu katika dini mbalimbali, lina heshimu na kuthamini namna yao ya kutenda na kuishi; sheria na mafundisho yao.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakaza kusema, Kanisa litaendelea kutangaza kwamba Yesu Kristo ni njia, ukweli na uzima na ambaye ndani mwake mwanadamu anapata utimilifu wa maisha ya utauwa na upatanisho kati yake na Mwenyezi Mungu. Mama Kanisa anawahamasisha watoto wake kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini, ili kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; mafao ya wengi, haki, amani na mshikamano wa kimataifa. Nyanyaso, dhuluma na mauaji ya kimbari ni kinyume kabisa cha Amri na upendo kwa Mungu na jirani. Tume ya Kipapa ya mahusiano na Wayahudi imekuwa ikiratibu mahusiano haya kwa kuzingatia Amri za Mungu. Mwaliko kwa waamini ni kusimama kidete kulinda uhai wa binadamu tangu pale anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika. Utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; ni mambo yanayopaswa kushughulikiwa na waamini wa dini hizi mbili.

Mtakatifu Yohane Paulo II alikazia umuhimu wa waamini kuwa ni mashuhuda wa maadili na utu wema. Washikamane kukabiliana na matatizo na changamoto zinazowakabili wenyeji wa mji wa Roma na wale wote wanaokimbilia usalama na hifadhi ya maisha yao. Mtakatifu Paulo VI, tarehe 28 Oktoba 1965 wakati akifunga maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican alikaza kusema, Mtaguso ni kielelezo cha Kanisa linalosali, Kanisa linalojadiliana, Kanisa linalokua na Kanisa linaloendelea kujijenga, ili kukoleza mchakato wa majadiliano ya upendo na walimwengu. Waamini wa dini mbali mbali wanahamasishwa kusimama kidete ili kujisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo kwa jirani zao; kulinda na kudumisha haki, amani, upendo na mshikamano; sanjari na kukuza uhuru wa kidini. Elimu ya dini na malezi, ni muhimu sana katika kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili.

Kwa upande wake, Rabbi Professa Elio Toaff, Mkuu wa Sinagogi la Wayahudi wa Roma, aliwapongeza Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwa mafundisho yake kuhusu majadiliano ya kidini. Aliwakumbuka na kuwaombea Wayahudi walioyamimina maisha yao, kama sehemu ya kulitakatifuza jina la Mungu. Imani na Amri zake zimeendelea kutamalaki licha ya nyanyaso na madhulumu dhidi ya Wayahudi. Sasa ni wakati wa kuhakikisha kwamba, kanuni maadili na utu wema, haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi yanapewa kipaumbele cha kwanza. Watu wote watambue kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wote wanaitwa kuwa watakatifu na wakamilifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu. Ni wakati kwa waamini wote kujizatiti katika kukuza na kudumisha uhuru wa kweli; utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni wakati wa kuondokana na mifumo mbalimbali ya kibaguzi, kwa kusimamia uhai wa binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo pamoja na uhuru wa kidini na kidhamiri sanjari na kukuza mahusiano na mafungamano miongoni mwa waamini wa dini mbalimbali.

Yohane Paulo II
13 April 2021, 15:16