Tafuta

Vatican News
Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema, Siku ya 58 ya Kuombea Miito Mitakatifu Ndani ya Kanisa: Yaliyojiri sehemu mbalimbali za dunia kwa muhtasari! Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema, Siku ya 58 ya Kuombea Miito Mitakatifu Ndani ya Kanisa: Yaliyojiri sehemu mbalimbali za dunia kwa muhtasari!  (Vatican Media)

Siku ya 58 ya Kuombea Miito Ulimwenguni: Yaliyojiri Kanisani!

Maadhimisho ya Siku ya 58 ya Kuombea Miito Ulimwenguni kwa Mwaka 2021 yamenogeshwa na kauli mbiu "Mtakatifu Yosefy Ndoto ya Miito" Mkazo zaidi ni kuhusu: Ndoto, Huduma na Uamianifu. Padre Livinus Nnamani amehudumu kama Padre kwa siku 31 na kufariki dunia! Maaskofu Katoliki Ureno waadhimisha kwa Juma zima la Kuombea Miito. Siku ya 38 ya Vijana Ureno!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 58 ya Kuombea Miito Ulimwenguni, iliyoadhimishwa Jumapili, tarehe 25 Aprili 2021, umenogeshwa na kauli mbiu “Mtakatifu Yosefu Ndoto ya Wito”. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, amekazia umuhimu wa: Ndoto, huduma na uaminifu; mambo msingi katika kukuza na kudumisha miito mbalimbali ndani ya Kanisa. Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Miito Ulimwenguni yamekwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu uliozinduliwa rasmi hapo tarehe 8 Desemba 2020 na yanatarajiwa kufungwa kwa kudema hapo tarehe 8 Desemba 2021. Yote haya yamo kwenye Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu. Baba Mtakatifu Francisko, katika maadhimisho ya Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji mwema, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ametoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi 9 kutoka Jimbo kuu la Roma.

Hawa ni Mapadre wa Jimbo, ambao wako tayari sasa kuendeleza utume wa Kristo Yesu katika: Kufundisha, Kuongoza na Kuwatakatifuza watu wa Mungu. Hii ni huduma kwa ajili ya watu wa Mungu. Kwa sasa wanao wajibu wa kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu ambalo wao wenyewe wanapaswa kwanza kulisoma, kulitafakari na kulimwisha katika uhalisia wa maisha yao. Wawe ni mashuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, tayari kuwafundisha watu wa Mungu kwa furaha inayobubujika kutoka katika ushuhuda wa maisha yao. Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa yawawezeshe kushiriki katika Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu, tayari kupyaisha maisha ya waamini kwa njia ya Fumbo la Pasaka. Mapadre wapya watambue kwamba, wameteuliwa kutoka miongoni mwa watu wa Mungu kwa ajili ya mambo ya Mungu, dhamana wanayopaswa kuitekeleza kwa furaha na upendo, daima wakilenga kumtukuza Mwenyezi Mungu katika maisha yao, ili mwanadamu aweze kutakatifuzwa. Katika kutekeleza utume wao, daima wajitahidi kuwa wameungana na Askofu wao mahalia, wajitahidi pia kuwaunganisha waamini ili waweze kuwa ni sehemu ya familia moja, inayofunga safari ya kwenda kwa Baba wa mbinguni kwa njia ya Kristo katika Roho Mtakatifu.

Mapadre wapya na wale wa zamani, wajitahidi kufuata mfano wa Kristo Yesu Mchungaji mwema, aliyekuja hapa duniani si kwa ajili ya kutumikiwa bali kutumikia na kutoa uhai wake, ili uwe ni fidia kwa wengi. Waoneshe ukaribu wa Mungu kwa watu wake, wawe na huruma, wapole na wanyenyekevu wa moyo! Wawe ni watu wa sala, walishiriki na kuadhimisha vyema Sakramenti za Kanisa na kwa namna ya pekee waadhimishe Ibada ya Misa Takatifu kwa uchaji na unyofu wa moyo! Mapadre wawe karibu na Mungu, Askofu mahalia, kati yao wenyewe kwa kujenga na kudumisha urika wa Mapadre na kamwe wasisahau kuwa karibu na watu wa Mungu wanaowahudumia na kamwe wasiwe ni wafanyabiashara! Baba Mtakatifu amekazia sifa kuu tatu za mchungaji wema: yule anayetoa uhai wake kwa ajili ya kondoo; anawajua na kuwapenda kondoo wake.

