Tafuta

Jubilei ya Miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipomtangaza Mtakatifu Theresa wa Avila kuwa Mwalimu wa Kanisa 27 Septemba 1970. Jubilei ya Miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipomtangaza Mtakatifu Theresa wa Avila kuwa Mwalimu wa Kanisa 27 Septemba 1970. 

Miaka 50 Mt. Theresa wa Avila Kama Mwalimu wa Kanisa

Mtakatifu Theresa wa Avila Mwalimu wa Kanisa alibahatika kuwa na mwanga angavu wa hekima inayosimikwa katika utakatifu wa maisha, ukweli na imani thabiti Alikuwa na nguvu na upendo wa ajabu unaojionesha katika: Sala, Liturujia na Mafundisho yake, kiasi cha kujisikia kuwa pamoja na Kanisa, kama shuhuda na chombo cha upatanisho na mageuzi makubwa ndani ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mtakatifu Theresa wa Yesu, au maarufu kama Mtakatifu Theresa wa Avila, Bikira na Mwalimu wa Kanisa, mwanzoni kabisa kabisa alijulikana kama “Teresa de Cepeda y Ahumada” aliyezaliwa tarehe 28 Machi 1515 mjini Avila, nchini Hispania. Muasisi wa Shirika la Wakarmeli. Alifariki dunia tarehe 4 Oktoba 1582. Akatangazwa kuwa ni Mwalimu wa Kanisa na Mtakatifu Paulo VI, tarehe 27 Septemba 1970. Sifa kuu za Mtakatifu Theresa wa Avila kama Mwalimu wa Kanisa ni kwamba, ni mtawa aliyebahatika kuwa na mwanga angavu wa hekima inayosimikwa katika utakatifu wa maisha, ukweli na imani thabiti zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu. Mtakatifu Theresa wa Avila, alikirimiwa nguvu na upendo wa ajabu unaojionesha katika sala na maandiko yake. Kwa hakika alikuwa ni “mwanamke wa shoka katika maisha ya: Sala, Liturujia ya Kanisa na Mafundisho yake, kiasi cha kujisikia kuwa pamoja na Kanisa, kama shuhuda na chombo cha upatanisho na mageuzi makubwa ndani ya Kanisa. Utume wake katika maisha ya kiroho, ni amana na utajiri mkubwa kwa Kanisa unaowafanya waamini wote kujisikia kuwa ni sehemu ya watoto wa Mungu na Kanisa.

Kwa hakika anasema Mtakatifu Paulo VI, Theresa wa Avila ni kielelezo cha utukufu wa Kanisa nchini Hispania. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mtakatifu Theresa wa Yesu ni mwalimu wa maisha ya kiroho, aliyebahatika kuwafundisha watu wa Mungu namna nzuri zaidi ya kusali, kwa kujenga mahusiano na mafungamano ya ndani na Mwenyezi Mungu. Mara nyingi alijitenga na kujipatia muda binafsi wa kukaa mbele ya Mwenyezi Mungu, wakazungumzana kama watu wapendanao katika maisha. Mtakatifu Theresa wa Avila, Bikira na Mwalimu wa Kanisa ni mwanamke wa kwanza kutangazwa na Kanisa kuwa Mwalimu wa Kanisa. Maana yake ni kwamba kwanza kabisa, Kanisa linatambua amana na utajiri mkubwa unaobubujika kutoka katika Maandiko ya Mtakatifu Theresa wa Avila sanjari na ushuhuda wa maisha yake. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia ujumbe, Askofu mkuu José María Gil Tamayo wa Jimbo kuu la Avila, wakati huu, Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Avila, kinapoadhimisha Kongamano la Kimataifa, kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu Mtakatifu Theresa wa Avila atangazwe kuwa ni Mwalimu wa Kanisa. Kongamano hili limeanza tarehe 12 na linahitimishwa Alhamisi tarehe 15 Aprili 2021.

Kanisa linapoadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu Mtakatifu Theresa wa Avila atangazwe kuwa ni Mwalimu wa Kanisa, ameendelea kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa “kufyekelea” mbali kuta za aina mbalimbali ziwe ni za kimwili, kimaisha au kitamaduni. Amekuwa ni kati ya wanawake waliochangia sana katika historia ya maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Ujumbe wake una wito na mashiko; maisha yake ya kitawa ni mfano bora wa kuigwa na wote wanaotaka kujitakasa ili kamwe wasimezwe na malimwengu. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu anasema; Mtakatifu Theresa wa Avila alikuwa na ibada ya pekee sana kwa Mtakatifu Yosefu, ambaye kwake alikuwa ni Mwalimu wa maisha, wakili mwaminifu na mwombezi.

Daima alikuwa na uhakika kwamba, kwa maombezi ya Mtakatifu Yosefu, Mwenyezi Mungu angeweza kumkirimia neema na baraka alizokuwa anahitaji katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Mtakatifu Theresa wa Avila alipotangazwa kuwa ni Mwalimu wa Kanisa kwa kusema kwamba, Mtakatifu Theresa wa Avila ni kiongozi na mwandani katika hija ya maisha ya hapa duniani. Ni kielelezo cha amani, usalama na utulivu wa ndani.

Mwalimu wa Kanisa

 

14 April 2021, 14:32