Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameungana na viongozi wa kidini kutoka nchini Ugiriki tarehe 16 Aprili 2016 walitembelea Kisiwa cha Lesvos la Kambi ya Wakimbizi ya Moria nchini Ugiriki. Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameungana na viongozi wa kidini kutoka nchini Ugiriki tarehe 16 Aprili 2016 walitembelea Kisiwa cha Lesvos la Kambi ya Wakimbizi ya Moria nchini Ugiriki. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Ugiriki: Wakimbizi & Wahamiaji

Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameungana na Patriaki Bartolomeo wa kwanza pamoja na Askofu mkuu Jerome II, Jumamosi, tarehe 16 Aprili 2016 baada ya kukutana na kusalimiana na wananchi wanaoishi katika Bandari la Lesvos, nchini Ugiriki, walisali kwa pamoja ili kuwaombea wakimbizi na wahamiaji waliofariki dunia wakiwa njiani kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko alikubali na kupokea mwaliko kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol pamoja na Rais Paulopoulos wa Jamhuri ya Watu wa Ugiriki na hivyo akaamua kutembelea Kisiwa cha Lesbos, Jumamosi tarehe 16 Aprili 2016. Baba Mtakatifu akiwa Kisiwani hapo, alijiunga na Patriaki Bartolomeo wa kwanza na Askofu mkuu Jerome II wa Kanisa la Athens na Ugiriki nzima kukutana na kuzungumza na wakimbizi wanaohifadhiwa Kisiwani hapo! Hija hii ya kitume ya kumi na tatu kimataifa, ulikuwa ni mwendelezo wa mshikamano wa huruma na mapendo kwa wakimbizi na wahamiaji; maskini na wale wote wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na sababu mbali mbali. Huu ni mwendelezo wa hija za kitume ambazo Baba Mtakatifu Francisko amefanya huko Tirana, Albania, Uturuki, Sarayevo, Bosnia na Erzegovina na Jumuiya ya Ulaya. Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameungana na Patriaki Bartolomeo wa kwanza pamoja na Askofu mkuu Jerome II, Jumamosi, tarehe 16 Aprili 2016 baada ya kukutana na kusalimiana na wananchi wanaoishi katika Bandari la Lesvos, nchini Ugiriki, walisali kwa pamoja ili kuwaombea wakimbizi na wahamiaji waliofariki dunia wakiwa njiani kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi!

Baba Mtakatifu Francisko alisema kwa bahati mbaya makaburi ya watu hawa hayana majina wala kumbukumbu yoyote, lakini ni watu wanaofahamika na kupendwa na Mungu na kwamba, kamwe hatawasahauliwa; wakumbukwe kwa sadaka na matendo yao ya kijasiri na wala si maneno matupu! Baba Mtakatifu aliwakumbuka na kuwaombea wale wote walijitosa katika safari ya kutafuta usalama na maisha bora zaidi, kwa kuvumilia woga, wasi wasi, nyanyaso na dhuluma na hatimaye, wakafika bandari salama. Mwenyezi Mungu kamwe hawezi kuwasahau watoto wake kama alivyofanya kwa Mtoto Yesu na Familia Takatifu kwa kuwapatia hifadhi salama; kwa sasa awe karibu na kuwalinda watu wanaoteseka, ili kwa kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, Jumuiya ya Kimataifa ijikite zaidi katika kudumisha misingi ya uhuru, utu na amani na kamwe asiwepo mtu anayelazimika kukimbia makazi yake kwa lazima! Baba Mtakatifu alimwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwasaidia watu kuondokana na utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu, bali waoneshe jicho la upendo na kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, tayari kushirikishana karama za zawadi mbali mbali kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kama familia moja ya binadamu. Baba Mtakatifu alikumbusha kwamba, binadamu wote ni wasafiri kuelekea kwenye makao ya milele ambako, kila chozi litafutwa, amani na usalama vitadumishwa milele!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza katika sala yake aliombea lishe kwa watoto wadogo, elimu kwa vijana, nguvu kwa watu wazima; ujasiri kwa wale waliokata tamaa, mshikamano kwa wale waliotengana na wenzi wao; aendelee kusafiri na wasafiri wote; awalinde na kuwasimamia wajane na yatima; awafungulie wafungwa na kuwaponya wagonjwa. Aliwaombea na kuwakumbuka watu wanaoishi ugenini, katika mazingira magumu na hatarishi; wanaohitaji msaada na wale waliokata tamaa na hasa zaidi wale wanaokimbilia wema na huruma ya Mungu. Wote hawa waweze kumiminiwa huruma na kupata wokovu! Amewaombea wale wote waliolala katika usingizi wa amani wakiwa njiani kutoka katika maeneo ya vita, kuelekea katika nchi ya usalama, amani na maendeleo. Alimwomba Mungu awasaidie wasiokuwa na matumaini, wanaoteseka kutokana na safari ngumu na awe ni tabibu wa wagonjwa na awe yote kwa wote wanaomtumainia kutoka katika maeneo yaliyokumbwa na majanga asilia, vita na mipasuko ya kijamii! Askofu mkuu Jerome II alimwomba Mwenyezi Mungu aliyeonesha ukuu dhidi ya nguvu ya Shetani na kifo, awajalie maisha ya uzima wa milele wale wote waliotangulia kwenye usingizi wa amani; malisho mabichi na utulivu, mbali kabisa na machungu na magumu ya maisha ambayo walikuwa wanayakimbia. Awasamehe dhambi za ona kuwaonesha uzuri na wema wake usiokuwa na mipaka, kwani Mungu ni mwema na sheria yake ni ukweli na kwamba, ni chemchemi ya ufufuko wa wafu.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox katika hotuba yake kwa wahamiaji na wakimbizi wanaohifadhiwa kwenye Kambi ya Moria, Lesvos nchini Ugiriki, Jumamosi, tarehe 16 Aprili 2016 aliwahakikishia wakimbizi hawa kwamba viongozi wa Makanisa wamefika kisiwani hapo ili kuwakumbusha kwamba, bado hawajasahaulika na kwamba, wanataka kuwaonesha mshikamano na ushirikiano kwa wananchi wa Ugiriki walionesha ukarimu na huduma ya upendo kwa wakimbizi na wahamiaji tangu walipowasili visiwani humo! Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema Mwenyezi Mungu ni kimbilio, nguvu na msaada wa watu wake na kamwe hawataogopa. Viongozi wa Makanisa wanatambua kwamba, hawa ni watu waliotoka katika maeneo ya vita, njaa na mateso makali na kwamba, wana machungu sana kuhusu familia zao. Hawa ni watu wanaotafuta usalama na maisha bora zaidi. Viongozi wa Makanisa walihuzunika na kusikitika sana walipoona tumbo la Bahari ya Mediterrania linageuka kuwa ni kaburi la wakimbizi na wahamiaji. Wameshuhudia upendo na ukarimu wa wananchi wa Lesvos na visiwa vya jirani, lakini pia wameshuhudia mioyo migumu ya ndugu zao, wakifunga mipaka na kwenda zao bila kuguswa na mahangaiko ya jirani zao! Hawa ni watu ambao hawakuthubutu kuwaangalia mahoni, nyuso wala watoto wao: ni watu ambao wamesahau utu na uhuru na matokeo yake wamemezwa na hofu pamoja na migawanyiko na kusahau kwamba, uhamiaji ni changamoto ya kimataifa!

