Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema, Mkesha wa Pasaka ni Mama wa Mikesha yote inayoadhimishwa na Mama Kanisa katika sala na liturujia ya Kanisa, kwani anaadhimisha Fumbo la Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Papa Francisko asema, Mkesha wa Pasaka ni Mama wa Mikesha yote inayoadhimishwa na Mama Kanisa katika sala na liturujia ya Kanisa, kwani anaadhimisha Fumbo la Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu.  (Vatican Media)

Jumamosi Kuu: Mkesha wa Pasaka: Nendeni Galilaya!

Inawezekana kuanza maisha mapya yanayopata chimbuko lake kutoka kwa Mungu. Pili, Kristo Yesu amefufuka ni mzima na anaendelea kutembea bega kwa bega na waja wake. Tatu, Kristo Mfufuka anawapenda waja wake upeo. Kristo Yesu aliyeteswa, akafa, amefufuka na amewatangulia kwenda Galilaya. Huu ni mwaliko kwa wafuasi wa Kristo Yesu kwenda nao mjini Galilaya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mkesha wa Pasaka ni Mama wa mikesha yote inayoadhimishwa na Kanisa. Kwa sababu ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kilele cha ukweli wa imani ya Kanisa katika Kristo. Yesu amefufuka kutoka wafu. Kwa kifo chake ameshinda mauti, wafu amewapa uzima. Rej. KKK, 638.  Huu ni Usiku ambamo wimbo wa Aleluiya Kuu unasikika, kielelezo cha imani ya waamini wanaokutana na Kristo Mfufuka katika maisha yao. Waamini wataendelea kumshangilia Kristo Mfufuka kwa muda wa Siku 50, hadi Sherehe ya Pentekoste. Kristo Mfufuka anapenda kuwahakikishia waja wake kwamba, uzuri utashinda ubaya; maisha “yatapeta” dhidi ya utamaduni wa kifo na kwamba, Kristo Yesu ni chemchemi ya huruma, upendo na msamaha wa Mungu. Mkesha huu una: Ibada ya Kubariki Moto na Ibada ya Mwanga inayohitimishwa kwa kuimba Mbiu Kuu ya Pasaka, kutangaza sifa za Mshumaa wa Pasaka, ambaye ni Kristo Yesu mwenyewe, mwanga wa Mataifa. Liturujia ya Neno la Mungu, muhtasari wa historia ya ukombozi ambayo ina masomo 7 kutoka Agano la Kale na 2 ya Agano Jipya. Kuna Liturujia ya Ubatizo ambamo waamini wamerudia tena ahadi zao za Ubatizo pamoja na Liturujia ya Ekaristi Takatifu.

Wanawake waliokwenda kaburini walikutana na Malaika; “Naye akawaambia, Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa; amefufuka; hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka. Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia. Wakatoka nje, wakakimbia kutoka kaburini; kwa maana wameingia tetemeko na ushangao; wala hawakumwambia mtu neno, maana waliogopa". Mk. 16:6-8. Baba Mtakatifu Francisko katika Mkesha wa Pasaka, tarehe 3 Aprili 2021 wakati wa mahubiri yake amefafanua maana ya ujumbe wa Pasaka wa kwenda Galilaya kwamba: Inawezekana kuanza maisha mapya yanayopata chimbuko lake kutoka kwa Mungu. Pili, Kristo Yesu amefufuka ni mzima na anaendelea kutembea bega kwa bega na waja wake. Tatu, Kristo Mfufuka anawapenda waja wake upeo na jinsi walivyo! Baba Mtakatifu anasema, wanawake walipigwa na butwaa na mshangao walipokuta jiwe limekwisha kuviringishwa na wao wakaingia na kuambiwa kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa, amefufuka na amewatangulia kwenda Galilaya. Huu ni mwaliko kwa wafuasi wa Kristo Yesu kwenda nao mjini Galilaya. Kwenda Galilaya maana yake ni kurudi tena katika historia ya maisha yao kama wafuasi wa Kristo, alipowaona, akawachagua na kuwatuma kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Galilaya ni mahali ambapo kwa mara ya kwanza walionja wema, huruma na upendo wa Kristo Yesu katika maisha yao. Wakamsikia akitangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na kutenda maajabu. Lakini mbele ya Fumbo la Msalaba, wakamkimbia na kumwacha peke yake, lakini kwa sasa amewatangulia Galilaya na anawaalika tena kumfuasa, ili kuanza tena upya, licha ya patashika nguo kuchanika Siku ya Ijumaa Kuu. Huu ndio mshangao wa huruma na upendo wa Kristo usiokuwa na kifani. Huu ni upendo unaofungua njia mpya licha ya mapungufu ya wafuasi wake. Kwenda mjini Galilaya maana yake ni kuchukua njia mpya na kutoka kaburini na kuanza mang’amuzi mapya ya maisha, tayari kupyaisha imani na urafiki wao wa Kristo Yesu ambaye kwa sasa ni mwandani wa safari ya maisha. Huyu si tena yule Kristo Yesu waliomjifunza kwenye Katekesi walipokuwa watoto wadogo. Ni mwaliko wa kuondokana na imani inayowatumbukiza katika mazoea, bali imani iliyopyaishwa, inayo mchangamotisha mwamini kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Hii ni njia ya kujiaminisha kwa Kristo Yesu katika hali ya unyenyekevu, tayari kushangazwa na njia za Mwenyezi Mungu. Mwaliko wa kwenda Galilaya ni fursa ya kukutana na Mwenyezi Mungu aliye hai. Kristo Mfufuka, bado ataendelea kuwashangaza wafuasi wake.

