Tafuta

Vatican News
Askofu mteule Christian Carlassare alivamiwa na majambazi na kupigwa risasi, akakimbizwa Nairobi kwa matibabu zaidi. Taarifa za kitabibu zinabainisha kwamba, kwa sasa anaendelea vyema. Askofu mteule Christian Carlassare alivamiwa na majambazi na kupigwa risasi, akakimbizwa Nairobi kwa matibabu zaidi. Taarifa za kitabibu zinabainisha kwamba, kwa sasa anaendelea vyema. 

Askofu Mteule Christian Carlassare Apigwa Risasi, Alazwa Nairobi!

Tarehe 8 Machi 2021 Baba Mtakatifu Francisko alimteuwa Padre Christian Carlassare kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Rumbek , nchini Sudan ya Kusini na alitarajiwa kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 23 Mei 2021, wakati wa Sherehe ya Pentekoste. Jimbo la Rumbek limekuwa wazi tangu mwezi Julai 2011 baada ya kifo cha ghafla cha Askofu Cesare Mazzolari. Amewasamehe wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na shambulio lililofanywa dhidi ya Askofu mteule Christian Carlassare MCCJ, mwenye umri wa miaka 43 wa Jimbo Katoliki la Rumbek, Sudan ya Kusini, usiku wa kuamkia, Jumapili tarehe 25 Aprili 2021; Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji mwema! Tarehe 8 Machi 2021 Baba Mtakatifu alimteuwa Padre Christian Carlassare kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Rumbek na alitarajiwa kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 23 Mei 2021, wakati wa Sherehe ya Pentekoste. Jimbo la Rumbek limekuwa wazi tangu mwezi Julai 2011 baada ya kifo cha ghafla cha Askofu Cesare Mazzolari. Taarifa za kitabibu zinaonesha kwamba, kwa sasa hali yake inaendelea vyema baada ya kusafirishwa kwenda Jijini Nairobi, Kenya kwa matibabu zaidi.

Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu amemtumia salam na matashi mema Askofu mteule Christian Carlassare MCCJ, ili kuonesha ukaribu na mshikamano wa Vatican na Kanisa zima katika kipindi hiki kigumu ambacho anapitia kwa sasa katika maisha na utume wake. Kwa upande wake, Rais Salva Kiir wa Sudan ya Kusini amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa haraka, ili kuwabaini waliohusika, waweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Serikali ya Sudan ya Kusini, haitaruhusu amesema Rais Salva Kiir kuona watu wachache wakilihujumu Kanisa, ili lishindwe kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuwahudumia watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini. Watuhumiwa 24 tayari wamekwisha kukamatwa kuhusiana na shutuma za kumvamia na kumjeruhi Askofu mteule Christian Carlassare MCCJ.

Kwa upande wake, Askofu mteule Christian Carlassare MCCJ amesema kwamba, kutoka katika undani wa moyo wake, amewasamehe wale waliompiga risasi. Na kutoka katika sakafu ya moyo wake, anawaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali kwa ajili ya watu wa Mungu Jimboni Rumbek, wanaoteseka zaidi yake kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo imekuwa ni kikwazo cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Amepata nafasi ya kuzungumza na Mama yake Marcellina ambaye ameshutumu biashara haramu ya silaha inayoendelea kupandikiza utamaduni wa kifo sehemu mbalimbali za dunia.

Hizi ni silaha zinazotengezwa katika Nchi zilizoendelea zaidi duniani. Mama Marcellina anasema, inafaa kukesha na kusali, lakini ni vyema zaidi, ikiwa kama viwanda vya kutengenezea silaha vitageuzwa kuwa ni viwanda vya kutengenezea amani duniani. Kwa bahati mbaya sana, wataalam wanatumia rasilimali watu na vitu na maendeleo makubwa ya teknolojia kwa ajili ya kutengenezea silaha na hivyo kupandikiza utamaduni wa kifo. Silaha hizi badala ya kusababisha maangamizi kwa watu na mali zao anasema, Mama Marcellina zigeuzwe na kuwa ni chemchemi ya Injili ya uhai na matumaini kwa watu waliopondeka na kuvunjika moyo. Tangu mwaka 2013 hadi mwaka 2018, Sudan ya Kusini imekuwa katika vita ya wenyewe kwa wenyewe kutokana na uchu wa mali na madaraka. Sudan ya Kusini ilijipatia uhuru wake kunako mwaka 2011 na wengi wakadhani kwamba, mwanga wa matumaini ulikuwa umeanza kuchomoza, lakini kufumba na kufumbua, Sudan ya Kusini, ikajikuta ikitumbukia katika vita!

Sudan Kusini
27 April 2021, 14:54