Patriaki Bartomeo wa kwanza alikaza kusema, walimwengu watahukumiwa kwa jinsi ambavyo wamewatendea wakimbizi na wahamiaji na kwamba, watawajibika kwa jinsi wanavyoshughulikia migogoro, kinzani na vita katika maeneo wanamotoka wakimbizi na wahamiaji hawa. Bahari ya Mediterrania lisiwe ni kaburi ya watu, bali mahali pa maisha panapowakutanisha watu wa tamaduni na staarabu mbali mbali; mahali pa kukutana na kujadiliana. Bahari inapaswa kuwa ni mahali pa salama! Migogoro, kinzani na vita huko Mashariki ya Kati ni chanzo kikuu cha wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi, amani na usalama vikirejeshwa huko, changamoto hii itakoma. Viongozi wa Makanisa wanasali ili haki za Wakristo na makundi ya watu wachache waendelee kukaa huko Mashariki na wala wasitoweke na kutoweka katika ramani ya dunia. Viongozi wa Makanisa wamewahakikishia wakimbizi na wahamiaji kwamba, kamwe hawatawasahu, wataendelea kuwatetea na kwamba, wataendeleza mchakato wa amani! Bara la Ulaya linapaswa kulitambua hili kuliko Mabara mengine yote, iko siku amani na utulivu vitarejea kati ya watu!

Kwa upande wake, Askofu mkuu Jerome II, Mkuu wa Kanisa la Athens na Ugiriki nzima amesema, uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko utasaidia kuvuta hisia za Jumuiya ya Kimataifa ili kuaangalia na hatimaye, kuguswa na mahangaiko pamoja na mateso ya wakimbizi na wahamiaji. Viongozi wa Makanisa kwa kauli moja wana laani vikali vitendo vyote vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Uwepo wa viongozi hawa Kisiwani Lesvos uwe ni mwanzo wa mageuzi yatakayosaidia amani nau salama kwa wananchi wote. Wahusika wote wanaosababisha mateso haya wanapaswa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ili kukomesha nyanyaso na dhulumu dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Mateso na mahangaiko ya watoto wasiokuwa na hatia ni kielelezo cha kufilisika kwa utu na ubinadamu; mshikamano na upendo kutoka Barani Ulaya. Askofu mkuu Jerome II aliwashukuru na kuwapongeza wananchi wa Ugiriki kwa kuonesha mshikamano wa huruma na upendo; kwa kusaidia kubeba Msalaba wa matumaini wakimbizi na wahamiaji wanaoelekea kwenye Mlimani Kalvari. Kanisa linaendelea kuwalilia wale wote wanaopoteza maisha kwa kufa maji baharini. Kanisa litaendelea kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji kadiri ya uwezo wake na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa iwajibike kikamilifu katika kuwasaidia wahanga wa matukio haya. Ni matumaini ya Askofu mkuu Jerome II kutoona tena maiti za watoto wachanga zikielea kwenye ufuko wa bahari, bali watoto wakiwa na nyuso za furaha, huku wakifurahia zawadi ya maisha ya utotoni!

Wakimbizi Ugiriki

 

15 April 2021, 15:15