Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil linamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa moyo na ukaribu wake wa kibaba kwa watu wa Mungu nchini Brazil wanaopambana na UVIKO-19. Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil linamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa moyo na ukaribu wake wa kibaba kwa watu wa Mungu nchini Brazil wanaopambana na UVIKO-19. 

Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil: Mafundisho ya Papa Francisko

Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil linamshukuru Papa Francisko kwa uwepo wake wa kibaba hasa katika kipindi hiki ambacho Brazil inapambana na janga la UVIKO-19. Baba Mtakatifu ameendelea kulichangamotisha Kanisa kujenga umoja na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, ili ulimwengu uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, Cnbb, tangu Jumatatu tarehe 12 hadi 16 Aprili 2021 linafanya mkutano wake wa 58 kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Kwa namna ya pekee, Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil linamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa uwepo wake wa kibaba kwa watu wa Mungu nchini Brazil hasa katika kipindi hiki ambacho Brazil inapambana kufa na kupona na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Baba Mtakatifu ameendelea kulichangamotisha Kanisa kujenga umoja wa Kanisa sanjari na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, ili ulimwengu uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Maaskofu wamegusia kuhusu hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq, kuanzia tarehe 5 – 8 Machi 2021 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Hija hii ilifumbata mambo makuu matatu: Ukaribu wa Baba Mtakatifu kwa Wakristo nchini Iraq, kuhamasisha ujenzi wa Iraq mpya katika haki na usawa na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene ili kudumisha udugu wa kibinadamu.

Maaskofu wanamshukuru Baba Mtakatifu kwa Waraka wake wa Kitume wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” unatoa dira na mwongozo wa kuweza kufikia: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa watu kutambuana kwamba, wao ni ndugu wamoja na wanahamasishwa kutegemezana na kusaidiana, kwani wote wako ndani ya mashua moja! Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu akisema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa busara na haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa na Malaika katika ndoto!

Hii ni tafakari makini katika malezi na makuzi ya watu wa Mungu katika hatua mbalimbali za maisha! Maaskofu Katoliki nchini Brazil wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kutangaza na kuzindua Katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Miaka 5 tangu achapishe Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”. Katika maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2021, Mama Kanisa amezindua Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” utakaohitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani. Kilele cha maadhimisho haya mjini Roma ni tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”. Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” ulitiwa mkwaju, tarehe 15 Oktoba 2020. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa washiriki wa mkutano huu kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran kilichoko mjini Roma alikazia pamoja na mambo mengine kuhusu: Janga la elimu duniani, maana ya elimu, umuhimu wa kupyaisha mfumo wa elimu duniani na hatimaye, mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika maboresho ya mfumo wa elimu duniani!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Economy of Francesco” yaani “Uchumi wa Francisko” ni sehemu ya mbinu mkakati wa utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, ili kuweza kuzama zaidi katika uchumi unaohuisha na wala si ule unaowatumbukiza watu katika kifo. Uchumi fungamani unaojikita katika tunu msingi za utu na heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni uchumi unaojielekeza katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko anawataka kujikita katika mchakato wa kupyaisha uchumi na amani duniani. Zote hizi zinaonesha Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji katika Kanisa (Magisterium) ya Baba Mtakatifu Francisko. Maaskofu katika mkutano wao, wamejadili pia udhaifu wa Serikali katika kusimamia na kuratibu mapambano dhidi ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, mipasuko ya kisiasa na kijamii na umuhimu wa watu wa Mungu nchini Brazil kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo.

Maaskofu wamekazia kuhusu umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha ya waamini, ili waweze kuyafahamu Maandiko Matakatifu na hatimaye, kumfahamu Kristo Yesu. Wamtangaze na kumshuhudia kwa ari na mwamko mpya zaidi. Kanisa linataka kutangaza na kumshuhudia Kristo kuwa ni kiini cha maisha na wokovu wa walimwengu sanjari na kukabiliana na changamoto ya ekolojia fungamani. Utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele. Kiini cha maadhimisho ya Sinodi Amazonia kuanzia tarehe 6-27 Oktoba, 2019: Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani.” Maaskofu wanajiandaa pia kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya mkutano wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean CELAM unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba 2022. Kampeni ya Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2022 itaongozwa na kauli mbiu “Udugu na Elimu”.

Maaskofu Brazil

 

 

 

15 April 2021, 16:28