Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko ametuma salam za rambirambi kwa watu wa Mungu nchini Australia kutokana na kifo cha Kardinali Edward Idris Cassidy, Rais Mstaafu wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo. Baba Mtakatifu Francisko ametuma salam za rambirambi kwa watu wa Mungu nchini Australia kutokana na kifo cha Kardinali Edward Idris Cassidy, Rais Mstaafu wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo.  (Vatican Media)

Kardinali Edward Idris Cassidy: 5 Julai 1924 - 10 Aprili 2021! Umoja!

Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake za rambirambi zilizotumwa kwa Askofu mkuu Adolfo Tito Yllana, Balozi wa Vatican nchini Australia, anasema, amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa Kardinali Edward Idris Cassidy na kwamba, anapenda kutoa salam zake za rambirambi kwa watu wote walioguswa kwa msiba huu mzito. Mazishi yake ni tarehe 19 Aprili 2021.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Askofu mkuu Adolfo Tito Yllana, Balozi wa Vatican nchini Australia, anatarajiwa, Jumatatu tarehe 19 Aprili 2021 kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mazishi ya Kardinali Edward Idris Cassidy, Rais mstaafu wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo aliyefariki dunia hapo tarehe 10 Aprili 2021 huko New Castle, Australia. Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake za rambirambi zilizotumwa kwa Askofu mkuu Adolfo Tito Yllana, Balozi wa Vatican nchini Australia, anasema, amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa Kardinali Edward Idris Cassidy na kwamba, anapenda kutoa salam zake za rambirambi kwa watu wote walioguswa kwa msiba huu mzito. Baba Mtakatifu anamkumbuka kwa moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu aliyemwezesha Mtumishi wake mwaminifu, kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya Vatican na Kanisa katika ujumla wake. Ni kiongozi aliyejitosa kutangaza na kushuhudia Injili katika muktadha wa majadiliano ya kiekumene, ili kuhamasisha umoja wa Wakristo.

Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii, kumwombea Hayati Kardinali Edward Idris Cassidy, kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma, upendo na msamaha, ili sasa aweze kuipumzisha roho yake katika usingizi wa amani, huku akiwa na tumaini la ufufuko na maisha ya uzima wa milele. Baba Mtakatifu anatoa baraka zake za kitume kwa wale wote wanaoomboleza na wale watakaoshiriki katika mazishi ya Kardinali Edward Idris Cassidy. Wajaliwe pia faraja na amani ya Kristo Mfufuka! Itakumbukwa kwamba, Hayati Kardinali Edward Idris Cassidy alizaliwa tarehe 5 Julai 1924 huko Sydney, Australia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 23 Julai 1949 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kati ya mwaka 1952 hadi mwaka 1955 alitumwa na Jimbo Katoliki la Wagga Wagga kujiendeleza zaidi na hapo akahitimu na kujipatia Shahada ya Uzamivu kuhusu Sheria za Kanisa kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran. Mwaka 1953 alijiunga na Chuo Cha Diplomasia ya Kanisa na baada ya mafunzo yake, akateuliwa kuwa ni sehemu ya wanadiplomasia wa Kanisa.

Kwa nyakati mbalimbali alifanikiwa kutekeleza utume wake nchini India kati ya Mwaka 1955 hadi mwaka 1962. Baadaye alitumwa Ireland, El Salvador na Argentina. Mtakatifu Paulo VI akamteuwa kuwa Askofu mkuu tarehe 27 Oktoba 1970 na hatimaye, akamteuwa kuwa ni Balozi wa Vatican, Taiwan, China. Tarehe 15 Novemba 1970 akawekwa wakfu kuwa Askofu mkuu na kutumwa Bangaladesh kama Balozi wa Vatican na Mwakilishi wa Kitume nchini Burma. Baadaye alitumwa kuwalisha Vatican nchiniAfrika ya Kusini, Lesotho na Netherland. Tarehe 23 Machi 1988 aliteuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Katibu msaidizi wa Vatican katika masuala ya kumla, utume aliouendeleza hadi tarehe 12 Desemba 1989, alipoteuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa ni Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo hadi tarehe 3 Machi 2001 alipong’atuka kutoka madarakani na kurejea nchini Australia kwa mapumziko. Aliteuliwa na kutangazwa kuwa Kardinali na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 28 Juni 1991. Baada ya utume wote huu ndani ya Kanisa, tarehe 10 Aprili 2021 akafariki dunia, tayari kuanza safari ya kuonana na Hakimu mwenye haki na huruma, Kristo Yesu, huko mbinguni!

Kardinali Cassidy

 

16 April 2021, 15:28