Maana ya Pili ya kwenda Galilaya ni kupyaisha uelewa wa waamini juu ya Kristo Yesu anayeishi, na hivyo kuendelea kuwa ni mwandani wa maisha, kwa imani na matumaini ya upya wa maisha. Mji wa Galilaya ulikuwa pembezoni mwa jamii. Kwa mshangao mkubwa anasema Baba Mtakatifu Francisko, Kristo Yesu alianza kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu pembezoni mwa jamii, ili kuonesha kwamba, watu wote wanakumbatiwa na Mwenyezi Mungu na wala hakuna aliyesahauliwa na kusukumwa pembezoni mwa jamii. Kila mtu anayo fursa ya kuweza kupokea Neno na kukutana na Mwenyezi Mungu kwa njia ya ufunuo wa Kristo Yesu. Huu ni ujumbe mahususi kwa maskini, wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja na wale wote waliopondeka na kuvunjika moyo. Hakuna mtu aliyesahaulika mbele ya Mwenyezi Mungu. Kristo Yesu Mfufuka kwa mara nyingine tena, anawaita na kuwatuma wafuasi wake kwenda pembezoni mwa maisha na vipaumbele vya jamii, ili kuwashirikisha imani na matumaini. Kristo Yesu amewatangulia kati ya wafanyakazi wenzao, jirani na wale wote wanaokutana nao katika safari ya maisha.

Mjini Galilaya, wafuasi wa Kristo wataweza kukutana tena na ufunuo wa Uso wa Kristo Mfufuka kati ya watu waliokata tamaa; wale wanaofurahia maisha kutokana na neema na baraka za Mungu zilizowatembelea; watakutana na nyuso za watu wanaohuzunika katika maisha, lakini zaidi nyuso za maskini. Waamini watashangazwa, kuona jinsi ambavyo ukuu wa Mungu unavyofunuliwa katika mambo ya kawaida kabisa na kwamba, uzuri wake unang’aa kwenye nyuso za maskini na watu wa kawaida! Baba Mtakatifu anasema, kwenda Galilaya maana yake ni kumtambua Kristo Mfufuka, anayewapenda upeo katika kila hatua ya maisha yao! Huu ni mwaliko wa kuvunjilia mbali kuta za utengano zinazotokana na maamuzi mbele, ili kujenga ujirani mwema na hatimaye, kugundua neema ya Mungu katika maisha ya kila siku. Waamini wamtambue Mwenyezi Mungu katika Galilaya ya maisha yao kila siku. Kwa kuambatana na kushikamana na Mwenyezi Mungu, kwa hakika maisha yatabadilika tu!

Licha ya “patashika nguo kuchanika”, kuteleza na kuanguka katika dhambi na ubaya wa moyo; vita, ghasia, mateso na kifo, lakini Kristo Mfufuka bado anaendelea kuratibu historia ya maisha ya mwanadamu! Kwa wale wote wanaohisi kuzungukwa na giza nene katika maisha yao, bado hawajachelewa, wanachotakiwa ni kufungua nyoyo zao na kusikiliza ujumbe wa Pasaka “Msiogope kwa maana amewatangulia kwenda Galilaya”. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake kwa kusema, kwa hakika ndoto zao zitatekelezwa, machozi yao yatafutwa, hofu na mashaka yataondolewa na matumaini kushika mkondo wake. Kristo Yesu amewatangulia kwenda Galilaya na kwa kuwa pamoja na Kristo maisha yanapyaishwa!

Papa Kesha Pasaka

 

04 April 2021, 14:51