Maadhimisho ya Siku ya 58 ya Kuombea Miito Ulimwenguni yamewagusa watu wengi kutokana na kifo cha Padre Livinus Esomchi Nnamani wa Shirika la Mama wa Mungu, “Mater Dei” aliyefariki dunia tarehe 23 Aprili 2021, akiwa na umri wa miaka 31 tu tangu alipozaliwa. Katika hali ya hatari ya kifo iliyokuwa inamzunguka, alimwomba Baba Mtakatifu Francisko kibali cha Kupewa Daraja Takatifu ya Upadre, tarehe 31 Machi 2021 na Baba Mtakatifu akaridhia ombi lake na kupatiwa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 01 Aprili 2021kwa mikono ya Askofu Msaidizi Daniele Libanor akiwa Hospitalini. Padre Livinus Esomchi Nnamani ameweza kuupokea wito na zawadi ya Daraja Takatifu ya Upadre kwa muda wa siku 23 tu. Tarehe 26 Aprili 2021 anaagwa na familia ya Mungu Parokia ya San Giovanni Leonardi, Jimbo la Roma, tayari kurejeshwa nchini Nigeria kwa maziko! Usiogope! Anasema Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya mitandao ya jamii kwamba, ni maneno ya Kristo Yesu yanayowambata na kuwaandama wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao kwamba, Mwenyezi Mungu atakuwa nao daima katika maisha na uaminifu wao kila siku ya maisha!

Ikumbukwe kwamba, katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, kuna Mapadre na watawa wengi wamepoteza maisha yao kutokana na kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Waamini wanapoombea Miito Mitakatifu, wawakumbuke hata hawa Mapadre na watawa waliotangulia mbele ya haki, wakiwa na imani na tumaini la ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Ni katika muktadha huu, Padre Bonaventure Luchidio, Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari, PMS, nchini Kenya anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili ya miito mitakatifu pamoja na kuchangia kwa hali na mali, ili kuendeleza miradi ya miito nchini Kenya, kama ushuhuda wa ukarimu kwa ajili ya kuenzi miito mitakatifu. Mchango huu ni muhimu kwa ajili ya malezi na majiundo ya Majandokasisi, wanaojiandaa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu.

Kwa upande wake, Padre Stefano Kaombe, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Francisko Xsaveri, Chang’ombe, Jimbo kuu la Dar es Salaam katika mahubiri yake, amekazia nafasi na dhamana ya familia katika mchakato wa kuchipua, kulea na kukuza miito mbalimbali ndani ya Kanisa. Amesema, umefika wakati wa kubadili “dhana ya Padre kuwa ni kitega uchumi na mradi wa familia” na kujielekeza zaidi kuhusu Daraja Takatifu ya Upadre kama wito na zawadi kutoka kwa Mungu. Wazazi na walezi watambue kwamba, watoto ni zawadi ya Mungu, wawe tayari pia kumtolea Mungu zawadi ya watoto wao kwa ajili ya huduma kwa Kanisa kama Mapadre na Watawa na kamwe wasiwe ni kikwazo kwa watoto wao. Mapadre pia wawasaidie wazazi, ndugu na jamaa kutambua kwamba, Upadre ni wito na zawadi wanayoiwekeza katika imani na kamwe si kitega uchumi. Vinginevyo watawachanganya Mapadre badala ya kudemka katika huduma, watadumaa na kusinyaa kwa msongo wa mawazo, mwanzo wa kukata tamaa na kuonja machungu ya Upadre na Utawa!

Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno kuanzia tarehe 18 hadi 25 Aprili 2021 limeadhimisha Juma la Kuombea Miito Mitakatifu kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Kuota Ndoto ya Mungu”. Lengo la maadhimisho haya ni kujenga utamaduni wa kulea na kukuza miito mitakatifu ndani ya Kanisa, kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi. Imekuwa ni fursa kwa Maaskofu kutoa mifano hai kwa ajili ya vijana na familia na ndoa, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ana mpango kwa kila kiumbe chake. Kusali kwa ajili ya kuombea miito ni dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa unyenyekevu, ari na moyo mkuu! Jimbo kuu la Lisbon, Ureno limepewa dhamana ya kuandaa Maadhimisho ya Siku ya 38 ya Vijana Ulimwenguni kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39 na yataadhimishwa mwezi Agosti mwaka 2023. Hapa pamekuwa ni chemchemi na chimbuko la miito mitakatifu ndani ya Kanisa na kwamba, Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo, limejikuta likiwa na sura ya ujana, pasi na makunyanzi; Kanisa ambalo limewasukuma vijana kuendelea kujiaminisha kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kwa upande wake, Baraza la Maaskofu Katoliki Poland linawataka watu wa Mungu nchini humo kusali, kulea, kukuza na kuwasindikiza vijana kutekeleza ndoto katika miito yao mbalimbali, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yosefu, Msimamizi wa Kanisa la Kiulimwengu.

Siku 58 ya Miito
25 April 2021, 15:25