Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu mstaafu Felix del Blanco Prieto ni kiongozi aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya diplomasia ya Kanisa na huduma kwa maskini, amana na utajiri wa Kanisa. Askofu mkuu mstaafu Felix del Blanco Prieto ni kiongozi aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya diplomasia ya Kanisa na huduma kwa maskini, amana na utajiri wa Kanisa.  (Vatican Media)

Askofu mkuu Felix del Blanco Prieto: Huduma Kwa Maskini

Askofu mkuu Felix del Blanco Prieto, Mtunza Sadaka ya Kipapa Mstaafu, aliyewahudumia maskini kwa ari na moyo wa unyenyekevu wakati wa uongozi wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, amefariki dunia tarehe 10 Aprili 2021 kwenye Hospitali ya Gemelli akiwa na umri wa miaka 83 ya kuzaliwa. Ibada ya Misa imeongozwa na Kardinali Parolin na kuhudhuriwa na Papa Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Nasadiki kwa Ufufuko wa wafu: Kanisa lina amini na kutumaini kwa uthabiti kabisa kama vile Kristo Yesu alivyoteswa, akafa na kufufuka kwa wafu na anaishi daima, vivyo hivyo wenye haki baada ya kifo chao, wataishi daima na Kristo Yesu Mfufuka, naye atawafufua siku ya mwisho. Ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele ni kazi ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Neno mwili, linamwelezea mwanadamu katika hali yake ya udhaifu! Askofu mkuu Felix del Blanco Prieto, Mtunza Sadaka ya Kipapa Mstaafu, aliyewahudumia maskini kwa ari na moyo wa unyenyekevu wakati wa uongozi wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, amefariki dunia, hapo tarehe 10 Aprili 2021 kwenye Hospitali ya Gemelli akiwa na umri wa miaka 83 ya kuzaliwa. Ibada ya mazishi, imeongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Alhamisi tarehe 15 Aprili 2021 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kuhudhuriwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa faragha. Askofu mkuu Felix del Blanco Prieto, Mtunza Sadaka ya Kipapa Mstaafu alizaliwa tarehe 15 Juni 1937 huko Mogrovejo, Castilla y León, nchini Hispania.

Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 27 Mei 1961 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Balozi wa Vatican na kumpandisha hadhi ya kuwa Askofu mkuu na kuwekwa wakfu kuwa Askofu mkuu hapo tarehe 6 Julai 1991. Tangu wakati huo alifanya utume wake wa Diplomasia ya Kanisa nchini Angola, Sao Tome na Principe. Cameroon na Equatorial Guinea, Malta na Libya. Tarehe 28 Julai 2007, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Mtunza Sadaka ya Kipapa hadi tarehe 3 Novemba 2012 alipong’atuka kutoka madarakani. Tarehe 10 Aprili 2021 akiwa na umri wa miaka 83 akaitupa mkono dunia. Maskini ni hazina, amana na utajiri wa Kanisa, hawa ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu. Matendo ya huruma ndicho kigezo kikuu ambacho Kristo Yesu atakitumia Siku ya Hukumu ya Mwisho.

Waamini wawe makini dhidi ya uchu wa mali na madaraka, mambo ambayo yanaweza kuhatarisha hata maisha yao ya kiroho na kujikuta wametumbukia katika kiburi, ubinafsi na hatimaye, kumezwa na malimwengu. Lakini, ikumbukwe kwamba, haya ni mapambano endelevu katika maisha ya kiroho! Hakuna kulala hadi kieleweke! Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Hayati Askofu mkuu Felix del Blanco Prieto, aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya huduma kwa Kanisa kama mwanadiplomasia na mtunza sadaka ya Kipapa. Kwa njia ya huduma hii, aliweza kukutana na kuzungumza na maskini, akakisikiliza na kujibu kilio chao kadiri ilivyowezekana, kwa niaba ya Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii ni zawadi ya maisha inayopokelewa kwa moyo wa shukrani na kutumika kwa ajili ya huduma ya upendo kwa maskini. Hayati Askofu mkuu Felix del Blanco Prieto katika maisha na utume wake, alibahatika kukutana na watu wa kila aina kutoka katika tamaduni na mazingira mbalimbali.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, anakaza kusema, alijitahidi kuwa ni chombo na shuhuda wa upendo, huruma, uvumilivu na utambuzi kwa jirani zake. Alijitahidi kutangaza ukweli, akajikita kutafuta: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kuwaheshimu na kuwathamini watu; mambo ambayo yanapata chimbuko lake katika Injili ya upendo na amani, mambo msingi katika diplomasia ya Vatican. Hayati Askofu mkuu Felix del Blanco Prieto ameacha ukumbusho wa kudumu katika maisha na utume wake kwa Kanisa. Alizamisha maisha yake kutafuta kwanza ufalme wa Mungu na mengine yote angepewa kwa ziada. Alikuwa mwaminifu na mwadilifu katika kutekeleza dhamana na majukumu yake. Akajiaminisha kwa Mungu hata nyakati za mateso, mahangaiko ya ndani pamoja na mateso wakati wa uzee na ugonjwa wake.

Maombolezo

 

17 April 2021, 15:05