Tafuta

Jumapili ya Huruma ya Mungu: Zawadi za Kristo Mfufuka kwa wale walionjeshwa huruma ya Mungu: Amani, Roho Mtakatifu kwa maondoleo ya dhambi na Madonda Matakatifu chemchemi ya huruma ya Mungu. Jumapili ya Huruma ya Mungu: Zawadi za Kristo Mfufuka kwa wale walionjeshwa huruma ya Mungu: Amani, Roho Mtakatifu kwa maondoleo ya dhambi na Madonda Matakatifu chemchemi ya huruma ya Mungu. 

Jumapili ya Huruma ya Mungu: Madonda, Roho Mt. na Amani!

Baba Mtakatifu Francisko: Zawadi za Kristo Mfufuka: Amani inayowachangamotisha kutoka kifua mbele ili kushiriki kikamilifu katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Zawadi ya Pili ni Roho Mtakatifu, kwa ajili ya toba, wongofu wa ndani na maondoleo ya dhambi. Zawadi ya tatu anasema Baba Mtakatifu ni Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mama Kanisa, tarehe 11 Aprili 2021 ameadhimisha Jumapili ya Huruma ya Mungu iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2000. Mtakatifu Maria Faustina Kowalska ni kati ya watakatifu waliotangaza, wakashuhudia na hatimaye, kueneza Ibada ya huruma ya Mungu. Chemchemi ya huruma ya Mungu inafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Ibada hii inakolezwa kwa kwa njia ya Novena ya Huruma ya Mungu inayoanza Ijumaa kuu na kuhitimishwa katika maadhimisho ya Jumapili ya Huruma ya Mungu. Kuna Saa kuu la Huruma ya Mungu, mwaliko kwa waamini kujizamisha katika huruma ya Mungu, ili kuiabudu, kuitukuza na kusifu uweza mkuu wa Mungu katika kuwahurumia na kuwakomboa wadhambi. Huruma ya Mungu imeshinda haki! Waamini wanahamasishwa kukuza na kudumisha Ibada na uchaji wa Mungu wanapoadhimisha Sakramenti za Huruma ya Mungu yaani: Ekaristi Takatifu na Upatanisho, chemchemi ya utakatifu na mchakato katika uinjilishaji mpya unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Rozari ya Huruma ya Mungu ni chombo cha Ibada kinachowaunganisha waamini wote kuomba huruma ya Mungu kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu mzima. Kristo Yesu ni mwokozi Mwenye Huruma isiyokuwa na kifani. Rozari ya Huruma ya Mungu inawasaidia waamini kutekeleza dhamana na wajibu wao wa Kikuhani, waliojitwalia wakati walipobatizwa. Kwa njia hii, wanapyaishwa na kuwa ni sadaka safi inayounganishwa na Sadaka ya Kristo Yesu, Mfalme wa amani, upendo na huruma! Baba Mtakatifu Francisko, katika maadhimisho ya Jumapili ya Huruma ya Mungu, tarehe 11 Aprili 2021, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la “Santo Spirito in Sassia”, lenye Ibada ya pekee kwa huruma ya Mungu, Jimbo kuu la Roma. Katika mahubiri yake amezungumzia kuhusu zawadi kuu tatu ambazo Kristo Yesu Mfufuka anawakirimia wale ambao wameonjeshwa huruma ya Mungu katika maisha yao: Amani inayowachangamotisha kutoka kifua mbele ili kushiriki kikamilifu katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, kwa kutambua kwamba, kila mtu anayo thamani kubwa machoni pa Mungu.

Zawadi ya Pili ni Roho Mtakatifu, kwa ajili ya toba, wongofu wa ndani na maondoleo ya dhambi. Huu ni mwaliko kwa waamini kukimbilia katika kiti cha toba, ili kuonja upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao! Sakramenti ya Upatanisho, inawainua wale wote walioteleza na kuanguka dhambini. Hii ni Sakramenti ya Ufufuko. Zawadi ya tatu anasema Baba Mtakatifu ni Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu. Mtakatifu Toma, Mtume kwa kugusa Madonda Matakatifu ya Yesu, akatubu, akaongoka na kuwa Shuhuda wa Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ufunuo wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa watoto wake. Udhaifu wa kibinadamu na imani haba “kama kiatu cha raba” ikapata kuonja huruma na upendo wa Mungu unaoganga, kuponya na kuokoa.

Upendo wa Mungu ni chachu ya mwanzo na upyaisho wa ulimwengu. Hii ni changamoto kwa waamini walionjeshwa huruma na upendo wa Mungu kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao! Baba Mtakatifu Francisko katika mitandao ya kijamii, Jumapili ya Huruma ya Mungu anawakumbusha waamini kwamba, wanapaswa kujisikia daima kwamba, ni watu waliohurumiwa ili hatimaye, wao pia waweze kuwa na huruma! Hii ni fursa kwa waamini kuangalia ikiwa kweli wameendelea kujizatiti kama mashuhuda na vyombo vya Huruma ya Mungu, kielelezo makini cha imani tendaji inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili!

Chemchemi ya Huruma

 

 

12 April 2021, 14:49